Habari za Punde

Makamu wa PIli wa Rais atembelea Nyumba ya Kulelea Watoto Yatima ya Mazizini na Nyumba za Serikali za Kutunza Wazee Welezo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla Kushoto akionyesha kutoridhika kwake na mazingira halisi ya Vyumba wanavyolala Watoto wanaoishi kwenye Nyumba ya Watoto Yatima iliyopo Mazizini.

Kushoto ya Mh. Hemed ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Idrissa Kitwana Mustafa, Msimamizi Mkuu wa Nyumba ya Kulelea Watoto Yatima ya Mazizini Bibi Pili Sadalla Mussa na wa kwanza Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dr. Omar Dadi Shajak.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akimjuilia hali Mmoja wa Wazee wanaoishi kwenye Nyumba za Serikali za Kutunza Wazee zilizopo Mtaa wa Welezo Wilaya ya Magharibi A.

 Msimamizi Mkuu wa Nyumba za Hifadhi ya Wazee zilizopo Sebleni Bibi Ashura Suleiman akimtembeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akimtembeza maeneo mbali mbali ya Nyumba za Wazee Sebleni kujionea hali halisi ya Mazingira ya eneo hilo.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema Watendaji wa Taasisi za Ustawi wana jukumu kubwa la kusimamia matunzo ya Wazee wa Nyumba za Welezo na Sebleni ikiwa ni utekelezaji wa dhima iliyoshiba ucha Mungu utakaowapatia malipo mengine makubwa ya hapo baadae.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema hayo wakati akizungumza na Viongozi, Wafanyakazi pamoja na Wazee Wanaohifadhiwa Nyumba za Sebleni na Welezo alipofanya ziara Maalum katika Mikutano Miwili tofauti kuangalia mazingira halisi ya Makaazi ya Wazee hao pamoja na kufahamu changamoto zinazowakabili kila siku.

Alisema pale zinapoibuka changamoto, matatizo na hata kasoro ndogo ndogo ni vyema kwa Watendaji hao kwa kushirikiana na Viongozi wao waziwasilishe katika ngazi husika bila ya kuvunjika moyo ili yale malengo ya Serikali ilipoamuwa kuwapatia huduma za Makaazi Wazee wasiojiweza yalete mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Hemed alitahadharisha kwamba hakuna hata Mzee Mmoja anayeweza kulalamika bila ya kuwa na sababu yoyote. Hivyo kinachohitajika katika mazingira hayo ni kuona busara zaidi zinatumika katika kuwapatia huduma Wazee hao  ili waendelee kuishi kwa Amani na upendo mkubwa.

Alibainisha kwamba Wazee lazima wahudumiwe ipasavyo kutokana na hali halisi ya maazingira yao Kiumri na Afya zao ambazo hazistahiki hata kidogo kukaa na nja muda mrefu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kuandaa utaratibu maalum wa  kila Mwezi utakaoweza kuwapatia huduma za Afya Wazee hao.

“Iwe mwiko kwa Mzee mwenye Umri mkubwa kukaa foleni ya kumuona Daktari kwa ajili ya kupata huduma za Kiafya. Wao kwa umri wao wanahitaji kutunzwa katika mazingira bora”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed Suleiman.

Mheshimiwa Hemed alisema haipendezi na ni jambo la masikitiko kuona Mzee mwenye umri mkubwa analazimika kupanga mstari wakati anapohitaji huduma za Afya Hospitalini.

Mapema Wazee wa Nyumba hizo mbili za Sebleni na Welezo wameipongeza Serikali Kuu kwa hatua zake inazoendelea kuzichukuwa za kuwahifadhi sambamba na kuwahudumia Wazee hao.

Walisema huduma za chakula pamoja na nguo kwa baadhi ya wakati hasa inapofikia kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramnadhani wamekuwa wakipata matumaini makubwa yanayowaletea faraja katika Maisha yao ya kawaida.

Hata hivyo Wazee hao waliomba kuangaliwa Zaidi kiwango cha fedha wanazopatiwa na Serikali kwa kila mwezi ili ziendelee kuwahudumia katika mahitaji yao madogo madogo ya kila siku.

Kwa upande wao baadhi ya Watendaji wa Ustawi wa Jamii wanaowahudumia Wazee hao wa Sebleni na Welezo walikumbusha kupatiwa maposho yao ya muda wa ziara pamoja na  yale ya kipindi cha mripuko wa Homa Kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona {Covid - 19}.

Watendaji hao walisema  muda wao mwingi wamekuwa wakiutumia kuwahudumia Wazee hao jambo ambalo wanashindwa kupata muda mwengine wa ziada kuweza kutafuta riziki ili kujiongezea kipato kitakachokidhi mahitaji yao ya msingi.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliitembela Nyumba ya Kulelea Watoto Yatima iliyopo Mazizini ili kungalia changamoto na matatizo yanayowakabili Watoto hao wanaohitaji kupata huduma stahiki kama walivyo Watoto wengine.

Wakielezea changamoto zinazowakabili Watoto hao walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ipo haja ya kupewa kipaumbele katika masomo yao kwa kupatiwa Mwalimu wa masomo ya ziada kama wanavyopata huduma hizo Wanafunzi wa Mitaani.

Walisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mashirikiano katika malezi yatakayosaidia kuwapunguzia changamoto zinazowapata ikiwemo kupewa adhabu wakati mwengine kutishiwa kufukuzwa katika Nyumba hiyo pale zinapotokea hitilafu baina yao na Walezi wao.

Akitoa ufafanuzi wa changamoto hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ameuamuru Uongozi wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto kumpangia Kazi Nyengine Msimamizi Mkuu wa Nyumba hiyo ya Kulelea Watoto Yatima ya Mazizini baada ya kushindwa kuwajibika katika majukumu yake.

Mheshimiwa Hemed akiangalia mazingira halisi ya Makaazi ya Watoto hao ambayo hakuridhika nayo alisema Watoto wanahitaji kuhudumiwa na kuacha tabia ya kusimangwa ili kuwapa matumaini bora ya maisha yao huku akihimiza uwepo wa Mwalimu maalum atakayewasaidia katika masomo ya ziada.

Aliwahakikishia Watoto hao kwamba yeye pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi wataangalia mfumo utakaowezesha kupata Magodoro yatakayokidhi Vitanda vyao badala ya yale wanayoyatumia hivi sasa ambayo baadhi yao wanalazimika kuyatumia chini ya sakafu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuonya Mkandarasi anayesimamia matengenezo ya Nyumba hiyo kukamilisha utiaji wa Milango ya Makabati ndani ya Vyumba vya Nyumba hiyo katika kipindi kisichozidi Wiki moja kuanzia hivi sasa.

Alisema kwa vile matengenezo hayo madogo tayari yameshachukuwa Wiki Tatu sasa kuna haja kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto kuangalia Mkataba uliotiwa saini juu ya Matangenezo hayo na ikibainika uwepo wa uzembe Serikali haitasita kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya Mkandarasi husika.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.