Habari za Punde

Serikali kuanza mikakati ya kuiboresha ZBC

Na Mwandishi wetu


Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Tabia Maulid Mwita amesisitiza suala la nidhamu, uwajibikaji, na ubunifu  ndani ya shirika la Utangazaji  Zanzibar (ZBC) ili lengo la kuliboresha shirika hilo na kuweza kufanya kazi zake kwa ufanisi liweze kufikiwa.

Akizungumza katika kikao na watendaji na wafanyakazi wa shirika hilo Mh. Tabia amesema muda umefika kwa kwa wafanyakazi wa shirika hilo kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili shirika liweze kupiga hatua zaidi za kimaendeleo.

"Nasisitiza sana suala la uwajibikaji, nidhamu na uwadilifu katika maeneo yetu ya kazi. Ifike mahali kila mmoja anapotoka nyumbani ajuwe anatakiwa aje afanye nini katika eneo lake la kazi" amesema Mh. Tabia 

"Kamati (ya uchunguzi ) imeshaanza kazi rasmi, wito wangu ni kutoa mashirikiano ya moja kwa moja kwa kamati hiyo kwani ina lengo la kuboresha ZBC huku nikiamini kwamba ni kiu ya kila mmoja kuona ZBC inakuwa TV au shirika la mfano, kwahiyo ni vizuri kuandaa mikakati, ushauri na njia mbali mbali ambazo zitaiwezesha ZBC kuwa Bora zaidi" amesisitiza Waziri Tabia

Aidha Mh. Tabia amemuagiza mkurugenzi wa shirika hilo kuyapatia ufumbuzi wa haraka baadhi ya matatizo yanayolikabili shirika hilo ikiwemo malimbikizo ya posho za wafanyakazi, usafiri, na uingiaji na matumizi wa mapato ya shirika.

"Jambo jengine ikifika muda zikitoka OC zile posho za lkizo au za elfu tano tano za  mikutano ya kampeni nataka walipwe wote, haki za wafanyakazi ambazo hawakupewa naomba sana wapewe haki zao haraka iwezekanavyo pindi itakapoingia OC"   

'"Lakini pia suala la pesa za baraza la wawakilishi kwamba nyuma zilikuwa zinatoka lakini sasaivi hazitoki, hapo zilipokuwa zinatoka wafanyakazi wamesema hawakupewa, kama hawakupewa yaisabiwe madeni yao na walipwe kwa wakati"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.