Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais akutana na Uongozi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kuwasaidia Vijana wa Kike kupenda masomo ya Sayansi { FAWE}

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman akizungumza na Uongozi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kuwasaidia Vijana wa Kike kupenda  masomo ya Sayansi { FAWE} hapo Afisini kwake Vuga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kuwasaidia Vijana wa Kike kupenda  masomo ya Sayansi {FAWE} Dr. Mwatima Abdulla Juma akimueleza Mhe. Hemed wazo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kuwasaidia Vijana wa Kike kupenda  masomo ya Sayansi { FAWE} Dr. Mwatima Abdulla Juma akimueleza Mhe. Hemed wazo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo

Afisa Mkuu wa Taasisi ya Fawe Bibi Warda akielezea asilimia 75% iliyotengwa kuwasaidia Watoto wa Kike kwa kupatiwa sare pamoja na uwezeshwaji katika masomo ya ziada baada ya vipindi vya kawaida {Tuition}.

Picha na – OMPR – ZNZ

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Wana Jamii wanalazimika kujenga Utamaduni wa kuimarisha nguvu za Kujitegemea ili kuepuka athari za utegemezi wa nje ambao unaweza kuvuruga Mipango yao wanayoiweka  katika harakati zao za Maendeleo.

Akizungumza na Uongozi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kuwasaidia Vijana wa Kike kupenda  masomo ya Sayansi { FAWE} hapo Afisini kwake Vuga Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema mfumo wa kujitolea ndio ngao Kuu inayoweza kuleta mafanikio makubwa ya kujitegemea.

Alisema moyo wake umejenga matumaini makubwa kutokana na uwepo wa Taasisi hiyo ya Fawe iliyojikita kumkomboa Mtoto wa Kike kwa kumuandalia njia ya kujiamini katika Maisha yake ndani ya mfumo wa sasa wa Teknolojia utakaomsaidia kuepuka majaribu mbali mbali yaliyomzunguuka.

“Hongereni sasa Wana Fawe kwa mikakati yenu ya kumkombnoa Mtoto wa Kike  katika kumjengea uwezo wa kuyamudu masomo yake ya sayansi yenye ushawishi mkubwa wa kupata ajira katika Karne ya sasa ya Teknolojia”. Alismema Mh. Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikubaliana na wazo la Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Thabit Idarous Faina  la kuushawishi Uongozi wa Taasisi hiyo isiyo ya Kiserikali kufikiria wazo la Kuanzisha  Skuli Maalum ya Sayansi itakayowapa mwanga Watoto wa Kike katika kuwajengea uwezo Zaidi wa kitaaluma.

Alisema kufanikiwa kwa suala hilo kwa upande mwengine unaweza kujenga Historia Mpya kwa Vijana wa  Kike kuondokana na mfumo Dume uliojengeka kwa baadhi ya familia Nchini kuonekana kama ni Mtoto wa huduma za Nyumbani pekee.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kuwasaidia Vijana wa Kike kupenda  masomo ya Sayansi { FAWE} Dr. Mwatima Abdulla Juma alisema wazo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo limekuja kufuatia Mkutano wa Mawaziri wa Elimu wa Mataifa ya Kusini  na Mashariki mwa Bara la Afrika  waliokutana katika Miaka ya 2000 kujadili namna wanavyoweza kumuandaa Mtoto wa Kike kupenda Masomo ya Sayansi.

Dr. Mwatima alisema Taasisi ya Fawe ni matokeo ya chimbuko la Mkutano huo wa Mawaziri wa Elimu wa Afrika ambayo tayari kwa sasa imekuwa mshirika mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar katika kuwaandalia mazingira bora Wanawake kupenda Sayansi.

Alisema upo mfano hai wa mafanikio ya Taasisi ya Fawe pale ilipojikita kushawishi Wazazi kuwahimiza Watoto wao katika Skuli ya Kijini Matemwe hasa wale wa Kike kupenda Elimu ya sayansi ushawishi uliokwenda sambamba na kundi kubwa la Watoto kuendelea na masomo yao baada ya kuacha kutokana na mazingira na sababu mbali mbali.

Naye kwa upande wake Afisa Mkuu wa Taasisi ya Fawe Bibi Warda alisema Zaidi ya asilimia 75% ya Watoto wa Kike hapa Zanzibar wamekuwa wakiungwa mkono na Taasisi hiyo kwa kupatiwa sare pamoja na uwezeshwaji katika masomo ya ziada baada ya vipindi vya kawaida { Tuition}.

Bibi Warda alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Fawe kwa kushirikiana na Taasisi nyengine isiyo ya Kiserikali ya Milele Foundation zimeanzisha Klabu 30  za Wanafunzi Unguja na Pemba ili kupata wasaa wa kujipima kiwango chao cha Elimu.

Alisema hatua hiyo ilikwenda sambamba na Uwezeshwaji wa baadhi ya Wanawake  kwenye Miradi yao ya ukulima wa Mwani ingawa kwa sasa uwezeshaji huo umefifia kutokana na mripuko wa maambukizo ya Virusi vya Corona Duniani uliosababisha Wafadhili wengi kuelekeza nguvu zao kwenye Sekta ya Afya. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.