Habari za Punde

SUZA Kuendelea Kushirikiana Kuongeza Bidii na Ubunifu Katika Programu ya Ufundishaji wa Kiswahili Kufikia Dhamira Kufikia Oxford ya Kiswahili.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia katika hafla ya kumuaga iliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu SUZA Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusiniu Unguja leo 6/10/2020.
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amelitaka Baraza la Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kuendelea kushirikiana na kuongeza bidii na ubunifu katika kuiendeleza Programu ya ufundishaji wa Kiswahili ili kufikia dhamira ya kuifanya SUZA kuwa ‘Oxford ya Kiswahili’.

Dk. Shein ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar  (SUZA) ametoa rai hiyo katika hafla ya kuagwa, baada ya kukiongoza chuo hicho kwa miaka kumi, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema ni vigumu kuzungumzia historia na maendeleo ya Kiswahili bila kuzungumzia historia na maendeleo ya Kiutamaduni wa Zanzibar, huku akibainisha kuwa  Zanzibar ni nchi ya Kiswahili kinachozungumzwa kwa ufasaha katika maeneo ya mjini.

Alisema watu wengi huridhika kupata tafsiri ya maneno kutoka makamusi ya Kiingereza kutoka ‘Oxford’ kuliko makamusi mengine duniani, jambo ambalo linaweza kufikiwa nchini kwa kuweKa nguvu katika kuikuza na kuiendeleza lugha hiyo.

Aidha, alihimiza umuhimu wa kuimarisha skuli ya Kiswahili na lugha za kigeni ili kuifanya Zanzibar kuwa ‘Centre of Exellence’.

Alieleza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imefungua kituo cha Kiswahili katika eneo la Gymkhana hapa Zanzibar, hivyo ni vyema SUZA ikachangamkia jambo hilo na kuwa kituo cha Kiswahili.

Dk. Shein alisema ni jambo la kufurahisha hivi sasa Zanzibar kuwa na Vyuo vikuu vitatu ambavyo kwa wastani hutoa wahitimu 3,000 kila mwaka na kubainisha umuhimu wa Wazanzibari kusoma elimu ya juu hapa nchini, kwani itamuwezesha mhitimu kufahamu changamoto ziliopo na jinsi ya kuisaidia jamii.

Akigusia mafanikio ya SUZA katika kipindi cha miaka kumi (10) ya uongozi wake, Dk. Shein alisema katika kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa wataalamu, imeanzisha fani mbali mbali ili kwenda sambamba na mahitaji.

Alisema katika kipindi hicho kuna mafanikio makubwa ya kielimu yaliofikiwa kupitia SUZA , ikiwemo uanzishaji wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba pamoja na mafunzo ya Udaktari (doctor of Medicine), mafunzo yalioanza mwaka 2017/2018 na wanafunzi 25 kufaulu pamoja na wengine 48 waliofanikiwa kumaliza masomo yao mwaka 2018/2019.

Alisema SUZA imefanikiwa kuanzisha mafunzo ya shahada ya kwanza ya Udaktari wa meno mwaka 2019/2020 ambapo jumla ya wanafunzi sita wanaendelea vizuri na masomo hayo.

Rais Dk. Shein alisema jitihada za kusomesha madaktari ndani na nje ya nchi zimewezesha kuongeza idadi ya madaktari na watumishi wengine wa afya nchini, akibainishwa kuwepo uwiano wa madaktari na watu wanaowahudumia.

Alisema hivi sasa Daktari mmoja anawahudumia watu 6,276 kutoka wastani wa daktari mmoja aliekuwa akiwahudumia watu 31,838 mnamo mwaka  2010.

Alisema lengo hilo linaendana na Manifesto ya Chama cha Afro Shirazi pamoja na kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kwa nchi zinazoendelea cha daktari mmoja kuwahudumia watu 10,000.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka kumi ya Uongozi wake, chuo hicho kimefanikiwa kupata Ithibati kamili (full Accreditation) ya Tume  ya Vyuo vikuu Tanzania (TCU) .

