Habari za Punde

Ulega aitaka TIRA kusimamia mikataba ya Bima iandikwe kwa lugha ya Kiswahili

 

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Abdallah Ulega (wa tatu  kulia) akifafanua kuhusu matumizi ya kiswahili kwenye mikataba ya bima kwa alipotembelea ofisi za Mamlaka zilizoko Jijini Dar es Salaam.


Na Grace Semfuko - MAELEZO.                                                                       

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), kuzielekeza taasisi za bima nchini kutumia lugha ya Kiswahili katika mikataba ya wateja wao ili waielewe kabla ya kuingia katika mikataba hiyo lengo likiwa ni kutoa haki kwa wateja.

Ulega amesema wananchi wengi wanaingia katika mikataba mbalimbali ya Bima ambayo inaandikwa kwa lugha ya kigeni na matokeo yake wengi wamekuwa wakidhulumiwa haki zao kutokana na kutoisoma mikataba hiyo kufuatia kuchapishwa kwa lugha za kigeni.

“Lengo la kuja hapa ni kuja kusisitiza mikataba ya bima kwa wananchi iandikwe kwa lugha ya Kiswahili, tumekubaliana kuwa huduma za bima zitakwenda kwa Kiswahili, kwa kuwa kwenye bima kuna mambo mengi ambayo yanatakiwa yatafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili kama vile Sera za Bima. Haya yote yanatakiwa yajulikane kwa mawakala na makampuni yanayofanya shughuli za bima moja kwa moja kwa wananchi, sasa wanatakiwa kutafsiri mikataba yao iwe kwa lugha ya Kiswahili,” alisema Ulega.

Aidha, Ulega alisisitiza kuwa ili kuondokana na migogoro inayohusu  bima baina ya wananchi na makampuni ya Bima ni muhimu kuangalia upya lugha zinazotumika kwenye mikataba hiyo hatua ambayo Bima wamesema wameanza kuifanyia kazi.

“Namshukuru sana Kamishna wa Bima, amenihakikishia kwamba bima zinazokwenda moja kwa moja kwa wananchi ni lazima ziwe za lugha ya Kiswahili, lengo ni kuhakikisha wananchi wengi wanakata bima, na wanakwenda katika kukuza uchumi wa Taifa letu, sasa watakwenda kutumia lugha ya Kiswahili kwa sababu ndio lugha inayoeleweka zaidi na ninayo imani kwamba wananchi wengi wataingia kwenye utaratibu huu wa bima kwa sababu kile kitu wanachokiingia watakuwa wanakielewa kwa urahisi” aliongeza Ulega.

Kwa upande wake Kamishna wa Bima kutoka TIRA,  Dkt. Mussa Juma amesema zoezi hilo limeanza kufanyiwa kazi kwa kuziagiza taasisi zinazotoa bima nchini kutafsiri mikataba yao kwa lugha ya Kiswahili ambapo kufikia mwezi Juni zoezi hilo litakuwa limekamilika.

“Wazo la kutafsiri lugha ya Kiswahili lilitokana na changamoto, maoni na malalamiko ya wananchi, wengi wanashindwa kulipwa haki zao kwa sababu wanakuwa hawajaelewa kilichoandikwa kwenye mkataba huo, mtu anakuwa na huo mkataba bila kuelewa kwamba analipwa au halipwi, na anapokuja kudai anaambiwa mbona tumeandika kwenye mkabata wako kwamba hiki kitu hakilipwi? ndio maana tukaona kuna kila sababu ya kutafsiri mikataba hiyo ili kutowanyima haki wananchi” alisema Dkt. Juma.

Ulega amefanya ziara hiyo TIRA lengo likiwa ni kuimarisha lugha ya Kiswahili kwenye shughuli za bima na kuwafanya wananchi kunufaika na shughuli hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.