Habari za Punde

Zoezi la Urejeshaji wa Fomu za Uchaguzi Mdogo Jimbo la Pandani Pemba na Wadi ya Kinuni Unguja.

Na. JaalaMakame Haji- ZEC

Zoezi la Uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi wa Wagombea wa Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Pandani na Wadi ya Kinuni ambao utafanyika tarehe 28 Machi, 2021 limekamilika ambapo jumla ya Wagombea sita wamejitokeza kwa Uchaguzi wa Wadi ya Kinuni na Wagombea kumi Jimbo la Pandani.

Akizungumza wakati wa urejeshaji wa fomu hizo msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Pangawe Ndg.Suluhu Ali Rashid alisema hatua inayofuata ni kufanya uteuzi wa Wagombea hao ili kufanya Kampeni katika Maeneo waliyoomba kuteuliwa mara baada ya kupewa uthibitisho wa uteuzi.

Bw.Suluhu aliwataja waliochukua na kurejesha fomu Wadi ya Kinuni kuwa ni Bi Salama Rajab Masinga kupitia CCM, Ndugu.Kassim Ali Abdalla wa CUF, Ndugu. Hamad Hassan Hamad ACT Wazalendo, Ndugu. Bakar Muhammed Abeid wa Chama cha Demokrasia, Ndugu.Maulid Suleiman Fadhil wa Chama cha Demokrasia Makini na Ndugu. Zamir Ali Mabrouk kutoka Chama cha UPDP.

Naye Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Pandani Khamis Abdalla Hassan aliwataja waliochukua fomu na kurejesha kuwa ni Ndugu.Mohammed Juma Ali wa CCM, Ndugu. Said Hamad Ali wa Demokrasia Makini, Prof. Omar Fakih Hamad ACT Wazalendo, Ndugu.Massoud Ali Said Chama cha Wananchi CUF, na Ndugu. Ali Jabir Khamis wa Chama cha ADC.

Wengine ni Ndugu.Khamis Faki Mgau Chama cha NRA, Bi Asha Fumu Ali Cham cha UPDP, Ndugu. Ali Hamad Omar wa Chama cha ADA TADEA na Ndugu. Mohammed Sharif Khamis kutoka Chama cha NLD.

Ndugu.Khamis Hassan aliwataka wagombea watakaoteuliwa mara baada ya kuwekwa wazi kwa fomu za uteuzi kwa saa ishirini na nne kuendelea kudumisha Amani ya nchi katika kampeni za uchaguzi hadi kumalizika kwa Uchaguzi huo.

Ndugu Khamis alieleza kuwa, Kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Pandani na Wadi ya Kinuni zinatarajiwa kuanza tarehe 13 mpaka 26 Machi, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.