Aidha, alisema Serikali ilifanya uamuzi wa kuziunganisha na SUZA taasisi mbali mbali, ikiwemo Chuo cha Utawala wa Fedha Chwaka, Chuo cha Kilimo Kizimbani, Chuo cha Habari Kilimani, Chuo ca Afya Mbweni pamoja na Chuo cha Utalii Maruhubi, kwa lengo la kuinua hadhi na kiwango cha elimu inayotolewa na taasisi za elimu ya juu.

Hata hivyo alisema wakati vyuo hivyo vinaunganishwa na SUZA wako watu walioonyesha kutokuelewa, hivyo akatumia fursa hiyo kuipongeza Kamati maalum iliyoundwa kushauri na kutoa mapendekezo ya kuunganisha vyuo hivyo.

Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alitoa shukurani kwa Mkuu wa Chuo hicho kwa juhudi kubwa za kusimamia mendeleo ya chuo hicho pamoja na hatua za kuhamasisha elimu ya juu kwa  akinamama, hivyo kuongeza ufaulu kwa jinsia hiyo kwa kiwango cha juu.

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Said Bakari Jecha alisema katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Dk. Shein, SUZA imepata mafanikio makubwa na ya haraka na kufanikiwa kupata umarufu mkubwa wakati ambapo vyuo vingi Duniani hupata mafanikio kama hayo baada ya  miaka mingi kupita.

Akisoma maelezo hayo kwa niaba yake, mwanatalaamu Mwita Mgeni alisema Chuo hicho kimetekeleza kikamilifu Ilani ya CCM , ambapo pamoja na mambo mengine kwa zaidi ya asilimia themanini ya wanafunzi wanasoma kupitia  mikopo inayotolewa serikalini.

Aidha, Makamo Mwenyekiti wa Chuo hicho Dk. Zakia Mohamed Abubakar alisema katika kipindi cha Uongozi wake, Dk. Shein alifanya juhudi kubwa kukiendeleza chuo hicho kiasi cha kupata mafanikio ya kupigiwa mfano, ikiwemo kukuza ubora wa elimu kufuatia hatua za uimarishaji wa miundo mbinu ya elimu, nguvu kazi pamoja na upatikanaji wa maslahi bora.

Alisema kutokana na msukumo mkubwa wa Dk. Shein, chuo hicho kimeweza kuanzisha ‘SUZA TV’ iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa taaluma kwa wanafunzi wa Sekondari, hususan wanaosoma masomo ya Sayansi na Hisabati.

Katika hatua nyengine, Mwanataaluma Ameir Mohamed Makame, akisoma risala ya wanataaluma, alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa mchango mkubwa wa kukiendeleza chuo hicho ndani ya kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake kwa kuangalia maslahi yao pamoja na kuwepo uwazi katika suala la upandishaji vyeo.

Alisema katika kipindi hicho wanataaluma walipata fursa za masomo ndani na nje ya nchi pamoja na kupata  nyadhifa za kufanyakazi katika maeneo mbali mbali.

Alisema Jumuiya ya wanataaluma inampongeza kwa dhati Dk. Shein kwa hatua ya kuwaamini na kuwateua wanataaluma wanawake kushika nyadhifa za kuiongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja chuo hicho.

Hata hivyo, mwantaaluma huyo alisema bado kada hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo ya kuwepo idadi ndogo ya wanataaluma katika kiwango cha shahada ya Uzamivu.

Aidha, aleleza kuwa wanataaluma wa SUZA wanakabiliwa na kuwepo kwa tofauti kubwa ya maslahi (mishahara) kati yao na wenzao wanaovitumikia vyuo vikuu mbali mbali Tanzania Bara.

Ameir alieleza matumaini makubwa waliyonayo wanataaluma wa SUZA ya kuwa Mkuu wa Chuo hicho ajae atayapatia ufumbuzi masuala hayo ili kuwatia moyo wanataaluma.

Katika hafla hiyo, viongozi mbali mbali wa Serikali walihudhuria,akiwemo Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilali, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, Mawaziri pamoja na wake wa Viongozi wakuu.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.