Habari za Punde

Kamati ya hamasa ya Mapinduzi Cup yaundwa


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Omar Hassan (King) 

Na Mwandishi wetu


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Omar Hassan (King) ametangaza majina nane ya wajumbe wa Kamati ya Uhamasishaji wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021.
 
Kamati hiyo itakayojumuisha wajumbe kutoka Zanzibar na Tanzania bara itaongozwa na Mwenyekiti Taufiq Salim Turkey ambae ni Mbunge wa Jimbo la Mpendae na wajumbe wengine saba ambao ni Hassan Mussa Ibrahim (Has T), Salum Issa Ameir, Mwanahawa Rajab Iddi, Khamis Mwinjuma (Mwana FA) Jerry Muro,  Salama Jabir na Ali Saleh (Alberto).
 
Akitangaza majina hayo kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Tabia Maulid Mwita amesema lengo la kamati hiyo ni kunogesha  na kuwahamasisha wananchi kupitia wasanii wa sanaa za asili, maigizo na kizazi  kipya ili kuwezesha kufana kwa sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katibu King pia ameitumia fursa hiyo kuwashajihisha wananchi kushiriki kwa wingi katika michuano hiyo yenye mnasaba wa kuyaenzi  mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
 
Wasanii mbali mbali watatumbuiza  kabla ya mechi, wakati wa mapumziko na baada ya mchezo katika Mashindano ya msimu huu ambayo yanatarajiwa kuanza January 1 au 3, 2021 kwa kuzishirikisha timu 9 zikiwemo Malindi, Mlandege, Chipukizi na Jamhuri kwa upande wa Zanzibar na Tanzania bara ni Mabingwa watetezi Mtibwa, Simba, Yanga, Azam na Namungo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.