Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Ameweka Jiwe la Msingi Kiwanda Cha Nguo Chac Basra Chumbuni Jijini Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,.Dk. Ali Mohamed Shein akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Basra Textille Mill Ltd Ndg. Ahmed Osman, wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Kiwanda hicho cha Nguo cha Basra Zanzibar  

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar si mwanagenzi wa viwanda hivyo kuanzishwa kwa  kiwanda kipya cha nguo cha Basra Textile Mills Ltd kutairejesha Zanzibar katika medani ya viwanda.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la  Kiwanda kipya cha nguo cha Basra Textile Mills Ltd, kilichopo Chumbuni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni hafla ya mwisho ya uwekaji wa mawe ya msingi wa miradi katika uongozi wake akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Rais Dk. Shein alitoa shukurani maalum kwa mwekezaji na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Basra Textile Mills Ltd Ahmed Osman kwa uwamuzi wake wa kuja kujenga kiwanda cha ushoni na kutengeneza nguo hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa hatua yake hiyo ni katika kuziunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha sekta ya viwanda kama ilivyoelezwa katika ibara ya 84 ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Alisema kuwa Kampuni hiyo ina uwezo mkubwa na kiwanda hicho kitakuwa ni cha mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki na matarajio kiwanda hicho ni kuzinduliwa mnamo Januari mwakani katika sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Januari 1964.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, juhudi za kuimarisha sekta ya viwanda zilizochukuliwa, zimezaa matunda ambayo baadhi yake ni kuanzishwa kwa kiwanda hicho cha nguo cha Basra.

Alisema kuwa kiwanda hicho ni matokeo ya juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya viwanda ambapo mradi huo ni mkubwa wa kimkakati ambao utatoa fursa za ajira kwa wananchi wengi hatua kwa hatua.

Alisema kuwa ajira 1,600 zitakazotolewa katika kiwanda hicho ni miongoni mwa ajira 300,000 anazozielezea mgombea wa Urais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi katika mikutano ya kampeni za CCM unguja na Pemba.

Alisisitiza haja ya kupewa ushirikiano wawekezaji hao na kuwa na subira kama wanavyosema wazee subira huvuta kheri na sio muda mrefu matunda ya uwekezaji huo yataonekana.

Rais Dk. Shein alieleza kwamba mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 8.2 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 18 mwaka 2018.

Alisisitiza haja ya kwa wananchi kuvipenda vitu vinavyotengenezwa hapa hapa nyumbani kwa kuwa watu wa mwanzo ambao watanunua bidhaa za nguo na vitambaa kutoka katika kiwanda hicho ni wananchi wa Zanzibar.

“Nguo zitatengezwa Zanzibar na kupelekwa nje ya nchi ambapo lebo maalum zitawekwa za kuitaja Zanzibar hatua ambayo itaitangaza Zanzibar vizuri kitaifa na kimataifa”, alisema Rais Dk. Shein.

Pia, Rais Dk. Shein aAliwataka wananchi wanaoishi eneo hilo la Chumbuni ambao wako karibu na kiwanda hicho kukilinda na kukitunza sambamba na kuhakikisha suala la wizi wa malighafi na bidhaa za kiwanda hicho hautokei.

Akielezea kuhusu malighafi zitakazotumika katika kiwanda hicho ikiwemo gesi, Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kwa muda huu uendelee kununua gesi kutoka Tanzania Bara huku akiwapa matumaini kwamba si muda mrefu gesi wataipata hapa hapa Zanzibar mara tu itakapoanza kuchimbwa.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaishi kwa matumaini kwamba ipo siku Zanzibar itapata rasilimali zilizopo katika ardhi yake na bahari yake ikiwemo gesi ambayo utafiti umeonesha kwamba kiwango kiliopo ni kikubwa sana.

Rais Dk. Shein pia alitoa agizo kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) la kuhakikisha kwamba mapema mwezi ujao kazi ya kuziondosha waya za laini kubwa ya umeme zilizopita kwenye maeneo ya kiwanda hicho ziwe imekamilika.

