Na Jovina Bujulu-MAELEZO\
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), ni chombo chenye mamlaka kisheria ya kuratibu na kusimamia
Uchaguzi Mkuu na Chaguzi ndogo ambacho ambayo ilianzishwa rasmi Januari 13,
1993, chini ya Ibara ya 74 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977.
NEC katika kutekeleza
majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya kuwa chombo kinachoaminika katika
kusimamia uchaguzi Afrika huku kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, ugawaji wa
majimbo na utoaji wa elimu ya mpiga kura
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuimarisha demokrasia.
Pamoja na majukumu
mengine ya NEC, pia inasimamia maadili ya uchaguzi ambayo ni makubaliano ya
pamoja baina ya Vyama vya Siasa, Serikali pamoja na Tume yenyewe. Maadili haya
hueleza mambo yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanywa katika mchakato wa
uchaguzi, wakati wa kampeni za uchaguzi, upigaji kura na kutangaza matokeo ya
uchaguzi.
Aidha, maadili ya
uchaguzi yanahusu kuheshimiana, kuzingatia ratiba ya kampeni, kuelimisha
wanachama wa vyama katika misingi ya kuelewa sera za vyama husika, kutojenga
chuki, kushirikiana na kutobeba silaha za aina yoyote katika mikutano ya
kampeni.
Katika kutekeleza
maadili haya, Msimamizi wa Uchaguzi au Msimamizi Msaidizi ngazi ya Kata
anatakiwa kutekeleza zoezi la kusimamia na kuendesha uchaguzi kwa mujibu wa
sheria, kanuni, taratibu na maelekezo ya Tume kwa kuzingatia uwazi na uadilifu.
Hivyo, Vyama vya Siasa vinawajibu wa kuzingatia Kanuni na Maadili ya Uchaguzi
ya mwaka 2020 ili kuepuka madhara yanayoweza kusababisha kuharibika kwa
mchakato wa Uchaguzi.
Ili kuhakikisha maadili
haya yanatekelezwa, Msimamizi wa Uchaguzi au Msimamizi Msaidizi ngazi ya Kata anawajibu
wa kuunda kamati za maadili katika ngazi ya Jimbo na Kata baada ya kupata
maelekezo kutoka Tume na atatakiwa kuvitaarifu Vyama vya Siasa, Serikali na kuwasilisha
majina ya wajumbe siku saba kabla ya siku ya uteuzi.
Kamati zitakazoundwa ni
pamoja na Kamati ya Maadili ngazi ya Kata, Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, Kamati ya Maadili ngazi ya
Taifa, na Kamati ya Maadili ya Rufaa,
ambapo majukumu ya kamati hizo ni kusimamia na kushughulikia malalamiko
yanayotokana na ukiukwaji wa maadili wakati wa kampeni za uchaguzi kuanzia hatua
ya kuanza kampeni hadi kukamilika kwake.
Kila kamati itakuwa na
mwenyekiti na wajumbe ambao watatokana na aina ya kamati, kwa mfano Kamati ya Maadili
ya Kata itakuwa chini ya uenyekiti wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya
Kata na wajumbe ni mwanachama mmoja kutoka kila chama cha siasa chenye mgombea
udiwani na mwakilishi wa Serikali
aliyeteuliwa na Katibu Tawala wa Wilaya.
Kwa upande wa Kamati ya
Maadili ngazi ya Jimbo, mwenyekiti wake atakuwa ni Msimamizi Msaidizi, ngazi ya
Jimbo na wajumbe wake ni mwanachama mmoja kutoka kwenye chama cha siasa chenye
mgombea wa ubunge na mwakilishi wa Serikali aliyeteuliwa na Katibu Tawala wa
Wilaya.
