Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais akutana na Uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampas ya Karume

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, akifanya mazungumzo na uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampas ya Karume, alipokutana nao ofisini kwake Vuga Zanzibar.

Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Pro Shadrack Mwakalila akielezea azma ya Uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampas ya Karume utaratibu wa kuanza Ujenzi wa Majengo ya Dakhalia ili kuwaondoshea usumbufu Wanafunzi wake.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Uwepo wa waatalamu wa fani tofauti wanaofinyangwa kupitia vyuo mbali mbali nchini, ni moja ya sababu inayopelekea kupatikana kwa taifa la wasomi watakaochangia kuleta maendeleo kwenye sekta mbali mbali nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ameyasema hayo alipofanya mazungumzo na uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, alipokutana nao ofisini kwake Vuga Zanzibar.

Alisema Serikali inathamini mchango wa vyuo vya Taalum akitolea mfano chuo cha Kumukumbu ya Mwalimu Nyerere, kinachoendelea kutoia wataalamu wa kadi tofauti, na kuupongeza Uongozi wa Chuo hicho kwa uono wao wa  kuanzisha kampasi Kisiwani Pemba.

Mh. Hemed alieleza kwamba hatua hiyo muhimu itasaidia Zaidi Wananchi na hasa Vijana wa Zanzibar kuendelea kupata taaluma kwa urahisi zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mafanikio yaliyopatikana ndani ya uongozi wa Chuo hicho yanatokana na mashirikiano ya kina na ameuhakikishia Uongozi wa Chuo hicho kwamba serikali itaendelea kuwaunga mkono huku ikiwataka nguvu za ziada katika kukikuza chuo hicho ili kizidi kukuza taaluma nchini.

Alibainisha kwamba kwa vile watanzania wanaendelea kufaidi matunda ya Chuo hicho, ipo haja ya kutanua wigo wa elimu nchini, kwavile wahitimu wa Taasisi hiyo tayari  wanatumika katika sekta mbali mbali za Serikali na hata zile binafsi.

Mheshimiwa Hemed ameelezea faraja yake kutokana na kasi ya Taasisi hiyo ya Elimu inayokwenda sambamba na utayari wa Awamu ya Nane wa kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwategemea Zaidi wasomi hao.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Pro Shadrack Mwakalila amesema Wanafunzi na hata Wakufunzi wa Chuo hicho wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Dakhalia.

Katika kukabiliana na tatizo hilo linalichangia kupunguza muda wa masomo Prof Mwakalila alieleza kwamba Uongozi wa Chuo hicho umeshaandaa utaratibu wa kuanza ujenzi wa hMajengo ya Dakhalia itakayotoa huduma kwa wanafunzi 1,960.

Aidha Pro. Mwakalila alieleza kuwa licha ya kuwapa elimu wanafunzi chuoni hapo, pia wanawajenga kuwa na uelewa wa uongozi na maadili, pamoja na mbinu za kujua namna bora ya kujiajiri ili kuondokana na dhana ya kusubiri ajira serikalini.

Kwa kutambua uwajibikaji wa serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dr Hussein Ali Mwinyi, Pro Mwakalila amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman kwa utendaji wake ambao unaleta matumaini makubwa kwa watanzania.

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar kilianza na wanafunzi 22 mwaka 2013, ambapo hadi kufikia 2020 kina jumla ya wanafunzi 1,920.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.