Habari za Punde

Wane waokolewa baada ya zoezi la uokozi kufuatia kuanguka kwa Beit al Ajaib

 Naibu Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar Kamanda Gora Haji Gora akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman jitihada walizochukuwa walinzi kuwaokoa Wajenzi Wanne walionasa kwenye kifusi cha Jumba la Beit El Ras Forodhani.
Hamad Matar Abdulla akiwa miongoni mwa walioangukiwa na Kifusi katika Jumba la Ajab Forodhani akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Dr. Khalid Salum Mohamed na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mh. Leila Mohamed Mussa jinsi alivyopata huduma baada ya Mtihani uliomkumba .

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed pamoja na Viongozi wenzake wa Serikali wakimfariji Mmoja wa wahanga wa ajali ya Jengo la Kihistoria ya Beir el ajaib liliopo Forodhani Mjini Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

 Vikosi vya Ulinzi na Usalama vikisaidiwa na baadhi ya wahandisi wanaosimamia matengenezo makubwa ya Jumba Kihistoria la Beit erl ajaib vimefanikiwa kuwaokoa Wajenzi Wanne wa Jengo hilo waliofukiwa na vifusi kufuatia kuporomoka kwa jengo hilo majira ya mchana wa sala ya Ijumaa  .

Zoezi hilo linaloendeshwa likiwa na vifaa vyote vya uokozi linaendelea kufanyika muda wote ili kuhakikisha kwamba kifusi hicho kilichoporomoka kinaondoshwa na hakuna Mwananchi aliyebakia katika eneo hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwa sambamba na Mawaziri pamoja na Viongozi wengine wa Serikali, Mikoa na Wilaya  ni miongoni mwa Wananchi walioshuhudia zoezi hilo.

Naibu Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar Kamanda Gora Haji Gora alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uokoaji wao ulilazimika kuwa na hadhari kubwa kutokana na mazingira halisi ya mporomoko wa kifusi cha Jumba hilo.

Kamanda Gora alisema ingawa Opereshi ya kuondoa Kifusi hicho itaendelea muda wote hadi sasa wamefanikiwa kuwapata Wajenzi Wanne katika kundi la Wajenzi Watano ambapo Mmoja alifanikiwa kuwahi kutoka katika dhahama hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman na Viongozi wenzake walifika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kuwakagua majeruhi wa ajali hiyo ambao wanaendelea kupata huduma za matibabu baada ya kufikwa na Mtihani huo. Pia alipata Fursa za kuwakagua wagonjwa wengine.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Dr. Marijan Msafiri alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Majeruhi hao wanaendelea na matibabu pamoja na uchunguzi Zaidi wa kiafya endapo wamepata athari yoyote katika miili yao.

Dr. Marijan alisema Wagonjwa Wawili kati ya Wanne wamelazimika kufanyiwa uchunguzi Zaidi Zaidi katika chumba cha Upasuaji baada ya kupata athari za miguu  kutokana na kuangukiwa na kifusi cha Jengo hilo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwapata pole Wajenzi hao na kuwataka kuwa na moyo wa subra kutokana na Mtihani uliowakumba na Serikali kupitia Wizara ya Afya itahkikisha kwamba wanaendelea kupata huduma zote hadi Wataalamu wa Afya watakapothibitisha kurejea katika hali zao za kawaida.

Jumba ya Ajab ambalo ni kielelezo cha Utamaduni na Historia ya Zanzibar kwa karne kadhaa sasa linaendelea kufanyiwa matengenezo makubwa chini ya ufadhili wa Serikali ya Oman.

Matengenezo ya Jengo hilo yanakwenda sambamba kwa kuzingatia vigezo vya uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao umo ndani ya Hifadi ya Urithi wa Kimataifa chini ya usimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, sayansi na Utamaduni {UNESCO}.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.