Habari za Punde

Maazimio ya Kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo kilichokutana tarehe 05/12/2020 Dar es Salaam

 MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA ACT WAZALENDO KILICHOKUTANA TAREHE 05 DISEMBA 2020: ONOMO HOTEL DAR ES SALAAM


Jana tarehe 05 Disemba, 2020 Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilikutana katika kikao chake maalum, ikiwa na lengo la kujadili na kufikia maamuzi juu ya masuala kadhaa yanayohusu mustakabali wa Taifa na Chama chetu.


Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea taarifa ya maoni ya wanachama juu ya hali ya siasa nchini hususani Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2020 Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.


Katika mjadala wa kina, uliojikita katika maoni yaliyotolewa na wanachama, Kamati Kuu imezingatia kwamba;-


Historia ya kisiasa ya Zanzibar kwa kila uchaguzi tangu uhuru na hata baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi imekuwa ikigubikwa na hali iliyojaa majeraha, uhasama mkubwa wa kisiasa, watu kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa, kudhalilishwa kijinsia na mali za watu kuharibiwa. Hali hii imejirudia tena katika uchaguzi wa mwaka 2020, ambapo watu 17 wamefariki kutokana na madhila ya uchaguzi huu ikiwemo kupigwa risasi, vipigo na mashambulizi ya kimwili, na 302 wamejeruhiwa na wengine kudhalilishwa kijinsia na mali zao zikiharibiwa na kuibiwa. 


Wakati pekee ambao Zanzibar imefanya uchaguzi wa kistarabu na wananchi  kusalimika na maafa pamoja na madhila yanayotokana na uchaguzi katika historia ya chaguzi Zanzibar ni kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo Zanzibar ilikuwa imeingia katika  Maridhiano ya Novemba 5, 2009 kabla ya uchaguzi huo. Pia katika Uchaguzi wa mwaka 2015 ambao ulikuwa ni uchaguzi bora kuliko chaguzi zote kabla ya kufutwa kwake. Uchaguzi huu nao ulifanyika wakati ambapo Zanzibar ilikuwa ipo chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ni zao la Maridhiano. 


Kamati Kuu imejiridhisha  kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa kwa moyo Safi itakuwa ni kwa maslahi ya Zanzibar, Wazanzibari na Taifa kwa ujumla katika kuhakikisha kuwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu na uvurugaji wa Uchaguzi vinadhibitiwa kama ilivyokuwa wakati wa Uchaguzi wa mwaka 2010. Dhima ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa maslahi ya Wananchi inapaswa pamoja na mambo mengine kuhakikisha kuwa; 


i. Uchunguzi wa matukio yote yaliyotokea kabla, wakati na baada ya Uchaguzi ya uvunjaji wa haki za binaadamu, unafanyika na kuwafariji waathirika wote pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kupanga na kutekeleza matukio hayo.

ii. Kunafanyika Mabadiliko ya mfumo wa Uchaguzi Zanzibar ili kurejesha imani ya wananchi juu ya uwepo wa uchaguzi huru na wa haki. 

iii. Kunafanyika Marekebisho ya uendeshaji wa vyombo vya Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili vifanye kazi kwa Weledi (professionalism) na bila ubaguzi wa kisiasa.


Kamati Kuu imezingatia hali ilivyo Zanzibar hivi sasa ambapo siasa za chuki na uhasama zimerudi upya kutokana na makovu yanayotokana na uchaguzi wa Mwaka 2020. Kwamba Zanzibar inahitaji busara kubwa katika kuponya majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo. Pia, Zanzibar inahitaji hekima na busara katika kuhakikisha kuwa matukio ya namna hii hayajirudii tena na kwamba lazima kuwe na utaratibu wa kuhakikisha kuwa chaguzi zijazo zinakuwa huru, za haki, zinazokubalika na zenye hali ya utulivu. 


Hivyo basi, Kamati Kuu kwa kauli moja imefikia maazimio yafuatayo:-


1. Kamati Kuu IMEAZIMIA Chama kiwaruhusu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge, na Madiwani waliochaguliwa kwenda kukiwakilisha Chama na Wananchi waliowachagua.


2. Kwa kuzingatia Ibara ya 9(3) ya Katiba ya Zanzibar, Kamati Kuu imeridhia Chama kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na imeielekeza Kamati ya Uongozi kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.


Kamati Kuu imefikia maamuzi haya kwa kuzingatia maoni ya wanachama na viongozi wa Chama chetu, tathmini ya historia ya mapambano ya demokrasia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. 
Ado Shaibu,

Katibu Mkuu,

ACT Wazalendo,

06 Disemba, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.