Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akitoa agizo kwa Uongozi wa Taasisi inayosimamia masuala ya Uvuvi kujipanga vyema katika uendeshhaji wa Kituo cha Utotoaji wa Vifaranga vya Samaki.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza Uongozi wa Sekta inayosimamia masuala ya Uvuvi Zanzibar kujipanga vyema katika kuhakikisha Kituo cha utotoaji wa Vifaranga vya Samaki kinafanya kazi zake kama matarajio ya Serikali katika kuwajengea uwezo wa Ajira Wavuvi hapa Nchini.
Alionya kwamba juhudi za makusudi zinalazimika kuchukuliwa ili kuona mradi huo uliokuwa tegemeo kubwa kwa Wananchi wanaojishughulisha na Masuala ya Uvuvi unatoa huduma zilizokusudiwa.
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla alitoa agizo hilo baada ya kutoridhika na utendaji kazi Mradi wa Kituo hicho kiliopo eneo Beit El Ras Kaskazini ya Mji wa Zanzibar alipofanya ziara ya kushtukizia kwenye Kituo hicho.
Alisema Wananchi tayari walikuwa wameshajenga matumaini ya uwepo wa Kituo hicho muhimu kilichojengwa kwa gharama kubwa ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa Vifaranga vya Samaki hasa kipindi hichi ambacho Serikai imeshajipanga kuingia katika Uchumi wa Buluu.
“ Siridhishwi kabisa na hali halisi ninayoishuhudia kwenye Kituo hichi na kama ni kutoa alama kwa muonekano wake ulivyo ni sawa na Sufuri”. Alionyesha masikitiko yake Mhe Hemed.
Aliutaka Uongozi wa Sekta hiyo inayosimamia Uvuvi kwa kutumia Wataalamu wake kutoa mapendekezo yao kwa Serikali Kuu juu ya uendeshaji wa Kituo hicho ili yafanyiwe kazi ili mradi unaotokana na Kituo hicho ukisimamiwa vizuri unaweza kusaidia Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibainisha kwamba wakati wa ubabaishaji umekwisha kwa vile Wananchi waliamua kutoa ridhaa kwa Chama Tawala kuendelea kuongoza Dola jambo ambalo Serikali iliyopewa jukumu hilo kamwe haitaruhusu kushirikiana na mzembe, mbadhirifu au mbabaishaji.
Mapema Mkuu wa Kituo cha utotoaji wa Vifaranga vya Samaki Nd. Said Juma Shaaban alisema Kituo hicho kilianza matayarisho Mnamo Mwaka 2015 kwa kuungwa Mkono ya Shirika la Misaada ya Maendeleo la Korea { Koika} pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Kimataifa {FAO}.
Nd. Said alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mradi huo ulipangiwa kuzalisha Vifaranga vya Samaki, Kaa pamoja na Majongoo ili baadae visambazwe kwa Wafugaji wa mazao ya Baharini.
Naye kwa Upande wake Mkurugenzi wa Idara inayosimamia masuala ya Uvuvi Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe alisema kuzorota kwa Kituo hicho kunatokana na ukosefu wa Bajeti kamili ya kukiendesha.
Mradi huo ulipoanzishwa ulipangiwa kutoa ajira ya Wafugaji wa Samaki ipatayo 36,312, Wachuuzi pamoja na Wakulima wa Mwani wapatao Milioni 2,123,624 katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.
Aidha Mradi huo uliozinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba Balozi Seif Ali Iddi mnamo Tarehe 20 April Mwaka 2018 uligharamiwa na Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo { FAO} kwa Dola za Kimarekani Milioni 3.2.
No comments:
Post a Comment