Habari za Punde

Wizara ya Elimu yatangaza tarehe za mitihani ya wanafunzi wa darasa la nne, la sita na kidato cha Pili


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  Mhe Simai Mohammed Said akizungumza na Waandishi wa habari  wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar (hawapo pichani)  kuhusiana mitihani ya Wanafunzi wa Darasa la Sita na la Nne inayotarajiwa kufanyika wiki ijayo.

 Na mwandishi wetu

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetangaza tarehe za kuanza kwa mitihani ya wanafunzi kuaniza darasa la nne, la sita na kidato pili.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Waziri wa wizara hiyo, Simai Mohammed Said alisema kuwa mitihani hiyo itaanza kufanyika kwa wanafunzi wa darasa la nne ambao watafanya kuaniza Disemba 14 hadi 15 mwaka huu.

Alisema kuwa wanafunzi wa darasa la nne walioandikishwa jumla yao ni 50,217 wakiwemo wanawake 24,688 na wanaume 25,529, idadi ambayo imepunguwa kwa watahiniwa 5,414 sawa na asilimia 9.73 ya mwaka 2019.

Aidha alisema kwa wanafunzi wa darasa la sita wao watafanya  Disemba 17 hadi 21 mwaka huu, ambapo walioandikishwa ni 34,029  wakiwemo wanawake 17,762 na wanaume 16,267 kukiwa na ongezeko la watahiniwa 1,721 sawa na asilimia 5.33 ikilinganishwa na mwaka jana.

Aidha waziri huyo alisema kuwa kwa wanafunzi wa kidato cha pili mitihani yao itaanza rasmi Disemba 22 hadi Disemba 31 mwaka huu, na wanafunzi 33,897 ndio walioandikishwa wakiwemo wanawake 18,409 na wanaume 15,488.

Waziri Simai alisema kuwa katika watahiniwa hao wa kidato cha pili kuna upungufu wa watahiniwa 576 sawa na asilimia 1.67 ikilinganishwa na idadi wa watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani mwaka 2019.

Sambamba na hayo alisema wizara yake imeandaa mazingira mazuri ya ufanyaji wa mitihani kwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu kulingana na aina ya ulemavu alionao.

“Watahiniwa wenye mahitaji maalumu wameandaliwa mitihani yao kwa mujibu wa hali ya uhitaji wao ikiwemo hati nundu na kukuza maandishi”, alisema Simai.

Alisema kuwa watu wenye mahitaji maalumu walioandikishwa jumla yao ni 1,244 wameandikishwa wakiwemo wa darasa la nne 364, darasa la sita 231 na kidato cha pili ni 649.

Hivyo aliwataka wazazi na walezi kuwapa hamasa watoto wao ili kufika katika vituo vyao vya mitihani kwa wakati kwa ajili ya kutumia haki yao ya msingi ya elimu sambamba na kuwaomba madereva kutoa ushirikiano kwa wananfunzi ili waweze kufika skuli kwa wakati.

Mbali na hayo Waziri Simai aliwasisitiza watahiniwa hao kuacha kufanya udanganyifu na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na kanuni za mitihani na atakaebainika kwenye kinyume na taratibu hizo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutiwa kwa matokeo yake.

Waziri Simai aliagiza kufungwa kwa kambi zote za kujiendeleza zilizowekwa ndani ya skuli za serikali na binafsi na zile zilizowekwa nje ya skuli kuanzia Disemba 11 mwaka huu.

Nae Madina Mjaka Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa wizara hiyo alisema wanafunzi wote wamekuwa wakipewa mafunzo sawa lakini kwa upande wenye mahitaji maalum  wamekuwa wakipewa upendeleo maalumu ukilinganisha na wanafunzi wa kawaida.

Hata hivyo, alisema kuwa katika ufundishaji kuna ngazi tofauti kuanzia msingi hadi sekondari, hivyo haiwezekani kuanza kufundishwa mafunzo ya amali kwa madarasa ya msingi jambo ambalo litamkosesha msingi mzuri wa ufundishaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.