Habari za Punde

MKURUGENZI WA HUDUMA ZA SHERIA WIZARA YA MAJI ATOA NENO KWA MAMENEJA WA RUWASA NCHINI

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji Simon Nkanyemka katikati akimsikiliza kwa umakini Mhandisi wa Miradi Tanga Uwasa Mhandisi Salum Ngumbi  kushoto akielezea mradi unaotoa maji Pongwe kuelekea Muheza wakati wa ziara hiyo katikati Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Geofrey Hilly na kulia ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo
MKURUGENZI wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji Simon Nkanyemka kushoto akiteta jambo na Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Geofrey Hilly wakati alipotembelea mradi wa maji wa kutoa maji Pongwe kwenda wilayani Muheza uliopo eneo la Kilapula Jijini Tanga wakati wa ziara yake katikati ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo
MKURUGENZI wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji Simon Nkanyemka wa pili kutoka kulia aliyevaa shati jeupe kuwa na Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Geofrey Hilly wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wengine wakati wa ziara  ya siku mbili ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji pamoja na kubaini changamoto zake .
MENEJA wa Ruwasa wilaya ya Lushoto Eron Sizinga akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo kulia ni MKURUGENZI wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji Simon Nkanyemka
MKURUGENZI wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji Saimon Nkanyemka kulia akisistiza jambo katika mradi wa maji wa Shume-Manolo-Madala wilayani Lushoto wakati wa ziara yake  ya siku mbili ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji pamoja na kubaini changamoto zake mkoani Tanga wa kwanza kushoto aliyevaa chekundu ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo akifuatiiwa na Meneja wa Ruwasa wilaya ya Lushoto Eron Sizinga
MKURUGENZI wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji Saimon Nkanyemka aliyevaa shati jeupe na suruali nyeusi katika akimsikiliza Meneja RUWASA Wilaya ya Korogwe, Sifael Massawe akimueleza jambo wakati alipotembelea chanzo cha maji 

MKURUGENZI wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji Simon Nkanyemka amewashauri mameneja wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) kote nchini kwenda vijijini kutoa elimu kwa jamii umuhimu wa uchangiaji wa huduma za maji kama inavyoelekeza sheria ya maji namba 5 ya mwaka 2019.

Saimon alitoa ushauri huo jwilayani Muheza wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku mbili ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji pamoja na kubaini changamoto zake .

Alisema sheria ya Maji namba 5 ya 2019 inaeleza wazi kuwa miradi ya maji vijijini inatakiwa kuendeshwa na wataalamu waliosoma kupitia bodi za maji ikiwemo wananchi kuchangia huduma ili miradi iweze kuwa endelevu

“Hivyo kutokana na ziara yangu nimegundua wananchi wengi bado hawana uelewa juu ya sheria hii haswa katika suala la uchangiaji wa huduma haiwezekani kwa mwezi mtu analipa Sh 500 tu mameneja RUWASA nendeni kwenye miradi ya maji vijijini mkawaelimishe Wananchi”Alisema

Nkanyemka katika ziara hiyo aliambatana na Maofisa kutoka Bonde la Mto Pangani na  Mtaalamu wa Ubora wa Maji kutoka Wizara ya Maji pamoja na Meneja RUWASA mkoa wa Tanga,Upendo Lugongo alitembelea miradi ya maji katika wilaya za Korogwe,Lushoto na Muheza pamoja na kukagua chanzo cha maji cha bonde la Mto Zigi.

Akiwa wilayani Korogwe alitembelea mradi wa Maji wa Mtonga-Msambiazi  ambao unatoa huduma za maji katika vijiji vya Mtonga,Majengo na Msambiazi mradi ambao umegharimu fedha kiasi cha Sh milioni 595 ambapo changamoto aliyokumbana nayo ni mradi huo kukamilika lakini maji yanatoka kwa mgao kutokana  pampu kubwa iliyofungwa kwa ajili ya kusukumia maji haijaanza kazi kutokana Shirika la Umeme(Tanesco) wilayani humo haijafunga mita kubwa ya kuiwezesha pampu hiyo kufanya kazi.

