Na.Beatrice Sanga- MAELEZO
Sekta ya Viwanda ni moja ya sekta zinazochangia pato la Taifa na kutoa ajira kwa wafanyakazi wengi hususan vijana wanaofanya kazi katika viwanda vidogo na vya kati. Sekta hii ina wajibu wa kukuza viwanda ikiwa ni pamoja na kuongeza ujuzi kwa vijana hawa na kuleta mabadiriko ya kiuchumi pamoja na kuwa miongoni mwa nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali iliweka nguvu kubwa katika
kufanikisha utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda sambamba na
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2020/21-2025 na Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo utekelezaji huo umehamasisha na
kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kufikia malengo ya maendeleo ya muda
mrefu kama yalivyoanishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 Ili
kuhakikisha sekta hii inachangia na kuleta tija katika uchumi wa Taifa hasa
ujenzi wa viwanda mama ( basic industries) na kuimarisha viwanda vilivyopo.
Katika
kutekeleza mikakati sekta ya viwanda imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja
na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji wa bidhaa viwandani kama vile viwanda
vya kusindika vyakula na matunda, viwanda vya nguo, viwanda vya kusindika pamba,
viwanda vya chuma na viwanda vya vifaa vya ujenzi. Uhamasishaji wa ujenzi wa
viwanda uliowekewa mkazo na Serikali ya awamu ya tano umepelekea ongezeko kubwa
la viwanda nchini kutoka viwanda 52,633mwaka 2015 na kufikia viwanda 61,110
mwaka 2020.
Juhudi
za makusudi zimeendelea kuchukuliwa katika uongezaji thamani wa malighafi za
ndani hususan katika sekta za kilimo, uvuvi, mifugo, maliasili na madini. Hatua
hizo zinasaidia kuchangia kuongezeka kwa uzalishaji na mauzo ya bidhaa ndani na
nje ya nchi na hivyo kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kupelekea kukua
kwa uchumi pamoja na kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii kama vile ujenzi
wa shule, miundombinu, hospitali na upatikanaji wa huduma za maji na nishati
Mafanikio mengi yaliyopatikana kutokana na
juhudi zilizofanywa na Serikali ni pamoja na uendelezaji na uanzishwaji wa
viwanda vya marumaru, saruji, chuma, vinywaji, na matunda, nyama, maziwa, nguo
na mavazi, bidhaa za plastiki na ngozi, hii yote ni katika kuhakikisha viwanda
vya ndani vinakua na kuweza kuchangia kukua kwa pato la taifa
Aidha
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita sekta hiyo imepata mafanikio
mbalimbali yakiwemo ukuaji wa viwanda na uzalishaji, ukuaji wa shughuli za
ujasiriamali, uboreshaji wa mifumo ya ununuzi wa mazao ya wakulima, matumizi ya
matokeo ya tafiti mbalimbali na matumizi ya fursa za masoko zilizopatikana
kutokana na majadiliano ya Kikanda na ya Kimataifa.
Kutokana
na mafanikio ya sekta hiyo, ajira mbalimbali kwa Watanzania na wageni kutoka
nchi mbalimbali zimeweza kuzalishwa ambapo sekta hiyo imeajiri zaidi ya
Watanzania milioni 9 ikiwa ni ya pili katika sekta za kiuchumi ikifuatiwa na
sekta ya kilimo
Ajira
hizo zimewezesha wahusika kujiongezea vipato na kutatua changamoto zao za
kijamii na kiuchumi. Pia, zimeweza kuongeza chachu katika azma ya ujenzi wa
viwanda nchini ambapo takribani asilimia 99 ya viwanda vyote nchini vipo chini
ya sekta hiyo.
Ukuaji
wa sekta hiyo una mchango mkubwa katika kuifikisha Tanzania katika uchumi wa
kati uliotangazwa hivi karibuni na Benki ya Dunia Vilevile, imebeba dhamana ya
nchi ya kukua zaidi kwa uchumi unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025, hasa
ikizingatiwa kuwa inashirikisha Watanzania wengi katika shughuli za kiuchumi.
Viwanda
vingi vilivyoanzishwa vimekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya
malighafi za Tanzania hususan ongezeko la mnyororo wa thamani kwenye mazao ya
kilimo.
Katika
kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika
msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na
miundombinu
wezeshi , Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), 2020 imeahidi kujenga na kukuza
uchumi shindani hususani kupitia sekta za viwanda na huduma za kiuchumi
utakaowezesha ustawi wa wananchi wote.
Kupitia
viwanda vidogo vya kati na vikubwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imejipanga kikamilifu kuhakikisha inatengeneza ajira zaidi kwa vijana kupitia
viwanda vya ndani ambapo itasaidia vijana kuwa na uwezo wa kujikimu na
kuchangia katika kuongeza pato la nchi.
Pia
Serikali imejipanga kuchochea ukuaji wa uchumi, hususan katika sekta ya viwanda
vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya
huduma za kiuchumi pamoja na utalii. Hii itapelekea kukuza uchumi wa nchi,
kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja, kupunguza umasikini na kuongeza uwezo wa
taifa kujitegemea.
Aidha katika miaka mitano ijayo Serikali inaenda kuimarisha mazingira ya ujenzi wa viwanda vya kimkakati kwa kufanya mapitio na maboresho ya sera za mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekeleza mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini( Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Envinroment). MWISHO
No comments:
Post a Comment