Habari za Punde

India Yakabidhi Msaada wa Dawa Kwa Zanzibar Zenye Thamani ya Shilingi Milioni 268.

Balozi mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa India aliepo  Zanzibar Mhe.Bhagwant Singh (kushoto) akimkabidhi Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazurui moja ya boksi la dawa zilizotolewa msaada na nchi yake.katika hafla iliyofanyika Bohari Kuu dawa Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawa wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Omar Dadi Shajak akitoa hotuba ya makaribisho wakati Balozi mdogo wa India aliepo Zanzibar alipokabidhi msaada wa dawa katika Bohari Kuu ya dawa Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
Baadhi ya Wafanyakazi wa Bohari Kuu ya dawa na Wageni waalikwa wakishuhudi kukabidhiwa msaada wa dawa kutoka India katika hafla iliyofanyika Ofisini kwao Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar                 12.04.2021

Serikali ya India imeikabidhi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar msaada wa dawa za kutibu maradhi tofauti, ikiwemo Kensa, zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 268 za Tanziania.


Balozi mdogo wa India aliepo Zanzibar Bhagwant Singh alimkabidhi Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui shehena ya dawa hizo katika hafla iliyofanyika Bohari Kuu ya Dawa Marughubi.


Balozi Bhagwant amesema mashirikiano na mahusiano ya karibu kati ya India na Tanzania, ikiwemo Zanzibar, ulianza miaka mingi iliyopita na nchi hiyo imekuwa ikisaidia masuala mbali mbali ya Maendeleo ikiwemo Elimu, Afya, Kilimo na Ustawi wa Wananchi.


Ameahidi kuwa India itaendelea kuimarisha mashirikiano yaliopo kati yake na Tanzania kwa kutumia uwezo wa rasilimali walizonazo katika kusaidia kuimarisha uchumi wake.


Akipokea msaada huo, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui aliishukuru Serikali ya India kwa msaada huo mkubwa wa dawa ambao alisema utapunguza kwa asilimia tatu ya bajeti ya kuagiza dawa nje.


Waziri Mazrui alimueleza Balozi mdogo wa India kuwa sehemu ya dawa hizo tayari zimepelekwa kisiwani Pemba kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa kisiwa hicho.


Alisema Zanzibar kupatiwa msaada huo hasa dawa za kutibu maradhi ya Kensa, ambazo ni ghali sana kuzinunua, utasaidia sana wananchi kufuata matibabu Hospitali za maradhi hayo Tanzania Bara na Hospitali za nje.


Alieleza kuwa Wizara yake imeandaa utaratibu mzuri wa kielektroniki unaohakikisha kuwa usambazaji wa dawa kutoka Bohari Kuu hadi kufika Hospitali na vituo vya afya unakuwa na ufanisi na hazipotei njiani.


Wakati huo huo Waziri Mazrui amemuomba Balozi mdogo wa India kuwashawishi wawekezaji wa nchi yake kuja kuwekeza Viwanda vya Dawa Zanzibar ili kuondosha upungufu wa dawa nchini.


Aliahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iko tayari kutoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika kwa muwekezaji atakaeonyesha azma ya kuwekeza kiwanda cha dawa ili kuhakikisha lengo lake linafanikiwa.


Alisema Zanzibar kuwa na kiwanda cha dawa ni jambo la msingi na alikumbusha kuwa miaka ya nyuma kilikuwepo lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza kiwanda hicho kilisimamisha uzalishaji hadi hivi sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.