Vile vile alitembelea kituo cha maji katika kijiji cha Msambiazi ambacho kinapata maji kupitia mradi huo huku akikutana na malalamiko ya wananchi kuyalalamikia maji hayo kuwa yana rangi hali ambayo wananchi wameamua kuyatumia maji hayo kwa shughuli nyingine za nyumbani lakini si kwa matumizi ya binadamu.

Kufuatia malalamiko hayo,Nkanyemka  alimuagiza Meneja RUWASA Wilaya ya Korogwe, Sifael Massawe kuhakikisha Tanesco wanafunga mita hiyo ili kuondoa kero ya mgao wa maji pamoja na kuwatoa  wananchi hofu kuwa maji hayo ni salama kwa matumizi ya binadamu na serikali itahakikisha kupitia wataalamu wa Wizara ya Maji wanaondoa rangi hiyo.

“Kupitia mradi  mkubwa wa  maji wa HTM ambao utatoa huduma za maji katika wilaya za Muheza,Handeni,Korogwe na Pangani kupitia chanzo cha mto Pangani ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwezi Novemba mwaka huu, kutawekwa mtambo wa kuchuja maji,hali hii haitajitokeza tena serikali haitakubali kuwaletea maji yasiyo salama,yaliyopo ni salama tatizo ni rangi tu lakini yamepitia hatua mbalimbali za kuchuja,”alisema.

Hata hivyo kwenye wilaya ya Lushoto alitemebea mradi wa maji wa Shume-Manolo-Madala ambao unahudumia vijiji sita katika kata ya Manolo jimbo la Mlalo na wananchi 35,000 alitembelea tenki la kuhifadhia maji na kituo cha maji katika kijiji cha Nyolwe ambapo alikumbana na wananchi kulalamika kupata maji kwa mgao na wananchi wanataka kuchangia huduma ya maji kwa gharama ya Sh 500 tu kwa mwezi kwa kila kaya.

Akizungumzia suala hilo,Meneja Ruwasa Wilaya ya Lushoto,Eron Sizinga alisema kuwa mradi huo una matenki mawili  na vituo 71 ambavyo vinahudumia katika vijiji sita,na maji hayo yanatoka kwa mgao kutokana bado mradi upo katika hatua ya majaribio ya mkandarasi haujakabidhiwa kwa uongozi wa RUWASA ndio maana maji yanatoka kwa mgao mara moja au mbili kwa wiki kwa kila kijiji.

Wilayani Muheza alitembelea mradi wa maji wa Mashekiwasa ambao unahudumia vijiji vitatu vya Kimbo, Mashewa na Shembekeza ambapo pia alikumbana na changamoto ya wananchi kugoma kulipia huduma hizo za maji zaidi ya Sh 500 kwenye vituo na Sh 1000 kwa wale waliounganishiwa huduma hadi nyumbani.

Katika hatua nyingine,amepongeza hatua ya uhifadhi wa chanzo cha maji katika mto Zigi kupitia mradi wa uhifadhi wa vyanzo vya maji katika mabonde ya Ruvu na Zigi na kusema kuwa matokeo ya uhifadhi huo ni mfano wa kuigwa katika vyanzo vingine vya maji.

Katika mradi huo,wananchi wanaoishi kandokando ya vyanzo vya maji wamepewa elimu ya kupanda mazao mbadala ambayo hayaharibu vyanzo vya maji ambapo wananchi wameweza kuzingatia na kutunza vyanzo hivyo ambapo kiwango cha maji katika mto Zigi kimeongezeka kutoka mita 4.3 hadi mita 6.5 katika kipindi cha miaka mitano tangu mradi uanze.

Mafanikio mengine ni kupungua kwa kiwango cha mchanga ndani ya mto kutoka kilo 1.4 kwa eneo la mita za mraba hadi kilo 0.49 kwa eneo la kilometa za mraba pamoja na kuinua kiwango cha maisha ya wananchi kupitia miradi mbadala ya kiuchumi  na kuongeza kwa uelewa kwa wananchi juu ya uhifadhi vyanzo vya maji.

Mradi huo wa uhifadhi vyanzo vya Maji katika Bonde la Mto Zigi na Ruvu umefadhiliwa na serikali ya Tanzania kwa fedha kiasi cha Sh bilioni 11 na wanadu wa maenedeleo ambao ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) na GEF ambao kwa pamoja wametoa Sh 16.5 bilioni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.