Habari za Punde

Makamo wa Pili wa Rais, Mhe Hemed atembelea Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Nd. Sheha Mjaja kulia akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla alipofanya ziara Maalum Afisi za Mamlaka hiyo Maruhubi.
Mhe. Hemed Suleiman akipatiwa maelezo kwenye Kitengo cha Mawasiliano ndani ya Majengo ya Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa yaliyopo Maruhubi alipofanya ziara maalum ya kutembelea Taasisi na Idara zilizo chini ya Afisi yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabilana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib Makame akimkaguza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed sehemu mbali mbali ya Ghala Kuu la Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar hapo Maruhubi.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla amesema wakati umefika kwa Taasisi za Umma na hata zile binafsi kuandaa mpango maalum wa kuwasomesha Watendaji wao fani ya kukabiliana na maafa ili pale Taifa linapopata majanga likawa na nguvu kubwa za Kitaalamu katika kukabiliana  nayo.

Alisema Serikali Kuu Kupitia Kamisheni yake ya Kukabiliana na Maafa licha ya jitihada kubwa inazoendelea kuchukuwa za kuona pale yanayotokea Maafa inakabiliana nayo lakini bado ipo haja ya kuona ushiriki wa wadau wote zikiwemo Pia Taasisi za Ulinzi pamoja na Wananchi unapatikana.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla alitoa kauli hiyo wakati akiwa kwenye ziara Maalum ya kuzitembelea Idara na Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  ili kujitambulisha rasmi mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo lengo likiwa kuelewa mafanikio na changamoto zilizomo kwenye Taasisi hizo.

Alisema Taifa lazima lijipange  kwa kuwa na Wataalamu wake wa kutosha katika masuala ya kukabiliana na Maafa kwa vile Elimu ya Masuala hayo kwa sasa inapatikana hapa Nchini hadi ngazi ya Shahada ya kwanza na matokeo ya faida yake yanaweza kuonekana ndani ya kipindi kifupi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka Watendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa waendelee na Uzalendo wao kwa kutekeleza majukumu waliyopewa na Taifa kwa vile yanawagusa moja kwa Moja Wananchi katika Maeneo mbali mbali Nchini.

Mheshimiwa Hemed alielezea faraja yake kutokana na hatua kubwa iliyofikiwa kwa Watendaji wa Tume hiyo kuendelea kutoa Elimu kwa Umma Mijini na Vijijini na wakati mwengine hata kuvitumia Vyombo vya Habari katika kuifikisha Taaluma hiyo ya Wananchi katika kukabiliana na Maafa.

Hata hivyo aliwakumbusha Watendaji hao waendelee kuiheshimu  misaada na vifaa vinavyotolewa na Wafadhili pamoja na Washirika wa Maendeleo ambavyo hulengwa kuwapatiwa Wananchi wanaokumbwa na Majanga katika maeneo mbali mbali Nchini.

Akizungumzia maslahi ya Wafanyakazi hasa wale wa ngazi ya Chini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hapendelei kuona Watendaji hao wananyimwa haki zao kwa visingizio visivyokuwa na msingi.

Alisema Wapo baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Umma wanaoamua kujipatia Posho kwa kisingizio cha safari zisizo na tija kwa Taasisi yao lakini wanashindwa kuwakamilishia Posho Watendaji wao wadogo linalochukuwa Zaidi ya miezi sita jambo linaloleta chuki na uhasama unaochangia kuzorotesha uwajibikaji wa kila siku.

Aliagiza kwamba inapotokea uwepo wa madai ya Haki za Wafanyakazi wa daraja ya chini ni vyema kwa Wakuu wa Taasisi husika wakajinyima wao kwanza na badala yake kuwakamilisha Wafanyakazi wao ili kurejesha hali ya mashirikiano na upendo miongoni mwao.

Akitoa Taarifa  Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabilana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib Makame alisema Kamisheni imefanikiwa kuongeza Vituo vya Mawasiliano katika maeneo tofauti hadi Wilayani ili kuratibu Taarifa zote zinazohusiana na masuala ya Maafa.

Nd. Makame alisema hatua hiyo inakwenda sambamba na Maafisa wa Kamisheni hiyo kuanza zoezi la utoaji wa mafunzo juu ya namna ya kujiandaa kujikinga na mvua zinazokuja kwa vile maafa ni suala jipya linalokuja na mambo tofauti yanayokwaza harakati za Kijamii.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla alizitembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira pamoja na Idaya ya Mazingira hapo Maruhubi akisisitiza pamoja na jitihada kubwa inayoendelea kuchukuliwa lakini bado Elimu ya utunzaji wa Mazingira haijakidhi lengo.

Alisema hali ya mazingira  inaweza kuwa mbaya Zaidi kama hakutachukuliwa jitihada za ziada za kudhibiti uchafuzi wa mazingirea kutokana na jinsi yanavyoharibiwa na baadhi ya Watu kwa kisingizio cha kutafuta Riziki ambayo inakuwa sio ya halali.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwataka Maafisa wa Mazingira wa Wilaya na Mikoa kuongeza jitihada zitakazosaidia nguvu kubwa ya kudhibiti  kuenea kwa uchafuzi wa Kimazingira katika maeneo yanayowazunguuka.

Aliwaomba Maafisa hao kwa kushirikiana na Wataalamu wa Mazingira kujitahidi kufanya upembuzi wa Kimazingira katika Miradi Mipya inayoanzishwa hasa kwa  ile ya Sekta Binafsi na Uwekezaji ili kujiepusha mapema na hitilafu za kimazingira kwenye Miradi hiyo.

Alieleza kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa Miradi ya Taasisi za Serikali  na hii imepatikana kutokana na ushauri uliotolewa na Wataaamu wa Fani hiyo ya Mazingira.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.