Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kutoa Ushirikiano Utekelezaji wa Mradi Kuwarejesha Skuli Watoto Waliofikia Umri Kuwawezesha Kupata Elimu.

Makamu wa Pili wa Rais akihoutubia katika uzinduzi wa mradi wa kuwarejesha skuli watoto wenye umri wa elimu ya msingi katika hafla ambayo amemuakilisha Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Na.Kassim ABDI.OMPR. Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kutoa ushirikiano juu ya utekelezaji wa mradi wa kuwarejesha skuli  watoto  waliofikia umri ili kuwawezesha kupata elimu bora itakayosaidia kuwajengea mustkbali wa maisha yao ya baadae.

Rais Dk. Mwinyi alieleza hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika uzinduzi wa mradi wa kuwarejesha skuli watoto wenye umri wa elimu ya msingi ambao hawapo skuli hafla ambayo imefanyika katika kiwanja cha Skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeamua kufuta  michango ya kugharamia upatikanaji wa elimu kwa wazee na walezi ili kutoa fursa kwa watoto waliofika umri wa kuanza masomo waweze kupelekwa skuli kwa lengo la kupata haki yao ya msingi.

Makamu wa Pili wa Rais alifafanua kuwa miongoni mwa shabaha ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 1964 ni kutoa elimu bure kwa wazanzibari jambo ambalo ni haki ya msingi na kutekeleza azma hiyo itasaidia kujenga taifa la wasomi linalojitegemea kwa kuzalisha watalamu wake  na kuacha kutegemea wataalamu kutoka mataifa mengine pamoja na kufuta ujinga.

Alieleza kuwa, Serikali imeamua kutilia mkazo suala la elimu katika kuhakikisha  wananchi wake wanapata elimu bora kwa kutanua fursa za kielimu na kuimarisha miundombinu.

 “Serikali ya Awamu ya Nane kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025 imeweka shabaha zinazoendeleza sera ya elimu kwa wote” Alieleza Makamu wa Pili wa Rais

Mhe. Hemed alisema takwimu zinaonesha kuwa watoto wanaopatiwa elimu katika ngazi mbali mbali imekuwa ikiongezeka ambapo jumla ya wanafunzi laki tatu thalathini na moja elfu mia nne na ishirini na tano (332,425) wameandikishwa katika ngazi ya elimu ya msingi kwa mwaka 2021 ikilinganishwa na wanafunzi  laki mbili hamsini na sita elfu  arubaini na nane (256,048) kwa mwaka 2017, ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia ishirini na tisa nukta nne ( 29.4%).

“Serikali inakabiliwa na changamoto ya kuwa na watoto thalathini na tano elfu mia saba na thalathini na mbili  ambao hawajawahi kuandikishwa skuli ama waliandikishwa na wakatoroka, idadi hii ni kubwa na inailazimu Serikali kuwa na mkakati wa kuwarejesha watoto hao skuli”. Alisema Mhe. Hemed

Akizungunzia suala la watoto kurudi skuli  Makamu wa Pili wa Rais wa alieleza ili kuweza kuitatua changamoto hiyo kunahitajika mashirkiano ya karibu baina ya wadau mbali mbali wakishirikiana na wazazi.

Aidha, Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuishukuru Jumuiya inayoongozwa na Sayyidat Moza Mke wa Mfalme wa Qatar ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la kuhudimia Watoto (UNISEF) kwa kuamua kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwapatia elimu watoto wakizanzibari bila ya ubaguzi.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Hemed aliwaomba wananchi wa Zanzibar kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo hasa wazazi ambao ni walengwa hawana budi kutumia vizuri fursa ya mradi huo ili kuwawezesha watoto wao kupata elimu.

“Viongozi wa serikali kupitia ngazi  zote kuanzia Mkoa mkoa hadi Shehia lazima mushirikiane na viongozi wa majimbo kwa kuwatambua watoto hao” Alisisitiza Mhe. Hemed

Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Simai Mohamed Said alisema kuwa kupitia program hii iliozinduliwa rasmi Wizara imejipanga kutumia vifaa vya kisasa katika kukuza elimu kwa wanafunzi.

Mhe. Simai aliwataka wazazi na walezi kujenga utaratibu na utamaduni wa kuwanunulia watoto wao vifaa vya kujifunzia ikiwemo vitabu ili vieweze kuwasaidia katika kupata elimu.

“Niseme tu Natoa ahadi katika mikioa hii mitano, Mkoa utakaofanya vizuri katika utekelezaji wa Program hii utapata zawadi” Alisema Mhe. Simai

Akisoma taarifa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali Ali Khamis alisema wastani wa wanafunzi kwa kila darasa wanafunzo 80 kwa sasa ambapo bado kuna changamoto ya baadhi ya watoto hawajaandikiswa katika mfumo rasmi

Alieleza kwamba, Programu hii inawalenga pia watoto wenye ulemavu pamoja na wasichana kupitia skuli zote za Unguja na Pemba ambapo utahusisha wilaya zote kumi na moja (11) katika skuli mia moja (100).

Pia Katibu Mkuu Huyo alisema Programmu itawahusisha watoto waliopo vijijini ambao familia zao zinakabiliwa na hali duni ya kimaisha huku akiutaja mkoa wa Kaskazini Unguja ndio unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto walio nje ya mfumo wa kupata elimu ya Msingi.         

Akiwasilisha salamu za shirika la kimataifa linaloshuhulikia watoto duniani (UNICEF) Bibi  Shalin Baluguma alisema shirika lao linafurahishwa sana na jitihada za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  inayoongozwa na Dk. Hussein mwinyi kwa kuhakikisha inajali sana utoaji wa huduma za jamii kwa wananchi wake ikiwemo elimu.

Alieleza kuwa, katika suala la kupambana na maradhi ya Covid-19 Shirika lao limeshuhudia jitihada za hali ya juu zinazochukuliwa na uongozi wa Wizara ya elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar katika kuwakinga wanafunzi dhidi ya ugonjwa huo unaoambukiza.

Wakati huo huo, Makamu wa Pili wa Rais amejumuika pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Uguja katika sala ya Ijumaa katika Masjid Tas-bihi  Kivunge.

Akiwasalimu waumini waliosali katika mskiti huo Makamu wa Pili wa Rais aliwasisitiza wazazi kuwasimamia watoto wao juu ya suala zima la elimu kwani takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Kaskazini una idadi kubwa ya watoto waliotoroka Skuli.


Waziri wa elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Mhe. Simai Mohamed Said akizungumza na hadhara iliohudhuria katika uzinduzi wa mradi wa kuwarejesha skuli watoto wenye umri wa elimu ya msingi katika kiwanja cha Skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi zawadi kwa watoto waliorudi skuli kupitia program maalum inayosimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika uzinduzi uliofanyika katika Skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akisalimiana na watoto waliohudhuria katika uzinduzi wa mradi wa kuwarejesha skuli watoto wenye umri wa elimu ya msingi katika kiwanja cha Skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Muwakilishi wa Shirika la kimataifa linalohudumia hudumia watoto duniani Bibi Shalin Baliguma akitoa salamu za Shirika hilo katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kuwarejesha skuli watoto wenye umri wa elimu ya msingi katika kiwanja cha Skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi zawadi kwa watoto waliorudi skuli kupitia program maalum inayosimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika uzinduzi uliofanyika katika Skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.