Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais, Mhe Hemed awatengua Mkaguzi na Mhandisi wa Manispaa ya Mjini kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akifanya ziara Maalum ya kulikagua eneo la Bishara la Darajani hadi Muembe Ladu na kutoa siku tatu Siku Tatu kuondoshwa kwa uchafu wote uliomo kwenye eneo hilo.
Mhandisi wa Baraza la Manispaa ya Mjini Mzee Khamis akitoa maelezo ya baadhi ya changamoto za maji machafu yanayosumbua ndani ya eneo la Biashara la Darajani hadi Muembe Ladu.
Mhe. Hemed Suleiman akiwaagiza Wafanyabiashara kuzingatia mazingira bora mbele ya Maduka yao hasa uwekwaji wa vyombo vya moto vinavyosumbua wapiti njia kwenye Bara bara hiyo.
Mmoja wa Wafanyabiashara wa Maduka ya Mlandege alielezea hali halisi ya Biashara inayoridhisha kipindi hichi na kuishauri Serikali kuangalia upya Kodi wanazotozwa zilingane na muenendo wa Biashara Kimataifa.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Kati kati akimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Mjini Nd. Said Kulia yake kuwapangia kazi nyengine Mkaguzi na Mhandisi wa Manispaa hiyo baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kusimamia kazi za kila Siku.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amemuamuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Mjini kuwatengua na baadae kuwapangia kazi nyengine Mkaguzi na Mhandisi wa Manispaa hiyo baada ya kushindwa kusimamia majukumu yao ya Kazi ya kila siku.

Hatua hiyo imekuja kufuatia hali halisi ya mazingira yaliyopo katika eneo Kuu ya Kitovu cha Biashara Zanzibar ambalo limezunguukwa na miundombinu mibovu ya bara bara na baadhi ya sehemu hasa ukanda na Maduka makubwa kutuwama kwa maji machafu kwa kipindi kirefu.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ambae ameonyesha kukerwa kwake na hali hiyo alitoa agizo hilo alipofanya ziara Maalum ya kuangalia mazingira halisi ya eneo maalum la Biashara lililoanzia Darajani, kupitia Mchangani, Mlande, Biziredi na kumalizia Kituo cha Magari ya Abiria Muembe Ladu Mjini Zanzibar.

Alisema inasikitisha kuona mazingira ya Wafanyabiashara katika maeneo hayo sio mazuri hasa ikizingatiwa kwamba Watendaji wa Manispaa hiyo wakati wote wamekuwa wakipita kukusanya Kodi lakini wanasahau kuwajengea mazingira bora Wafanyabiashara hao.

“ Tabia ya kuwataka Wafanyabiashara  kutoa Kodi Kazi inayotekelezwa na Watendaji wa Manispaa lakini wakashinwa wala kuandaliwa mazingira mazuri ukweli watakuwa wamewatendea haki Wafanyabiashara hao”. Alisema Mh. Hemed.

Mheshimiwa Hemed alibainisha kwamba Darajani, Mchangani, Mlandege hadi Muembeladu ni eneo muhimu linalolazimika kuwa katika mazingira safi kwa vile limekuwa likikusanya  Watu wengi wakiwemo Wageni wa Mataifa tofauti Duniani wanaolitumia kwa ajili ya Biashara.

Alionya kwamba tabia ya Viongozi, watendaji na hata wale wanaopewa majukumu ya kusimamia mazingira ya Mji kuendelea kubakia Maofisini wakati kwenye Mitaa majukumu yao yanaharibika haitavumilia na Serikali italazimika kuchukuwa hatua kali zinazostahiki dhidi ya Watendaji hao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametoa Siku Tatu kwa Uongozi wa Manispaa ya Mjini kuhakikisha kwamba tatizo la kusambaa kwa maji machafu kwenye eneo hilo linaondoka kabisa sambamba na kuendelea kuwekwa usafi wa mazingira muda wote wa Biashara.

Aliutaka Uongozi wa Manispaa hiyo kuunda Timu itakayofanya utafiti wa kujua chanzo ya ubovu wa Makaro katika eneo lote la Mlendege, Kwahaji tumbo hadi Biziredi ili kuwaondoshea hofu Wakaazi wa maeneo hayo hasa wakati wa Mvua za Masika zinazotishia Maisha yao kutokana na mazingira ya Karo nyingi.

Akigusia suala la vyombo vya Moto kwenye bara bara ya Biziredi hadi Darajani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaagiza Wafanyabiashara wa Maduka pembezoni mwa Bara bara hiyo kutokubali kuona mbele ya Maduka yao inakuwa sehemu ya maegesho ya vyombo vya Moto.

Alisema tabia hiyo inayoleta kero na kusumbuwa Wananchi wanaotumia Bara bara hiyo haitavumiliwa na Serikali kwani vyombo vya Dola kwa kushirikiana na Manispaa italazimika kulichukulia hatua ya kinidhamu suala hiyo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman amewahakikishia Wananchi kwamba dhamira ya Serikali isemayo yajayo yanafurahisha, yajayo nema tupu  imewalenga wao katika kuwapatia huduma bora zitakazostawisha Ustawi wao wa Maisha ya kila uchao.

Alisema hilo halina shaka kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Usimamizi wa Rais wake Dr. Hussein Ali Mwinyi imeshalivalia njuga jambo hilo na dalili ya kulitekeleza imeanza kwa kasi huku wale wanaoshindwa kwenda na mwendo huo wanaweza kukaa pembeni.

Mapema baadhi ya Wafanyabiashara wa Maduka wa maeneo hayo walimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba maji machafu yanayotiririka kwenye Bara  bara hiyo kutokana na uchakavu wa baadhi ya Makaro imekuwa changamoto kubwa  inayowasumbua kila siku.

Walisema zipo baadhi ya karo za maji machafu na vinyesi zilizokuwa kero kwa muda mrefu kati ya Miezi sita na hata Miaka Miwili licha ya kutoa Taarifa kwa mamlaka zinazohusika za Manispaa, Malaka ya Maji Zanzibar pamoja na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Wakizungumzia hali ya Mwenendo wa Biashara Nchini, Wafanyabiashara hao wameiomba Serikali kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuangalia hali halizi ya kodi wanazotozwa ni vyema zioane na hali ya muenendo mzima wa biashara Kimataifa.

Naye kwa upande wa wakaazi ya Mtaa wa Kwahajitumbo Mmoja wa Wananchi wa Mtaa huo Binti Sulubu Hassan alisema hali ya Makaro ya Nyumba zao sio ya kuridhisha kutokana na mazingira ya mtaa wao ulivyo.

Binti Sulubu alisema hali ya mazingira ya Mtaa huo inakuwa mbaya zaidi hasa wakati wa msimu wa Mvua kubwa jambo ambalo ni hatari zaidi kwa Watoto wao wadogo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.