Habari za Punde

RC Chalamila Aipongeza TRA Kwa Kuongoza Ukusanyaji Mapato.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Albert Chalamila akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani hapa na kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. Lengo la kikao hicho ni kutathmini utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na kujadili mikakati mipya kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020/21.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede akizungumzia mafanikio ya TRA katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya awamu ya tano wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya na kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. Katika kipindi hiki cha miaka mitano, makusanyo yameongezeka kutoka shilingi trilioni 10.67 mwaka wa fedha 2014/15 hadi kufikia shilingi trilioni 17.87 mwaka wa fedha 2019/20.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakifuatilia kwa makini hafla fupi ya uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya na kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. Lengo la kikao hicho ni kutathmini utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na kujadili mikakati mipya kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020/21.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya na kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. Lengo la kikao hicho ni kutathmini utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na kujadili mikakati mipya kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020/21.
Baadhi ya Mameneja na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Albert Chalamila (wa tatu kulia) mara baada ya uzinduzi wa kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani hapa na kitahitimishwa tarehe 6 Septemba, 2020. PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO - MBEYA.

Na Veronica Kazimoto Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha miaka mitano ambapo makusanyo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka shilingi trilioni 10.67 mwaka wa fedha 2014/15 hadi kufikia shilingi trilioni 17.87 mwaka wa fedha 2019/20.

Akizindua kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kinachofanyika mkoani Mbeya, Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa, Serikali hutumia mapato hayo kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.  

Amesema ufanisi huo unaipa moyo ofisi yake na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na TRA katika kuhamasisha wananchi kulipa kodi kwa hiari kwa manufaa mapana ya nchi. Pia, ametoa rai kwa wakwepaji kodi na kusema kuwa, Serikali itashughulika nao kwani wanahatarisha ustawi wa nchi.

Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Dk. Edwin Mhede, amesema makusanyo hayo ni ongezeko la kutoka wastani wa sh. bilioni 850 zilizokuwa zinakusanywa kwa mwezi wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani hadi kufikia wastani wa sh. trilioni 1.5 kwa mwezi sasa hivi ikiwa ni ongezeko la asilimia 76 kwa mwezi.

Ameeleza kuwa, ongezeko hilo la makusanyo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na jitihada za serikali ya awamu ya tano katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi, kuhamasisha matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti na kudhibiti nidhamu na uadilifu kwa watumishi wa TRA.  

“Pia miradi mikubwa ambayo inatekelezwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia mapato ya ndani imekuwa ni chachu ya kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kwa kuwa walipakodi wanaona thamani ya kodi wanayolipa,” amesema Dkt. Mhede.

Dkt. Edwin Mhede amesema kwamba, Mamlaka hiyo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha watumishi wake wanafanya kazi kwa uadilifu na uwajibikaji. Katika kuhakikisha kuwa suala la maadili linazingatiwa, TRA imeunda idara maalum inayosimamia maadili na uadilifu wa watumishi hao.

Kikao kazi hicho cha tathmini ya utendaji kazi wa Idara ya Kodi za Ndani kimehudhuriwa na washiriki wapato 150 ambapo miongoni mwao ni Mameneja wa TRA wa mikoa na baadhi ya mameneja wa wilaya kutoka nchini kote na kikao hiki kinategemea kumalizika tarehe 6 Septemba, 2020.

Lengo la kikao hicho ni kutathmini utendaji kazi wa idara hiyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 na kujadili mikakati mipya ya mwaka wa fedha 2020/21 kwa ajili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.