Habari za Punde

Wananchi wa Mkata Waomba Kuboreshewa Miundombini

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.

WANANCHI wa kata ya Mkata wilayani Handeni wameiomba serikali kuboresha baadhi ya naeneo yenye upungufu wa kero ya maji ili wapate yakiwa safi na salama kwa muda wote kutokana na kero hiyo kupungua kwa kwa kiasi katika baadhi ya maeneo.

Wananchi hao walisema hayo juzi kwenye ziara ya mbunge wa Handeni vijijini John Sallu ya kukagua vyanzo vya maji katika eneo la Manga na Mkata jana, ambapo walisema kwasasa wakazi wa Mkata wanapata maji kwa bei nafuu baada ya maboresho ya miundombinu ya maji na kujengwa vituo zaidi ya 20 vya kuchotea maji kwenye maeneo mablimbali ya mji huo.

Akiongelea hilo mkazi mmoja Mwajabu Ayubu alisema kuwa awali katika mji huo mdogo ambao kwasasa ndio makao makuu ya wilaya, hawakuweza kupata maji safi kama hufahamiki vizuri kwa wauzaji kwani wengi walikuwa wakiuza kwa oda kutokana na umuhimu wa huduma hiyo.

"Mkata miaka ya nyuma tulikuwa tunanunua dumu moja la lita 20 kwa sh 1000 na muda mwingine hata kwa bei hiyo unaweza ukakosa maji, ila leo tunapata maji muda wowote kwa shilingi 50 bombani baada ya kuboreshewa bwawa la Mkata na kutengenezewa vituo zaidi ya 20 vya kuchota maji kwenye maeneo yetu", alisema Mwajabu.

Licha ya mafanikio hayo Pius Benedictor mkazi wa eneo hilo alishauri kuongezwa vituo vya kuchotea maji kwa maeneo ya pembezoni, kwani kuna baadhi ya maeneo bado hawajafikiwa na huduma hiyo kwa ukaribu zaidi.

"Tusiposhukuru kwa hili la maji tutakuwa wanafiki Mkata kwasasa madumu barabarani hakuna tena la msingi waongeze vituo pia kusafisha maji yatoke masafi kwa kuwa kuna muda yanatoka machafu sana hapo tutasahau kabisa suala la shida la maji", alisema Pius.

Mbunge Handeni vijijini John Sallu alisema katika kuboresha huduma za maji kuna ujenzi wa tanki jipya la maji Mkata pia kuchimbwa upya bwawa la maji la Manga ambalo lilivunjika tuta lake 2017 ili nalo liweze kutumika na kuongeza kupatikana maji.

Alisema wananchi zaidi ya 15,000 wa Manga na Mkata watanuifaika na miradi hiyo mipya, ambapo kwa Mkata mradi utakamilika mwezi April mwaka huu na utaongeza ujazo wa maji wa sasa na kupunguza kero ya maji iliyokuwepo.

Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira (RUWASA) wilaya ya Handeni Hossea Mwingizi alisema wanajenga tanki la maji la ujazo wa lita 5000 na lengo ni kuhakikisha wananchi ambao hawapati huduma za maji wanafikiwa na kupata maji muda wote ambapo mradi utakamilika April mwaka huu.

Aidha Mwingizi aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2021 mpaka 2022 wameweka bajeti ya kulijenga upya bwawa la Manga ambapo usanifu utaanza mwezi Machi mwaka huu.

Mkata ni moja ya mji mdogo katika wilaya ya Handeni ambao ulikuwa na shida ya maji kwa muda mrefu,ila kwasasa baada ya kuboreshewa bwawa la Mkata makali ya shida hiyo yamepungua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.