Aidha, kuhusu changamoto ya uchimbaji wa msingi wa kupitishia maji machafu yanayotoka kiwandani hapo alisisitiza kufanyika kwa utaratibu wa haraka ili kazi hiyo ifanyike kwa mashirikiano ya uongozi wa Kamati ya Mawaziri ya Baraza la Mapinduzi.

Rais Dk. Shein alitoa shukurani zake za dhati kwa kazi nzuri iliyosimamiwa vyema na Kamati iliyoundwa na Baraza la Mapinduzi ya Mawaziri iliyoongozwa na Balozi Amina Salum Ali Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, Waziri wa Fedha na Mipango, Salama Aboud Talib, Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati pamoja na Said Hassan Said Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kuwanasihi vijana watakaobahatika kuajiriwa katika kiwanda hicho kuitumia fursa hio kwa kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na nidhamu na wasiwe wavivu.

Vile vile alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wawekezaji wa kiwanda hicho kuzingatia maslahi ya wafanyakazi wao watakaowaajiri kwa kuwapa mshahara mzuri ili kila mmoja aridhike na aweze kutimiza wajibu na majukumu yake kikamilifu.

Hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambae pia, ni mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri, pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Nae Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali alieleza jitihada zilizochukuliwa na Serikali kupitia Wizara yake katika kuhakikisha kiwanda hicho kinajengwa katika eneo hilo huku akieleza mafanikio ya kiwanda hicho kwa uchumi wa Zanzibar pamoja na watu wake.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Juma Hassan Reli alisema kwamba kiwanda hicho ni suluhisho la kuagiza vitambaa kutoka nje kwani badala ya kuagiza sasa vitatengenezwa hapa hapa Zanzibar.

Alisema kuwa kiwanda hicho kikianza kazi kitaingiza fedha nyingi za kigeni katika uchumi wa Zanzibar na hivyo kufanya sarafu ya uchumi wa viwanda kuweza kuimarisha thamani ya sarafu ya Tanzania.

Alisema kuwa kufuatana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020 na Dira ya Maendeleo ya 2050, Serikali imepanga kuifanya Zanzibar iwe nchi ya viwanda pamoja na utalii.

Hivyo, alisema kuwa uanzishwaji wa Kiwanda hicho kutaongeza thamani ya zao la pamba kwa kupitia hatua mbali mbali za uzalishaji  wa zao hilo hapa nchini sambamba na kuondoa tatizo la kuondosha fedha za kigeni kwenda nje kupitia ununuzi wa bidhaa za nguo.

Alisisitiza kuwa kiwanda hicho hivi sasa kimeshanaza kupokea maombi ya bidhaa mbali mbali kutoka nchi za nje kama Kenya, Uganda na Tanzania Bara huku akieleza kuwa mahitaji makubwa kwa nchi za Msumbiji, Kenya, Rwanda na Comoro.

Mapema akisoma risala ya muekezaji Saleh Suleiman Hamad alisema kwamba Mradi wa Basra Textile Mills Ltd ni mradi uliosajiliwa Zanzibar na kuanzishwa kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (ZIPA) katika mwaka 2019.

Alisema kuwa Mradi huo umepangwa kutekelezwa kwa awamu tatu na kuzalisha bidhaa za aina mbali mbali za vitambaa na mavazi ambapo hadi kukamilika kwa awamu zake tatu unatarajiwa kugharimu kiasi cha TZS Bilioni 115.50 na kuajiri wafanyakazi wapatao 1,600.

Alisema kuwa mradi huo ukikamilika utaweza kuzalisha kiasi cha mita 250,000 za vitambaa kwa siku, ambayo ni sawa na mita milioni 7.5 kwa mwezi.

Sambamba na hayo, alizitaja bidhaa zinazotarajiwa kuzalishwa kuwa ni pamoja na vitenge, kanga, mashuka ya vitanda, mapazia, vitambaa vya mashati, vikoi, madira ya akina mama, sare za aina mbali mbali, vitambaa vya suti na kadhalika.

Alisisitiza kwamba masoko ya bidhaa za mradi huo ni nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Kusini mwa Afrika na hatimae Ulaya na Marekani.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.