Habari za Punde

Wanahabari Waaswa Kujadili Hali ya Uchumi Kwa Wanahabari.

 
Na: Habari MAELEZO.                                                                                                                      

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amewaasa waandishi wa habari nchini kujadili juu ya hali uchumi ya wanahabari katika vyombo                mbalimbali vya habari      hapa nchini.                                                                                                     

Akiongea katika kongamano la majadiliano la Wadau wa Habari kwa Maendeleo ya Nchi kuelekea kilele cha Siku Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Mei 3, itakayofanyika Jijini Arusha Dkt. Abbasi amesema wakati umefika kwa waandishi wa habari kutafakari na kujadili uwezo wa kiuchumi kwa vyombo vya habari ambavyo vingi huanzishwa kwa malengo binafsi.

"Uchumi wa wanahabari una hali mbaya, mishahara midogo na mara nyingine hupokea mshahara huo baada ya miezi sita, hawana bima wala pensheni; ni namna gani tutasaidia vyombo vya habari kiuchumi"

Aidha amesema Serikali ipo tayari kupokea mapendekezo na kuyafanyia kazi maoni, ushauri kutoka kwa wadau kwa lengo la kutafuta ufumbuzi

Amewataka wanahabari kujadiliana mfumo mzuri wa uendeshaji wa vyombo vya habari, na kwamba majadiliano hayo yatoe mawazo au mapendekezo ili Serikali iweze kuyafanyia kazi.

Ameongeza kwamba Serikali ipo tayari kupokea na kufanya mabadiliko ya kisera au kisheria iwapo patakuwa na hoja ya msingi kwa manufaa ya Taifa.

Mmoja wa Waandishi wa Habari, ( jina limehifadhiwa) amesema hali ya waandishi wa habari ni mbaya kiuchumi.

" Mimi nina miaka mitano (5) sasa nahesabika kama correspondent na sio muajiriwa hivyo sina mkataba wala mshahara, nalipwa kwa stories. Pia ninapotaka kwenda kutafuta stories, ofisi inanituma lakini hakuna nauli, nategemea kupiga simu kwa mwenzangu aliyepo eneo la tukio na matokeo waanahabari wanataka kwenda kwenye stori wanazotoa bahasha ili kukidhi mahitaji yetu kiuchumi".

Akichangia hoja ya uchumi kwa vyombo vya habari, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Deogratius Balile amesema vyombo vya habari vinaweza kuwa na uchumi endelevu iwapo vitashirikishwa katika mipango ya maendeleo ya Taifa .

"Mathalan, kushiriki katika kufahamisha umma malengo na mpango wa maendeleo wa taifa na pia nafasi yake katika kutangaza mpango huo". Amesema Balile.

Dkt. Abbasi amewashukuru Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali na Wadau mbalimbali wa habari kwa kuandaa kongamano hilo na akashauri UNESCO kuandaa makangomano mengine hata mata mbili au nne kwa mwaka kufanyika zaidi ya mara mbili kwa mwaka ili kujenga uelewa katika tasnia ya habari.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.