Habari za Punde

MHAGAMA ARIDHISHWA NA UTENDAJI TACAIDS

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akieleza jambo kwa wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati 
Mkurugenzi   Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt.  Leonard Maboko akijibu hoja za wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya walizowasilisha wakati wa kikao cha kamati hiyo

Na Mwandishi Wetu- Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi,Vijana ,Ajira na Wenye Ulemavu  Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI zimeendelea kuimarika hapa nchini.

 

Ameyasema hayo Februari 4, 2021katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) ikilenga kujenga uwezo kwa wajumbe hao kuhusu  majukumu ya Tume na utekelezaji wake.

 

“Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI milioni 1.2 walikuwa wanapata huduma za dawa za kufubaza virusi hivyo pamoja na kuimarika kwa huduma za upimaji wa virusi hivyo na utoaji wa elimu kuhusu Virusi hivyo na UKIMWI”,alisema Mhagama

 

Aliongezea kuwa, ofisi yake kupitia Tume ya Kuthibiti UKIMWI nchini itaendelea kutoa elimu kuhusu kinga dhidi ya VVU ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU hususani kwa vijana kupitia kampeni mbalimbali za mabadiliko ya tabia zinazolenga kuyafikia makundi yote.

 

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Alice Kaijage amesema kuwa wajumbe wa Kamati hiyo wataendelea kutoa michango yao ili kuiwezesha Tume hiyo kuimarisha zaidi utendaji wake hasa katika mapambanao dhidi ya UKIMWI.

 

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe.Ummy Nderiananga amesema kuwa Ofisi hiyo itachukua na kufanyia kazi ushauri uliotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo ili kuimarisha utendaji wa Tume na Mapambano dhidi ya UKIMWI.

 

Naye Mkurugenzi  Mtendaji wa  Tume hiyo Dkt. Leonard Maboko amesema kuwa kwa sasa mwamko wa wananchi kujitokeza kupima na kujua hali zao umeongezeka katika makundi mengi isipokuwa kundi la wanaume bado mwamko hauridhishi.

 

“Inakadiriwa hadi kufikia Disemba 2019 watu wazima 1,612,301 wenye miaka 15 na zaidi walikuwa wameambukizwa Virusi vya UKIMWI ambapo wanawake ni 983,471 na wanaume 628,830 na watoto chini ya miaka 15 walikuwa 93,000”alieleza Dkt. Maboko.

 

Naye mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo aliipongeza Tume kwa kuwajengea uwezo kuhusu muundo na utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha alitoa rai kwa kundi la vijana kuendelea kujitokeza kwa wingi kupima na kujua hali zao.

 

“Kamati tumefarijika kwa namna Tume ilivyojipanga kuhakikisha inaendelea kuelimisha makundi yanayoongoza kwa maambukizi mapya hasa vijana hivyo ni vyema kundi hili likawekewa mikakati ya makusudi ili kusaidia kukabili hali hiyo, kamati itaendelea kuunga mkono mapambano hayo,”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.