Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi "Kuekeza Katika Michezo Itakwenda Sambamba na Kukaa na Wadau wa Soka Zanzibar"

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Baraza la Kumi la Wawakilishi Zanzibar, katika ukumbi wa mkutano wa baraza Chukwani Jijini  Zanzibar na kushoto Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Maryam Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali  Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itawekeza kwenye michezo katika kuibua, kuelea na kuendeleza vipaji vya vijana.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la Kumi la Wawakilishi hafla iliyofanyika huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa katika hatua hiyo ya kuekeza kwenye michezo itakwenda sambamba na kukaa na wadau wa soka kutafuta jawabu la kuamsha msisimko wa ligi ya Zanzibar.

“Wakati nakua timu za Zanzibar za Small Simba, Malindi, Mlandege na KMKM zilikuwa ni timu zenye sifa na kuchachafya timu za Bara na zile za Afrika Mashariki” alisema Dk. Hussein Mwinyi.

Rais Dk. Hussein aliongeza kuwa azma ya Serikali ni kuona Timu ya Taifa ya Zanzibar inakwenda mbali katika kushiriki michuano ya Afrika ili kutumia vizuri fursa ya uanachama katika Shirikisho la Michezo la Afrika (CAF) ambayo imeipigania kwa miaka mingi.   

Aidha, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza kwamba eneo jengine ambalo litafanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Nane ni kushughulikia Sanaa, burudani pamoja na michezo kwani mambo hayo matatu yana nafasi ya kipekee katika kuwaunganisha Wazanzibari, kuwatambulisha Wazanzibari duniani na kukuza uchumi na ajira.

Aliongeza kuwa Muziki wa Taarab, muziki wa kizazi kipya na Sanaa ya filamu kupitia matamasha   ya ZIFF na ‘Sauti ya Busara’ yameitangaza sana Zanzibar na kuwa na mchango wa kipekee  hivyo, aliahidi kuyalea na kuyakuza matamasha hayo na mengine ili kutangaza hazina ya utamaduni na ustaarabu wa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii, kipato pamoja na ajira.

Kutokana na ligi ya Zanzibar kuwa na changamoto ya ufadhili, Rais Dk. Hussein Mwinyi amewahakikishia wanamichezo kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha ligi ya Zanzibar inapta ufadhili wa uhakika.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.