Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais, Mh. Hemed azungumza na Wakuu wa Taasisi za Umma Kisiwani Pemba




 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wakuu wa Taasisi za Umma Kisiwani Pemba hapo Ukumbi wa Mikutano wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Wakuu wa Taasisi za Umma wanapaswa kutekeleza dhima ya kuwasimamia Watendaji wao ikiwemo  Miradi ya Maendeleo na kuacha kuwajibika kimazoea ili kwenda sambamba na Kasi kubwa  ya Serikali iliyoamua kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo akiwasilisha salamu za shukrani za Rais wa Zanzibar za kuwapongeza Viongozi na Wananchi Kisiwani Pemba kwa kukamilisha Uchaguzi Mkuu katika misingi ya Amani wakati akizungumza na Wakuu wa Taasisi za Serikali Kisiwani Pemba hapo Ukumbi wa Makonyo Wawi.

Alisema nidhamu ya kazi lazima irejee maofisini kwa kuzingatia utaratibu  unaompa fursa kila Mtumishi kuangalia mapungufu yaliyomzunguuka katika eneo lake la kazi na kuchukuwa hatua  za maamuzi katika kutafuta suluhisho haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alieleza kwamba watendaji lazima wabadilike vyenginevyo utaratibu wa Serikali utawabadilisha ingawa dharura za kibinaadamu zinakubalika lakini pia haitakuwa kisingizio cha Mtumishi kuwepuka Wajibu wake aliyopangiwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa kudumisha Umoja, Ushirikiano na Mshikamano ambao ndio nguzo ya kufanikisha zile changamoto zinazojichomoza ndani ya Jamii na hata Taasisi za Umma.

Alifahamisha kwamba upo uwezekano Mkubwa wa changamoto zinazowakabili Watendaji wa Taasisi za Umma na Wananchi akatolea mfano changamoto hizo kuwa ni pamoja na huduma za Maji, Afya na hata Miundombinu midogo inayoweza kutatuliwa kwa nguvu za Viongozi katika ngazi za Wilaya na Mikoa.

Mheshimiwa Hemed alibainisha kwamba zile changamoto kubwa za Wananchi zinapaswa kuwasilishwa katika ngazi za juu za Serikali kwa hatua ya kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba  Mh. Omar  Khamis Othman kwa Niaba ya Wakuu wa Taasisi zote Kisiwani humo wamempongea Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi kwa ushindi mkubwa walioupata kwenye Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Alisema ushindi huo umedhihirish wazi jinsi Wananchi walio wengi Nchini Bara na Zanzibar kuendelea kuwa na imani na matumaini na Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongoza Dola Nchini Tanzania.

Mh. Omar kwa niaba ya Wakuu wa Taasisi hizo pamoja na Watendaji wote wa Umma wamemhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wako tayari wakati wowote kupokea maagizo, Mawazo na maelekezo ya Viongozi wao katika kuchapa kazi kuanzia sasa.

Alieleza kwamba kazi kubwa na yenye nguvu kwa sasa imekwisha na lililobakia kwa Watumishi wa Umma na Wananchi kuelekeza nguvu zao katika kujiletea Maendeleo huku wakitarajia mafanikio makubwa ya Serikali kama walivyoahidi Viongozi Wakuu wakati wa Kampeni ya Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.