Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi Ameutaka Uongozi wa ZIPA Kubadilika Katika Utekelezaji wa Majukumu Yao.Kufanikisha Dhamira za Uwekezaji.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisisitiza jambo wakati alipozumgumza na Uongozi wa  Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar ZIPA leo,katika Ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 15/12 2020. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kubadilika katika utekelezaji wa majukumu  yao ili kufanikisha dhamira za Wawekezaji.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar, wakati alipokutana na uongozi wa taasisi hiyo, ambapo walizungumzia utendaji kazi wa taasisi hiyo pamoja na kuzitolea ufumbuzi baadhi ya changamoto zinazokabili, ikiwemo za kukwama kwa baadhi ya miradi ya Uwekezaji.

Aliwataka watendaji hao kuhakikisha   ZIPA inakuwa kituo kimoja cha utoaji wa huduma zote za uwekezaji kwa muda mfupi (one stop centre), pamoja na kuwataka kuondokana na urasimu ambao umekuwa unawavunja moyo na kuwakimbiza wawekezaji.

Alisema iwapo taasisi hiyo  itafanyakazi zake kwa umakini na kwa weledi itasaidia sana kufanikisha dhamira ya Serikali ya kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Dk. Mwinyi alisema miongoni mwa sababu ya kuiweka Taasisi hiyo chini ya Ofisi yake ni kuhakikisha inafanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa na kufikia malengo.

Aidha, alisema pamoja na taasisi hiyo kutokuwa na ardhi kwa ajili ya uwekezaji, kuna nyakati ardhi hupatikana  lakini watendaji huendeleza utaratibu wa kupiga chenga, hivyo akatowa wito wa kupata taarifa zote za wawekezaji wenye nia ya kuwekeza, aina ya miradi pamoja na changamoto zinazowakabili.

Vile vile  aliitaka ZIPA kulifanya eneo lote la Mji mKongwe kuwa eneo la Uwekezaji  ili Serikali iweze kuingiza fedha na kukuza utalii.

Alisema eneo la Mji mkongwe lenye vivutio vingi vya Utalii ni muhimu, ikizingatiwa baadhi ya Wawekezaji tayari wameanzisha miradi ya hoteli kubwa  na hivyo kuingiza fedha nyingi.

Hata hivyo alisema pamoja na eneo hilo kuwa majengo kadhaa ya serikali, ikiwemo yale ya   Shirika la Nyumba Zanzibar pamoja Wakfu na mali ya Amana, bado uwepo wake haujainufaisha vya kutosha Serikali kwa vile majengo mengi yamekuwa yanakaliwa bila kulipiwa kodi.

Aliitaka ZIPA  kuwa taasisi ya kutafuta wawekezaji na kushughulikia masoko badala ya kusubiri wawekezaji kuja wao wenyewe.

Katika hatua nyengien Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wawekezaji kuwekeza katika visiwa pamoja na kuwataka wataalamu wa mazingira kutoa kanuni za kimazingira badala ya kuzuia miradi kufanyika.

Alisema kwa upande wake haoni sababu ya miradi ya Uvuvi katika kukwama na kubainisha kuwepo nia ya baadhi ya Wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo na hivyo akawataka kubainisha changamoto watakazokutana nazo ili Serikali itie mkono wake.

Alisema serikali inahitaji sana wawekezaji katika sekta ya uvuvi, hivyo akatoa wito wa kuja kuwekeza, sambamba na  kuwataka wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya umeme mbadala kufanya hivyo kwa msingi wa kuzalisha umeme  wa bei nafuu.

Aidha, aliitaka ZIPA kuanza kuifanyia kazi dhamira ya serikali ya kuimarisha sekta ya Utalii kisiwani Pemba.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA Salum Khamis Nassor, alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa uamuzi wa kukutana na uongozi wa taasisi hiyo, hatua aliyosema itafanikisha azma ya serikali ya kutekeleza Ilani ya CCM na ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni ya Uchaguzi mkuu.

Aliahidi kusimamia kikamilifu miongozo yote ya Serikali ili kuifanya ZIPA kuwa kituo kimoja cha kutoa huduma zote za Uwekezaji kwa muda mfupi (one stop centre).

Aidha, Mkurugenzi wa dara ya Miundombinu na Maeneo Huru Aziz Bakar Ali alisema katika dhamira ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa kituo muhimu cha Uwekezaji, tayari taasisi hiyo imekamilisha ‘master plan’ ya eneo la Micheweni.

Alisema ili kufanikisha azma hiyo kunahitajika miundombinu ya barabara ya wastani wa kilomita 3.4 kuelekea Micheweni, akibainisha tayari wameweka mapendekezo kwenye bajeti, hivyo wanahitaji kuungwa mkono na serikali.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.