Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdalla Akutana na Kuzungumza na Ujumbe wa Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumisi wa Umma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akizungumza  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora wa SMT Mh. Mohamed Mchengerwa na Viongozi Waandamizi wa Mfuko wa Tasaf na  Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania {Mkurabita} waliopo Zanzibar kwa ziara ya Kiserikali.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kati kati akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora wa SMT Mh. Mohamed na Tmu yake mara baada ya mazungumzo yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdull kati kati akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu wa Ofisi yake Nd. Thabit Idarous Faina Kulia na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Nd. Ladilaus Mwamanga Kushoto.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema suala la malalamiko ya mgawanyo wa Ajira kwa Zanzibar ya asilimia 21% katika Taasisi za Muungano litaondoka na kubakia kuwa Historia endapo waliopewa dhamana ya kulisimamia watalitekeleza kwa tatumia ueledi wao.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo Ofisini kwake Vuga wakati akibadilishana mawazo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa SMT Mh. Mohamed Mchengerwa aliyembatana na Viongozi Waandamizi wa Mfuko wa Tasaf na  Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania {Mkurabita} waliopo Zanzibar kwa ziara ya Kiserikali.

Alisema suala hilo la mgawanyo wa Ajira kwa Zanzibar ya asilimia 21% katika Taasisi za Muungano kwa vile halimo katika kero za Muungano linapaswa  kusimamiwa vyema katika Utekelezaji wake ili yale malalamiko yanayotolewa na na baadhi ya Wananchi yafikie ukomo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwashauri Wataalamu na Watendaji  wote wanaosimamia masuala hayo watumie Taaluma zao katika kuwaelimisha Wananchi mbinu na namna watakavyotumia fursa zinazotokea katika ajira  kupitia mfumo wa Teknolojia na Habari na Mawasiliano.

“ Nafarajika kuona suala hili tayari limeanza kufanyiwa kazi kwa vile hata ndani ya Vikao vya Baraza la Wawakilishi limekuwa likiulizwa na Wajumbe wa Baraza hilo. Inaonekana hata wewe Mwenyewe binafsi Mh. Waziri umelisikia au kupata taarifa zake”. Alifafanua Mh. Hemed Suleiman.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mohamed Mchengerwa na Wataalamu wake kwa jitihada kubwa wanazoendelea kuzichukuwa katika kuona suala la ajira za Wazanzibari katika Taasisi za SMT linazingatiwa katika utaratibu wake uliomo katika Katiba na Sheria.

Akizungumzia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Mheshimiwa Hemed Suleiman alionya kwamba Mtu au Kiongozi atakayeamua kugusa Fedha zilizotengwa na Tasaf kwa ajili ya Kaya Maskini kinyume na utaratibu uliowekwa atalazimika kuwajibishwa mara moja.

Alisema Fedha hizo zinazotolewa na Serikali lazima ziheshimiwe kwa vile zimetengwa na kulenga maalum ili ziwafikie Watanzania walio wengi katika maeneo mbali mbali hasa Vijijini ambao baadhi yao bado wanakabiliwa na kipato Duni.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba Wananchi wa kipato cha chini wanahitaji   kupata msukumo utakaowaonyesha njia ya kujikwamua kiuchumi kupitia Miradi ya Maendeleo ya Kijama kama Tasaf iliyobuniwa kuwakomboa Wana Jamii katika maeneo yote Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza wazi kwamba kupitia Miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} sifa ya Zanzibar kufanya vizuri ndani ya mpango huo lazima ibaki na kuendelea katika Awamu zote zinazofuata za Mfuko huo.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mh. Mohamed Mchengerwa alisema Yeye, Viongozi walio chini yake kupitia Wataalam walio Taasisi zilizo Ofisi hiyo wameandaa utaratibu utakaotoa fursa ya kuwasajili Wanafunzi wote wanaomaliza mafuzo yao ya  Sekondai na vyuo hapa Zanzibar.

Alisema hatua hiyo muhimu aliyoahidi kuifanyia Kazi yeye na Wataalamu wake  itarahisisha Kuwapata Vijana wa Zanzibar pale zinapotokea fursa za Ajira kwa Taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano  kwa mujibu wa Vigezo, sifa na Elimu zao zitakazokwenda sambamba na Ajira husika.

Waziri Mchengerwa alibainisha kwamba suala la Mafunzo kwa Watumishi Umma litazingatiwa kwa kina kupitia Mfumo wa Ushirikishwaji wa pamoja baina ya Vyuo vya Utumishi wa Umma vya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa upande wao Viongozi Waandamizi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf}, Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania {Mkurabita}pamoja na Sekreterieti ya Utumishi wa Umma na Ajira walisema lengo la kuanzishwa kwa Taasisi wanazozisimiamia ni kusaidia kuondosha Umaskini kwa Watanzania walio wengi Nchini.

Viongozi hao Waandamizi wa Taasisi hizo walisema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania {Mkurabita} umeleta mafanikio makubwa kwa Wananchi wa Zanzibar.

Walisema katika masuala ya Ajira mfumo unaoandaliwa hivi sasa wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano utamuwezesha Mwananchi hasa Kijana kuwa na uwezo wa kuomba nafasi ya Ajira kwa kutumia Simu yake ya Mkononi itakayomuwezesha kupata uelewa kwa lile atakalolohitaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora wa SMT Mh. Mohamed Mchengerwa na Timu yake ya Viongozi Waandamizi wa Taasisi za Tasaf, Ajira na Mkurabita wapo Zanzibar kwa ziara maalum ya Kiserikali kukagua Maendeleo ya Miradi ya Taasisi hizo inayotekelezwa Visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.