Habari za Punde

Waandishi wa habari Mkoani Tanga watakiwa kujiunga na NHIF


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAANDISHI wa habari mkoani Tanga kupitia Club yao Tanga Press wametakiwa kujiunga na huduma za Mfuko wa Bima ya Afya Nchini (NHIF) ili kupata unafuu kwenye matibabu kwani mfuko huo kwa sasa umeboreshwa na unatoa huduma zote kwa weledi mkubwa.

Akizungumza na nipashe jana ofisini kwake, Meneja wa NHIF mkoani hapa Ally Mwakababu alisema kuwa anashangazwa na hali ya waandishi wa habari mkoani hapa pamoja na uweledi wao lakini wamekua wazito kujiunga na mfuko huo ikizingatiwa wao ndio wahamasishaji na waelimishaji wakuu wa jamii kwa kuwapasha habari na kujiunga.

Mwakababu alisema kuwa karibu mikoa yote waandishi wamehamasika na kupitia vyama vyao wamejiunga na huduma zao lakini kwa mkoa huu bado wanaendelea kuwahamasisha ili nao wapate kunufaika na huduma kwani mfuko huo ndani ya mkoa umefanya maboresho makubwa katika hospitali ya Rufani ya Bombo pamoja na wilaya zote za mkoa.

"Huduma za bima ya afya zipo mpaka kwenye ngazi ya wilaya, pale kuna Mratibu wa huduma za afya kupitia ofisi ya mganga mkuu wa halmashauri husika, lakini kila mahali, kila halmashauri tumesajili maduka ya dawa pia tumeboresha huduma katika vitengo vya usafishaji wa figo, mama na mtoto, huduma za I.C.U uangalizi maalimu pamoja na huduma za dharura" alisema Mwakababu.

Aidha alifafanua kwamba NHIF mkoani hapa miaka ya nyuma ilikiwa chini ya mkoa wa Kilimanjaro na haikuwa na huduma zilizoboreshwa ambapo wagonjwa waliokua na matatizo kama ya kusafisha figo walikua wakifuata huduma nje ya mkoa kwenye hospitali za Rufani lakini tangu wameamua kuisimamia kimkoa huduma zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa na zinafanyika kiuweledi.

"NHIF kwa mkoa wa Tanga imewekeza zaidi ya shilingi milioni 650 kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020 kwa ajili ya kuboresha huduma ambazo hazikuwepo kupitia mfuko katika hospitali ya Rufani ya Bombo, kwahiyo sasa hakuna tena hata zile harakati za kutoa wagonjwa Bombo na kuwapeleka hospitali nyingine kubwa kwa mambo ambayo yanawezekana katika hospitali hiyo" alifafanua.

"Watu huko nyuma walikuwa wakisema hili tatizo haliwezekani lakini sasa linawezekana, kwa kwenye wodi ya akinamama vyumba vya kujifungulia vilikua vichache lakini sasa ukienda kule mpaka upasuaji unafanyikia kulekule badala ya kwenda kwenye chumba cha upasuaji" aliongeza.

Mwakababu alibainisha kwamba zamani ilizoeleka watu wanaopata huduma za NHIF ni watumishi pamoja na watoto wao lakini kwa sasa baada ya uboreshwaji wa huduma hata mfanyabiashara mdogo anaweza kujiunga na huduma hiyo huku akiongeza kwamba bado wanahamasisha wananchi wote kujiunga ili kupata unafuu wa huduma za matibu kuliko kusubiri kuugua au kuuguliwa na kuanza kupata garama za matibabu.

Hata hivyo Mwakababu alitoa wito kwa waandishi wa habari pamoja na wananchi wote wa Tanga kujiunga na mfuko huko kwani kwa sasa unasimama kama Daktari, huduma na pesa kutokana na mgonjwa mwenye kadi ya NHIF kua na uwezo wa kuchagua kituo cha matibabu kwa kufuata huduma za Daktari anayemtaka yeye amtibu na kuongeza kuwa mfuko huo kwa sasa ni mpya kwani umebadilika kwa kuboreshwa sio kama zamani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.