Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amefika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Kuwafariji Wanamichezo Waliopata Ajali

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwafariji Wanamichezo waliopata ajali ya kuvamiwa na gari  katika barabara ya Migombani wakati wakiwa katika mazoezi Ndg. Sastenesi Amasi na Ali Abdulla, waliolazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiondoka katika viwanja vya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar baada ya kuwatembelea na kuwafariji Wanamichezo wa Kundi la MUWAFAKI waliopata ajali ya kuvamiwa na gari wakati wakiwa katika mazoezi barabara ya migombani Jijini Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewapa pole wanamichezo wa kundi Shirikishi la mazoezi la MUWAFAKI waliopata ajali ya kugongwa na gari iliyokuwa ikienda mwendo kasi.

Rais Dk. Mwinyi amewapa pole majeruhi hao na kumuomba Mwenyezi Mungu awape nafuu na waendelee kupona haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kimaisha.

Kwa mujibu wa maelezo ya Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dk. Marijani Msafiri Marijani ajali hiyo imetokea leo (02.01.2021) mapema asubuhi huko katika barabara ya Migombani Jeshini, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi na kusababisha majeruhi 14.

Rais Dk. Mwinyi alielezwa kuwa ajali hiyo imetokea wakati kundi hilo la MUWAFAKI likifanya mazoezi ambalo linajumuisha vikundi Vitano kikiwemo kikundi cha Kitambi noma kutoka Zanzibar, kikundi cha Fighter na Wakali kutoka Dar-es-Salaam, kikundi cha Muungano kutoka Dodomana kikundi cha Uluguru kutoka Mkoani Morogoro..

Wanamichezo hao wa kundi hilo ambao jana walishiriki kikamilivu katika Bonaza la Maadhimisho ya Siku ya Mazoezi ya Viungo Kitaifalililofanyika hapa Zanzibar ambapo kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Marijani majeruhi hao wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mnazi Mmoja na watano miongoni mwao wamepata huduma na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Ajali hiyo imesababishwa na mwendo kasi wa gari aina ya IST yenye namba za usajili 634 HK iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Nassor Jabir Magondi ambae alikuwa akiendesha gari hiyo kwa mwendo wa kasi licha ya kuonyeshwa kibendera chekundu na miongoni mwa wasimamizi wa kundi hilo la mazoezi lakini gari hiyo ilimshinda na kuwagonga wafanyamazoezi hao.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.