Habari za Punde

Viongozi wavutana sakata la Rushwa Zanzibar

Na Mwandishi wetu, Zanzibar


VIONGOZI  Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwezeshaji Zanzibar  wameanza kuvutana kuhusu Kiongozi Mwandamizi wa Kamisheni ya Kazi, Khamis Omar kuendelea na kazi wakati anakabiliwa na kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni moja.

Kaimu Kamishina wa Kazi Suleiman K. Ali alisema pamoja na kutokea kwa tukio hilo lakini yeye sio msemaji zaidi ya Mkurugenzi wa uendeshaji na utumishi wa wizara.

‘Mimi nikilazimika kuzungumzia jambo hili nitalazimika kuitisha faili kutoka kwa wahusika ndio maana  nakuombeni muoneni Mkurugenzi wa uendeshaji na utumishi yeye ndio muhusika wa masuala ya watumishi.”alisema Suleiman.

Hata hivyo akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini Kwake Mwanakwerekwe Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi, Januari Fussi  alisema kwa mujibu wa mgawanyo wa madaraka msemaji wa jambo hilo ni Katibu Mkuu wa Wizara.

Akifafanua  alisema  Kamisheni ya Kazi na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) pia ni Mamlaka zinazojitegemea pamoja na kuwa zipo chini ya Wizara hiyo.

Alisema kwamba suala la Afisa wa Kamisheni ya Kazi kukamatwa kwa tuhuma za rushwa amewahi kusikia kupitia mitandao ya jamii lakini mpaka sasa hakuna barua yoyote kutoka ZAECA ya kuwataarifu kuhusu tukio hilo.

Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mussa Haji  alisema anakumbuka kutokea kwa kesi hiyo lakini aliwataka Waandishi wa Habari kumuona Kamishina wa Kazi kutokana na jambo hilo kuwa chini ya Idara yake.

“Kesi hii naikumbuka lakini muoneni Kamishina wa Kazi kwa ufafanuzi zaidi yeye ndio muhusika.”alisema  Mussa ambaye ni Mkurugenzi wa zamani wa  Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA)  kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na rais mwaka huu.

Kiongozi Mwanadamizi wa Kamisheni ya Kazi  Khamis Omar alikamatwa na ZAECA kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni moja kama shariti la kutoa kibali cha kazi kwa raia wa kigeni mwaka 2020.

Lakini Afisa uhusiano wa ZAECA  Yussuf Juma aliwambia Waandishi wa Habari kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa Umma mfanyakazi anapokabiliwa na kesi ya jinai kama ya rushwa na ufisadi anapaswa kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi kufanyika hadi kesi hitakapomalizika.

Katika mkutano wake na Wafanyakzi wa Mamlaka ya kuzuia rushwa na Uhujumu Uchumi hivikaribuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK Hussen Ali Mwinyi alisema serikali ya awamu ya nane itachukua hatua ya kumsimamisha kiongozi au mtendaji kama hatakabiliwa na tuhuma ya rushwa au ufisadi ili kupisha uchunguzi kufanyika.

Mkasa wa Kiongozi huyo mwanadamizi kuendelea na kazi kama kawaida umeibua mjadala mkubwa Zanzibar  kutokana na kuwepo kwa Vigogo mbali mbali waliosimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ubadhirifu akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Sabra Issa Machano Issa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.