Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Amuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi Ufunguzi wa Masjid Riadh Salhin Mgogono Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu baada ya kufungua Masjid Riadh Salhin kwa niaba ya Rais wa Zanzibar.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wakifuatilia Hostuba ya Ijumaa mara baada ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah kufungua Masjid Rioadh Mgogoni Pemba.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al Hajj Dr. Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha Wazazi na Walezi Nchini wajikite zaidi katika kuwafinyanga Vijana wao kwa ajili ya kuwandaa kushika nyadhifa za Uongozi ili kujihakikishia kuwa na Taifa jema lililoshiba Maadili.

Al –Hajj Dr. Hussein Ali Mwinyi alitoa kauli hiyo katika salamu zilizotolewa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullahwakati wa ufunguzi rasmi wa Masjid Riadh Salhin katika Kijiji cha Mgogoni Chake Chake Pemba.

Alisema masuala ya maadili sambamba na miongozo ya  Dini inapaswa kuhuishwa, na hayo hayataweza kupatikana kama hakukuwa na maandalizi mazuri na ya muda mrefu katika kuwaonyesha Vijana njia sahihi na muwafaka ya kujuwa wajibu wao.

Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Umoja na Mshikamano katika kufikia mafanikio hayo lazima udumishwe hasa katika Majengo ya Misikiti kwa vile ndio mahala pekee kwa Wana Kijiji au Mtaa kuzungumza masuala yao ya Kimaisha iwe ya Kidini, Kijamii na hata ya Kiuchumi.

“ Wananchi waendelee kushirikiana zaidi hasa kipindi hichi ambacho Taifa na Waumini wa Dini ya Kiislamu wanakaribia kuingia katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan”. Alisema Al – Hajj Dr. Hussein Mwinyi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameelezea kuridhika kwake na moyo wa Umoja unaoendelea kushamiri miongoni mwa Wananchi Nchini, uthibitisho unaowapa Wana Jamii kuelezea changamoto zao zainazowakabili bila ya kujali Itikadi, Tofauti zao za Kidini na maeneo wanayotoka.

Alibainisha wazi kwamba msimamo na mfumo wa Wananchi uliopo hivi sasa unaendelea kutia moyo na ari Viongozi Wakuu wa Serikali pamoja na wale Waandamizi wa Taasisi za Umma wanaowajibika kuwahudumia Wananchi walio wengi.

Aliwataka Wananchi na Waumini wa Dini na Madhehebu mbali mbali Nchini waendelee kuvuta subra ya kutanzuliwa kwa changamoto zinazowakabili hasa za huduma za Maji safi na salama na Umeme kwa vile tayari zinaeleweka na Serikali Kuu na wakati huu iko katika mchakato wa kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Al Hajj Dr. Hussein Ali Mwinyi aliwaahidi na kuwahakikishia Wananchi kwamba katika kipindi kifupi kijacho yanatarajiwa kutokea mabadiliko makubwa katika ustawi wa Jamii hasa huduma za Maji kwani haipendezi kuona Muumini anaingia Msikitini kutaka kufanya Ibada lakini matokeo yake anashindwa kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa huduma za Maji.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewapongeza Wananchi wa Kijiji cha Mgogoni kwa kuendeleza Umoja wao na kuwahakikishia kwamba Bara  bara  ya Madungu inayowasumbua wakati wanapohitaji huduma za mawasiliano ya usafiri itazingatiwa kwa hatua ya matengenezo.

Akisoma Risala ya Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi wa Kijiji cha Mgogoni, Mmoja wa Viongozi wa Kijiji hicho Sheikh Ali Juma alisema wazo la ujenzi wa Jengo hilo la Msikiti limekuja mnamo Tarehe 17Septemba 2018 kutokana na ongezeko la Idadi ya Watu.

Alisema Msikiti huo uliopata msukumo wa Wafadhili kwa asilimia 80% na wenyeji asilimia 20% umeleta faraja sio tu kwa Ibada bali pia utahusisha na shughuli za Kijamii ikiwemo kusimamia Maadili kutokana na kuporomoka kwa Silka kwa baadhi ya Vijana.

Akitoa chakula cha moyo kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu walioshiriki Ibada ya Sala ya Ijumaa na ufunguzi wa Msikiti huo, Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alitanabahisha kwamba Kila Mwanajamii anapaswa kuheshimua mamlaka zilizopewa jukumu la kuwasimamia katika masuala yao.

Sheikh Khalid alitolea Mfano Afisi ya Mufti Mkuu ndio yenye mamlaka na iliyopewa jukumu la kutangazia Mwezi unapoandama na kuwatanabahisha Baadhi ya Watu wenye tabia ya kutoa taarifa misikitini na wengine kutumia matangazo ya Redio wanapaswa kuelewa kwamba kufanya hivyo  ni kujichukulia  dhamana kinyume na taratibu.

Alisema Muumini anayeuona Mwezi na akaamua kutotoa Taarifa kwa mamlaka husika ambayo ni Afisi ya Mufti Mkuu na afunge mwenyewe bila ya kuwatangazia wenzake.

Mapema akitoa Hutba ya Ijumaa baada ya uzinduzi wa Msikiti huo Mwanazuoni Sheikh Said Abdullah Nassor alisema Msikiti ni Afisi na Kituo maalum kwa Waumini kusimamisha Ibada inayopambatana na Mirathi ya Elimu, dhikri pamoja na kukumbushana wajibu wa kuikimbilia haki na kuacha batil.

Sheikh Said Abdulla alisema Majengo ya Misikiti kwa mujibu wa taratibu za Dini halkadhalika yanapaswa kudumisha shughuli za Kijamii na Kiuchumi  ambazo wakati mwengine husaidia kuratibu mwenendo wa kuwahudumia Watoto Yatima, Wajane na Watu wenye Mahitaji Maalum {Walemavu}.

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu alibainisha kwamba ni vyema kwa Jamii isiridhie kuona Watoto Yatima, Wajane na hata Walemavu wanaendelea kuomba Mitaani wakati Majengo ya Msikiti  ndio yenye wajibu na haki ya kushughulikia matatizo yao na kinachohitajika ni moyo wa upendo na imani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.