Kamati nyingine ni ya Kamati
ya Maadili ngazi ya Taifa ambayo Mwenyekiti wake ni mjumbe yoyote wa Tume
atakayeteuliwa na Tume ambapo wajumbe watakuwa ni mwanachama mmoja kutoka
kwenye chama cha siasa chenye mgombea wa kiti cha Rais na mwakilishi wa
Serikali aliyeteuliwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Fauka ya hayo, pia ipo
kamati ya Maadili ya Rufaa ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi. Wajumbe wa kamati hii ni mwanachama mmoja kutoka kwenye Chama cha
Siasa chenye mgombea wa Kiti cha Rais na Mwakilishi wa Serikali aliyeteuliwa na
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa mwongozo
wa elimu ya mpiga kura uliotolewa na NEC, umeainisha baadhi ya matukio ya
ukiukwaji wa maadili kuwa ni pamoja na matumizi ya lugha za kashfa na matusi
kwa wagombea na viongozi wa Vyama vya Siasa wakati wa kampeni, kuzidisha muda
wa kampeni, kukiuka ratiba ya kampeni, maandamano ya wafuasi wa Vyama vya Siasa
yasiyokuwa na kibali cha Jeshi la Polisi kabla na baada ya kampeni, wafuasi wa
vyama kuharibu mabango ya wagombea wa vyama vingine, kubandika picha za
wagombea juu ya picha za wagombea wengine, wafuasi wa vyama na wagombea
kuingilia mikutano ya wagombea wa vyama vingine pamoja na kutoa kauli
zisizoweza kuthibitishwa.
Kwa mujibu wa Sheria ya
Uchaguzi Kifungu cha 46 (1) , Sura ya 343
na Kifungu cha 53 (1) cha Sheria ya Uchaguzi yaSerikali za Mitaa, Sura
ya 292. kipindi cha kampeni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani hutangazwa
na NEC ambapo kampeni zitaanza siku moja baada ya siku ya uteuzi na kumalizika
siku moja kabla ya siku ya Uchaguzi.
Aidha, Kanuni ya 40
(1-5) na 41 (1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020
zinaeleza kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ndiye ataratibu ratiba ya kampeni za
Uchaguzi wa Kiti cha Rais na atavitaka Vyama vya Siasa vinavyoshiriki Uchaguzi
wa Rais kuwasilisha ratiba za kampeni siku saba kabla ya siku ya uteuzi.
Hakika ratiba ni
muongozo unaosaidia wagombea kutokuingiliana katika kampeni zao wakati wa
kampeni, hivyo, mambo muhimu yakuzingatia
wakati wa uandaaji wa ratiba zao ni pamoja na tarehe, muda, mkoa, wilaya na
mahali ambapo mgombea atafanya kampeni zake na Mkurugenzi wa Uchaguzi akipokea
mapendekezo ya ratiba za kampeni kutoka kwenye Vyama vya Siasa ataitisha
mkutano kwa ajili ya kuratibu ratiba hizo.
Kwa mujibu wa Kanuni ya
42 (1-5) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015, ratiba ya
Kampeni za Uchaguzi wa Ubunge zitaratibiwa na Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya
Jimbo ambapo kila Chama cha Siasa au Mgombea atapaswa kabla ya kuanza kampeni
kuandaa mapendekezo ya ratiba na kuiwasilisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi siku
saba kabla ya siku ya uteuzi.
Mratibu wa Kampeni za
Udiwani kwa mujibu wa Kanuni ya 35 (1-5) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa za mwaka 2020 ni Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata, ambapo
kila Chama cha Siasa au Mgombea atapaswa kabla ya kuanza Kampeni kuandaa
mapendekezo ya ratiba ya kampeni na kuiwasilisha kwa Msimamizi Msaidizi wa
Uchaguzi ngazi ya Kata siku saba kabla ya siku ya uteuzi.
Uchaguzi utafanyika
Oktoba 28, mwaka huu 2020 ni wa sita tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini
mnamo mwaka 1992 ambapo Uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka 1995, ukifuatiwa na
Uchaguzi wa Mkuu wa mwaka 2000, 2005, 2010 na 2015.
No comments:
Post a Comment