Na Lilian Shembilu-MAELEZO
Serikali
ya Burundi imeipongeza Tanzania kwa kuendelea kuongeza fursa kwenye sekta ya
madini ambayo imeonesha mafanikio makubwa katika kukuza uchumi wa nchi na
kuinua vipato vya wananchi kwa ujumla.
Hayo
yamebainishwa na mwakilishi kutoka nchini Burundi, Niongao John Bosco katika Mkutano
wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika jijini Dar es
Salaam.
Aidha,
ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini kwa mualiko wa
mkutano huo kwa kuwa ni fursa kubwa kwao kwa sababu wamejifunza mambo mengi
kupitia mada zilizowasilishwa na ameiomba Tanzania kudumisha uhusiano mzuri wa
nchi hizo mbili kupitia sekta ya madini.
“Nimejifunza
mambo mengi kuhusu uandaaji wa shughuli za madini na mkutano huu umekuwa wenye
manufaa makubwa katika kukuza sekta ya madini nchini kwetu Burundi” alisisitiza
Bosco.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila
amewashukuru watoa mada na washiriki wote kwa kuchangia hoja nyingi zenye
mashiko ambazo zitaleta tija kwenye sekta ya madini nchini.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima ameipongeza Wizara ya Madini kwa
mabadiliko makubwa yanayoendelea kwenye sekta hiyo ambayo yamepanua wigo katika
biashara ya madini ikilinganishwa na miaka 6 iliyopita.
“Katika
kikao hiki yamezungumzwa mambo makubwa sana hivyo Wizara inatakiwa kuyazingatia
na kuyafanyia kazi. Naomba Wizara iteue kamati ya watu 10 ili iweze kusimamia
hoja zilizojadiliwa kwenye mkutano huu” alisema Malima.
Pia
Malima amewataka wachimbaji wadogo kujikusanya kama wafanyabiashara ili waweze
kusaidiwa hasa katika mikopo na kuacha migogoro pamoja na kulalamika katika
maeneo yao.
Sambamba
na hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Danstan Kitandula
ameipongeza Wizara ya Madini na kubainisha kuwa yote hayo ni matokeo ya uongozi
uliotukuka wa Rais John Pombe Magufuli, usimamizi mzuri wa Waziri wa Madini
Dotto Biteko pamoja na timu yote ya madini.
“Ni
vyema changamoto zote kuhusu sekta ya madini zipatiwe ufumbuzi ili wajumbe wa
mkutano huu wasione wanapoteza muda. Maarifa yatumike ili changamoto za kikodi
ziweze kutatuliwa kwani zimekuwepo kwa muda mrefu sasa” alisisitiza Kitandula.
Akifunga
mkutano huo wa siku tatu Waziri Biteko aliwashukuru wadau wote waliohudhuria na
walioshiriki kwa njia ya mtandao, ambapo mada tisa na hoja 17 ziliwasilishwa.
Pia amewahakikishia kuwa sekretarieti itazifanyia kazi.
“Kongamano
hili ni maono ya Mheshimiwa Rais na ukweli ni kwamba manufaa yake yanazidi
kuonekana na mara zote maelekezo yake yanakazia Watanzania wafaidike na madini”
aliongeza Biteko.
Mkutano
wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini ulilenga kuwakutanisha wadau
wa sekta ya madini wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujadili na kupeleka
mbele sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuvutia wawekezaji.
Pamoja na hayo mkutano huo ulilenga kubainisha fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kuhamasisha matumizi ya teknolojia kwa wachimbaji wadogo, kuzikutanisha taasisi za kifedha na wadau wa madini ili taasisi hizo ziweze kujifungamanisha na sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi.
No comments:
Post a Comment