Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Azungumza na Wahadhari wa Chuo Kikuu Huria Tanzania Ikulu Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania ukiongozwa na Makamo Mkuu wa Chuo Prof.Elifas Tozo Bisanda (kulia kwa Rais) na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Simai Mohammed Said na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wahadhari wa Chuo Kikuu Huria Tanzania ukiongozwa na Makamo Mkuu wa Chuo Prof.Elifas Tozo Bisanda, walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu

Rais Dk. Mwinyi alikutana na uongozi wa Chuo Kikuu Huria chini ya Makamo Mkuu wake Profesa Elifas Tozo Bisanda ambapo katika mazungumzo yao uongozi huo uliumpongeza Dk. Mwinyi pamoja na chama chake cha CCM kwa ushindi uliopata katika uchaguzi mkuu uliopita.

Aidha, uongozi huo ulimpa pole Rais Dk. Mwinyi kwa misiba iliyotokea ya Kitaifa ukiwemo msiba wa Hayati Dk. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

Pia, uongozi huo ulitumia fursa hiyo kumuomba Rais Dk. Mwinyi kuwapelekea salamu zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kupokea vyema majukumu ya Urais sambamba na kuendeleza amani na utulivu nchini.

Uongozi huo ulimueleza Rais Dk. Mwinyi mafanikio makubwa yaliopatikana tokea kuanzishwa  kwa chuo hicho hapa Zanzibar mnamo mwaka 1994 ambapo hadi mwaka wa masomo uliomalizika Juni mwaka uliopita wameweza kudahili wanafunzi wapatao 4,534 hapa Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Profesa Basinda alieleza kwamba kati ya wanafunzi hao waliohitimu ni 1,855 sawa na asilimia 41 ya waliodahiliwa ambapo hayo ni mafanikio makubwa kwa Zanzibar kwani katika vyuo huria wanafunzi wanaofanikiwa kuhitimu huwa hawazidi asilimia 25.

Nae Rais Dk. Mwinyi kwa upande wake alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi huo pamoja na Chuo hicho kwa juhudi zake kubwa unazozichukuwa katika kutoa elimu kwa wanafunzi wa Zanzibar ambao wamekwua wakifanya vizuri.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na chuo hicho ili kizidi kupata mafanikio.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.