Habari za Punde

MAVUNDE: CHAGAMKIENI MIKOPO YA NYUMBA, VIWANJA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma                                                                                                     

MBUNGE wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde amewahamasisha watumishi wa Kituo cha afya Makole kuchangamkia fursa ya kununua nyumba na viwanja vya makazi, katika    mpango unaoendeshwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Benki ya Azania.                                                                                                                                           

Mhe. Mavunde alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dodoma alipokuwa akipokea vifaa tiba vilivyotolewa na PSSSF kwa Kituo cha afya Makole kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa umma iliyoadhimishwa kuanzia Juni 16 hadi 23, 2021.                              

“Ndugu wafanyakazi wa kituo cha Makole, nawahamasisha jitokezeni kutumia fursa hii ya kumiliki nyumba na viwanja kama walivyosema wenzetu wa PSSSF, kwa mpango huu wa kulipa kidogo kidogo, naamini kila anaweza kupata anachotaka, hivyo jitokezeni” alisisitiza Mhe. Mavunde.

PSSSF kwa kushirikiana na Benki ya Azania wana utaratibu wa kukopesha nyumba zilizojengwa na Mfuko na viwanja kwa Wanachama wake na Wananchi kwa ujumla kwa riba nafuu na masharti rafiki zaidi kwenye soko. Lengo la mpango huo ni kuwawezesha wanachama na wananchi kumiliki nyumba na viwanja kwa utaratibu wa kulipa kidogo kidogo kwa riba nafuu ya asilimia 10.Bei ya nyumba ni kati ya millioni 36 hadi 61 kutegemeana na ukubwa wa nyumba.

Nyumba zinazouzwa zipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Shinyanga, Tabora, Mtwara na Iringa. Viwanja vipo Ruvuma, Kagera, Tabora, Iringa, Katavi, Morogoro, Dar es Salaam, Rukwa, Lindi na Mtwara.

Akizungumzia ziara ya PSSSF katika kituo cha afya Makole, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema, “Kwa kuzingatia ujirani wetu huu, PSSSF imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa kituo hiki ikilenga kuboresha huduma zitolewazo, kwani kama mjuavyo nia ya serikali ni kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma bora za afya. Ili kuhakikisha tunaendeleza azma hiyo, katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu, tunachangia vifaa tiba katika kitengo cha kina Mama Wajawazito na kitengo cha Meno kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za tiba ya meno ikiwemo utengenezaji wa meno bandia”.

Kwa upande wa Mbunge wa Dodoma Mjini aliishukuru PSSSF kwa kuendelea kusaidia kituo hicho ambacho alisema kwa sasa kinatoa huduma kwa watu wengi zaidi wakiwemo watumishi wa PSSSF, na aliongoza, “Msaada huu utakwenda kuleta matokeo chanya kwa wananchi wote.Pia Mkurugenzi Mkuu, naomba mkifanye kituo hiki kiwe rafiki kwenu kwa kuendelea kutoa misaad mara kwa mara.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA Hosea Kashimba (kulia) akikabidhi vifaa tiba kwa Mbunge wa jimbo la Dodoma (mjini)., Mhe. Anthony Mavunde (katikati) na Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya cha Makole Bibi Tumaini Kapungu mwishoni mwa wiki iliyopita. PSSSF imetoa msada huo kwa Kituo hicho kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa umma iliyoadhimishwa kuanzia Juni 16 hadi 23, 2021.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, akizunumza kwenye hafla hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba (kulia), akimkabidhi sehemu ya vifaa tiba hivyo, Mbunge wa Dodoma (mjini) Mhe. Anthony Mavunde.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.