Habari za Punde

Shirika la Afya Duniani (WHO) kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar kuhakikisha wananchi wanapatiwa kinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza

Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya  Duniani DK Girman Andermichael  (kushoto) akitoa ufafanuzi wa chanjo ya Corona na kipindupindu kwa Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto Nassor Ahmed Mazrui (wa kwanza kulia) huko Ofisini kwake Mnazi mmoja Zanzibar.
Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto,Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akimsikiliza  Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani  Dr.Tigest Ketsela Mengestu (kushoto)aliyefika ofisini kwake kuzungumzia chanjo ya Corona na kipindupindu huko Ofisini kwake Mnazi mmoja Zanzibar.

Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto,Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Wizara ya afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto na Wawakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) huko Ofisini kwake Mnazi mmoja Zanzibar.

Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto,Mhe. Nassor Ahmed Mazru  wakisalimiana na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Dunian Ms. Jacqucline  Mahor  wakati wa kukabidhiana vifaa tiba  huko Ofisini kwake Mnazi mmoja Zanzibar.

 Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto,Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akimkabidhi kitabu cha historia ya Zanzibar  Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani MS. Jacqucline  Mahor huko Ofisini kwake Mnazi mmoja Zanzibar.

PICHA NA KHADIJA KHAMIS - IDARA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

Na Issa Mzee        Maelezo         3/06/2021.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeahidi  kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar katika kuhakikisha wananchi  wanapatiwa kinga dhidi ya maradhi mbalimbali ya kuambukiza ikiwemo corona na kipindupindu.

Ahadi hiyo imetolewa na  mwakilishi wa WHO nchini Tanzania Dr.Tigest Ketsela Mengestu wakati akizungumza na Waziri wa afya Zanzibar ofisi kwake Mnazi Mmoja na kufanya mazungumzo na Waziri huyo kuhusu mikakati mbalimbali inayoweza kufanyika ili kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanakuwa salama.

Dr Ketsela alimwambia Waziri Mazrui kuwa Shirika la Afya Duniani litaendelea kushirikiana na  sekta ya afya Zanzibar katika kuhakikisha mikakati ya kupambana na maradhi ya COVID 19 (corona) ikiwemo kupatiwa chanjo inafanikwa vizuri ili kuwalinda wananchi na mripuko wa maradhi hayo.

Alieleza kuwa kutokana na muingiliano mkubwa uliopo baina ya wananchi wa  Zanzibar na  watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani unaweza kupelekea maambukizi ya maradhi mbalimbali hivyo ipo haja ya kuhakikisha wananchi wanapatiwa chanjo mapema ili kuwaepusha na athari zinazoweza kujitokeza.

Alisema kuwa katika kufanikisha zoezi la chanjo ya corona Shirika litaendelea kushirikiana na Wizara ya afya kwa kusaidia kuboresha vituo vya afya na kuvijengea uwezo wa kuwahudumia wananchi pamoja na kuwapatia vifaa ili kurahisisha zoezi hilo.

Nae Waziri wa afya,Ustawi wa Jamii,Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema utolewaji wa chanjo ya maradhi ya COVID 19 na ugonjwa wa kipindupindu ni hatua muhimu na  itasaidia katika kuwaweka wananchi wa Zanzibar salama ili waweze kuendelea na haraki mbalimbali za kujitafutia maisha.

Alieleza kuwa kutakuwa na chanjo za aina mbili moja ya maradhi ya corona na ya pili ni ya ugonjwa wa kipindupindu hivyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano  katika kupatiwa chanjo hizo kwani ni muhimu kwa afya zao.

Aidha Waziri Mazrui alimueleza mwakilishi huyo kuwa chanjo ya maradhi ya kipindupindu inatarajiwa kutolewa hivi karibuni kutokana na mvua zilizonyesha   ambazo zinaweza kuleta mripuko wa maradhi ya kipindupindu.

“Tutawapatia chanjo hiyo wafanyakazi wa afya,wafanyakazi wa viwanja vya ndege, wazee pamoja na wananchi wote kwani ni muhimu kwao na pia ni salama na ninawaasa wananchi waache kusikiliza maneno ya upotoshaji mitandaoni kwani hayana ukweli wowote” alisema Waziri.

Alieleza kuwa miongoni mwa hatua za awali zitakazo chukuliwa katika zoezi hilo ni kutoa elimu kwa wananchi wote wa Zanzibar ili waelewe umuhimu wa chanjo hizo kwa lengo la kufanikisha mkakati huo pamoja na kuwataka wananchi watoe ushirkiano mzuri katika kufanikisha zoezi hilo.

Alifafanuwa kuwa ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na ukuaji wa uchumi wa taifa kwa jumla unategemea na uwepo wa afya bora kwa wananchi hivyo amewataka wananchi kupatiwa chanjo ili kusaidia ukuaji wa uchumi wao na wataifakwa ujumla.

Kwa upande wake Mwakilishi wa shirika la afya Duniani aliepo Zanzibar Dk.Girman Andermichael amesema WHO inafanya kazi kwa karibu na sekta ya afya Zanzibar kwa muda mrefu na kufanikiwa katika kusaidia miradi mingi ya afya Zanzibar ikiwemo kutoa vifaa na wataalamu.

Alieleza kuwa bado kuna uhitaji wa vifaa tiba katika vituo vingi vya afya Zanzibar na kuahidi kuwa shirika litaendela kufanya jitihada mbalimbali kwa upande wa Zanzibar katika kuhakikisha chanjo za maradhi yote zinapatikana nchini.

Wakati huohuo mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya Watu Ulimwenguni (UNFPA),Jacqueline Mahon amemkabidhi Waziri wa afya,Ustawi wa Jamii,Wazee jinsia na Watoto msaaa wa vifaa tiba ikiwemo mashine za kumsaidia mama kupumua kwaajili ya matibabu ya kusaidia mama na mtoto, wenye thamani ya dola za kimarekani laki moja na elfutano mia moja na ishirini na nne(105,124 USD).

Mwakilishi huyo alisema lengo la msaada huo ni kusaidia jitihada za Rais wa Zanzibar katika kuboresha sekta ya afya na kufikia malengo ya maendeleo endelevu na yakitaifa ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga hapa Zanzibar.

Aidha mwakilishi huyo ameahidi kufanya kazi pamoja na sekta ya afya ilikuongeza kasi ya kupunguza vifo vinavoweza kuzuilika vya akina mama na watoto wachanga Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.