Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Amefungua Chuo Cha Amali cha Dayamtambwe Wilaya ya Wete Pemba leo 15/10/2020.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiondoa kipazia kuweka Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Chuo Cha Amali Dayamtambwe Wilaya ya Wetev Pemba leo 15/10/2020 na 9kulia kwa Rais) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma, hafla hiyo imejumuisha Vyuo vya Dayamtambwe Pemba na Chuo cha Amali cha Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.  
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kuzinduliwa kwa Chuo cha Amali cha Daya Mtambwe na kile cha Kisongoni Makunduchi ni fursa ya pekee ya kuimarisha sekta ya ajira kwa vijana hapa nchini.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Chuo Cha Amali, Daya Mtambwe, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba kilichofunguliwa sambamba na Chuo cha Amali cha Kisongoni Makunduchi, Wilaya ya Kusini Mkoa  wa Kusini Uguja, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Alisema kuwa vyuo hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana na kuwataka vijana wasivunjike moyo na waendelee kusoma na faida yake watakuja kuiona wao wenyewe hapo baadae.

Rais Dk. Shein alisema kuwa matajiri na mabilionia wengi hapa nchini na hata nje ya nchi wengi wao utajiri wao unatokana na ujasiriamali.

Rais Dk. Shein alieleza kuridhika na mafunzo mapya ambayo yameongezwa katika masomo kwenye vyuo vya amali yakiwemo masomo ya uvuvi na kilimo ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufitia uchumi wa buluu.

Kutokana na ombi la uongozi wa Wizara hiyo ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutaka eneo kwa ajili ya mafunzo ya kilimo, Rais Dk. Shein ameahidi kuwapa eneo hilo huku akiwaelea kuwa kwa upande wa bahari wanaruhusika kuendelea na mafunzo yao ama pale watakapokwenda bahari kuu hapo ndipo utaratibu inabidi kufuatwa.

Aliongeza kuwa juhudi hizo za uwanzishwaji wa vyuo hivyo una madhumuni ya kuwapatia fursa vijana ambao hawakubahatika kuendelea na masomo wapate taaluma na mafunzo yatakayowapa ujuzi wa fani mbali mbali na hatimae wapate uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa wenyewe.

“Utaratibu huu unazingatia ule usemi maarufu usemao “Kufeli skuli, sio kufeli katika maisha”,alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa vituo vya mafunzo ya amali ni fursa nyengine muhimu ya kuwapa mafunzo ya ujuzi wa fani mbali mbali za ufundi vijana na wengi kati ya wanaomaliza katika vituo hivyo wanaendelea na maisha yao kwa mafanikio makubwa.

Alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Chuo hicho na kile cha Makunduchi katika Mkoa wa Kusini Unguja kumewezesha kuwa na Chuo cha mafunzo ya Amali kwa kila Mkoa katika Mikoa yote mitano ya Zanzibar.

Alisema kuwa Mkoa wa Kusini Pemba wanacho Chuo cha Amali kule Vitongoji, Kaskazini Unguja kipo Mkokotoni, Mjini Magharibi kipo Mwanakwerekwe na mwaka huu tumekamilisha ujenzi wa vyuo hivi katika Mkoa huo wa Kaskazini Pemba na kule Makunduchi katika Mkoa wa  Kusini Unguja.

Aliongeza kuwa kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, palikuwa na skuli moja tu iliyokuwa ikitoa mafunzo ya ufundi au amali iliyokuwa ikiitwa “Trade School” iliyopo Mikunguni Unguja ambapo katika skuli hii, vijana walipata mafunzo ya ufundi wa uashi, useremala na ufundi wa mifereji au ufundi bomba.

Alisema kuwa baada ya Mapinduzi mafunzo katika skuli ya ufundi ya Mikunguni yaliendelezwa na vile vile, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilijenga Chuo cha Ufundi cha Karume mnamo mwaka 1965 ambapo kazi nzuri ya kuwapa vijana waliojiunga na chuo hicho mafunzo ya ufundi wa fani mbali mbali zikiwemo umeme, ufundi wa magari, uhunzi, uashi na ufundi wa mifereji zilifanyika.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisema kwa kutambua umuhimu wa kuyaimarisha mafunzo ya amali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Mamlaka ya Mafunzo ya Amali, mwaka 2008 kwa sheria Namba 8 ya mwaka 2006 ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya Zanzibar ya 2020 pamoja na MKUZA Awamu ya kwanza na ya Pili, ili kuzidi kuimarisha na kusimamia utoaji wa mafunzo ya amali na kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa  mafunzo ya amali hayana mbadala katika sekta ya elimu na hivi leo Zanzibar inajivuni uimarishwaji wa sekta ya elimu tokeo skuli za awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina ubaguzi na kuitumia fursa hiyo kukemea ubaguzi huku akisisitiza kwamba hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho hakina ubaguzi.

“Chuo hichi majengo yake yanavutia sana kila kitu kimefanywa tena bila ya ubaguzi na anayefanya ubaguzi hiyari yake”.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali huku akisisitiza kwamba Chuo hicho kipelekwe walimu wenye sifa ili maendeleo zaidi yapatikane kama yalivyopatikana katika vyuo vyengine vya mafunzo ya elimu hapa nchini.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Risiki Pembe Juma alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa jitihada zake za kuhakikisha anaitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 ambapo aliahidi kukijenga chuo hicho na amekijenga.

Alisema kuwa kazi iliyofanywa ni kubwa sana na isiyo mfano hivyo alimpongeza Rais Dk. Shein kwa busara zake mapenzi na miongozo yake mizuri iliyopelekea kufanikishwa kwa mradi huo.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Idrissa Muslim Hijja alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza nafasi za ajira kwa vijana kwa kuongeza nafasi zaidi za mafunzo na kuwapatia vijana stadi na ujuzi katika fani mbali mbali za mafunzo ya amali, ufundi na biashara kwa mujibu wa soko la ajira.

Alisema kuwa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Daya ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambapo kazi ya ujenzi ilianza rasmi tarehe 22 Juni 2016 na sasa imekamilika na kukabidhiwa rasmi Serikali.

Aliongez akuwa Kampuni ya Ujenzi ya ZECCON ya hapa hapa Zanziar ndio iliyokamilisha ujenzi huo ikisimamiwa na Wakala wa Majengo Zanzibar na samani za Dakhalia zote zimtengenezwa na kufungwa na Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar ambapo ujenzi huo kwa ujumla wake umegharimu TZS Bilioni 11.2.

Alisema kuwa chuo hicho kitakuwa na huduma za dakhalia na hivyo kitapokea vijana kutoka pande zote za nchi ambapo kina uwezo wa kuandikisha wanafunzi 420 na wote kupata huduma za dakhalia wakati ambapo uwezo wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Makunduchi ni kuandikisha wanafunzi 512.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.