Habari za Punde

Serikali na Mpango wa Kudhibiti Uchafuzi wa Bahari

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

SERIKALI kupitia Shirika la Uwakala wa meli nchini (Tasac) iliona ipo haja ya kuja na mpango wa kupambana na uchafuzi wa mazingira baharini na kwenye maziwa kutokana kumwagika kwa mafuta ili kuepuka madhara kutoka nchi jirani ambayo yanatokana na uchafuzi huo.

Akifungua warsha ya pili ya wadau wa mpango wa Taifa wa kujiandaa na kupambana na umwagikaji wa mafuta kwenye bahari na maziwa jana, mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela alisema serikali kwa kuona umuhimu wa kukuza na kulinda uchumi wa nchi kupitia uchumi wa bluu, imeandaa mpango huo ili kudhibiti machafuko yanayoweza kutokea nchi jirani na kuleta madhara nchini.

"Niipongeze sana Tasac na Serikali kwa kuliona hili kwa kuja na mpango huu ambao utatufanya tuwe imara katika kukabiliana na uchafuzi utakaojitokeza, na niseme kwamba mpango huu umekuja muda muafaka kwakuwa tumeona ina dhamira ya dhati ya kutanua huduma zetu kwa kujenga na kutanua bandari yetu ili kufanya shuhuli za usafirishaji wa mafuta" alisema.

"Kwakuwa sisi mkoa wa Tanga tumepakana na nchi zenye bahari na maziwa, kama kwa mfano mafuta yamemwagika bahari ya Mombasa yanaweza yakaja mpaka kwenye bahari ya upande wetu, vile vile ikitokea kwa upande wa Mozamboque madhara yale yanaweza kuja upande wa kwetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania" aliongeza Shigela.

Shigela alisema kutokana na matumizi mengi ya binadamu katika bahari na maziwa uwezekano wa uchafuzi ni mkubwa hivyo kila mdau aliyeshiriki warsha hiyo kwa nafasi yake anapaswa kuelewa na kujipanga kufanyia kazi mpango huo wenye lengo la kukuza uchumi wa Taifa.

Naye Mkurugenzi Idara ya udhibiti uchumi Tasac Nahson Sigalla alisema kuundwa kwa shirika hilo ni hatua ya kisera ya serikali iliyolenga kuinua mchango wa usafiri kwa njia ya maji katika ukuaji wa uchumi wa Taifa ambayo pia ni mdhibiti mahsusi katika huduma za usafiri kwa njia ya maji na inatarajiwa kuimarisha na kutia mkazo katika udhibiti huo kama ilivyo kwa nchi nyingine zenye bahari.

Sigalla pia alisema Tasac ina majukumu ya kusimamia ulinzi na usalama na kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na shuhuli za usafiri majini ambapo katika jukumu hilo husimamia utekelezaji wa mikataba ya Kimataifa ya Shirika la Bahari Duniani iliyoridhiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Hivyo basi, kutokana na majukumu ya Tasac, ni kazi ya msingi shirika kusimamia na kusuia uchafuzi wa mazingira unaotokana na umwagikaji wa mafuta kutoka kwenye vyombo vya usafiri majini, kwa sababu hiyo, shirika kwa kishirikiana na Taasisi nyingine za serikali liliandaa mpango huu mwaka 2016 ambao ulifanyiwa mabadiliko mwaka 2020 na kuridhiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi" alisema Sigalla.

"Kama nchi, tulibaini umuhimu wa mpango na kuuandaa, aidha mpango huu unakidhi matakwa ya mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania tumeiridhia, napenda nitoe taarifa kuwa, leo itakuwa mara ya pili kufanya warsha na mazoezi katika mkoa huu wa Tanga, warsha ya kwanza tulifanya Septemba 10 hadi 12 mwaka 2019" aliongeza.

Sigalla alifafanua kwamba wakati wa warsha ya kwanza walikubaliana kuupatia mkoa wa Tanga vifaa vya kupambana na mafuta yaliyomwagika baharini huku wakishauriana baada ya zoezi hilo kukamilika zoezi la pili lifanyike mkoani hapa ili kuzidi kuwajengea wadau uwezo wa kpambana na hali hiyo pindi itakapojitokeza.

"Tuliyafanya hayo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kazi ya uhudumiaji mafuta kwa kuzingatia ujio wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda kuja Chongoleani mkoani Tanga, ahadi ya kukabidhi vifaa mkoani hapa imetekelezwa  mei 12 mwaka jana, sasa tumekuja kutekeleza ahadi ya kufanya warsha ya pili" alifafanua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.