Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Ameifungua Barabara Mpya ya Kiwango Cha Lami Matemwe hadi Muyuni Kuadhimisha Miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa katikati akitembea kwa miguu mara baada ya kuifungua Barabara ya Matemwe -Muyuni(7.6km)Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja.  Ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi Zanzibar.

Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar. 8/1/2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaaliwa Majaliwa ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa barabara mpya iliyojengwa Matemwe Muyuni kutokana na uimara na ubora wa barabara hiyo.

Ameyaesma hayo huko Matemwe Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho mara tu baada ya kuifungua barabara hiyo ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa barabara hiyo itarahisisha wananchi na wakaazi wa hapo kuondokana na adha ya usafiri iliyodumu kwa muda mrefu na kujieletea maendeleo kwa kuweza kusafirisha biashara zao kwa urahisi zaidi.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutaweza kukuza sekta ya uwekezaji kwa wageni mbalimbali wanaokuja kuwekeza kutokana na kuwepo miundombinu imara yenye kuvutia na kupelekea kupata pato la Taifa.

Waziri Mkuu amefahamisha kuwa Serikali inaimarisha miundombinu ya barabara za lami kwa wananchi ili kuwaondoshea usumbufu na kuwapatia hudma muhimu za kijamii Mjini na Vijijini ikiwa ni kutekeleza ahadi kwa asilimia 98.

Waziri Majaliwa ameelezea kuwa barabara ya Matemwe Muyuni ni kiungo muhimu kwa Mkoa wa Kaskazini kwani imeweza kuunganisha barabara mbalimbali ikiwemo Pongwe Chwaka na Kiwengwa ili kuimarisha mawasiliano ya karibu kwa wananchi.

Hata hiyo amewataka wananchi wa Kijiji hicho kuchangamkia fursa zilizopo pamoja na kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kusisitiza kuepuka kukaa pembezoni mwa barabara ili kujikinga ajali.

Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa barabara hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Mustafa Aboud Jumbe amesema ujenzi wa barabara hiyo ni jitihada za Serikali ya Mapinduzi  ya kuwaetea maendeleo wananchi pamoja na kuimarisha miundombinu muhimu nchini.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 7.58 imejengwa kwa mkopo kutoka Bank ya Maendeleo ya Afrika(AfDB) kupitia mkandarasi kutoka China (China Civil Engeneering Construction Corparation  CCECC) chini yay a usimamizi wa Kampuni ya Ujerumani Gauff ambayo imegharimu bilioni 5.8 hadi kukamilika kwake

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.