Habari za Punde

Hakuna Sababu ya Kuwa na Watoto Wanaodhurura Mitaani - DKT. JINGU

Na Mwandishi wetu, Dar es salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema hakuna sababu ya kuwa na Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa kipindi hiki cha elimu bila malipo.

Akizindua mwongozo wa usimamizi shirikishi wa programu za Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi leo Jijini Dar es Salaam Dkt. Jingu amesema tatizo la Watoto kuzurura mitaani hasa katika miji mikubwa linahitaji suluhisho la pamoja ili kupata Kizazi imara.

"Kwa namna ya pekee naomba nizungumzie kundi moja muhimu kwa Watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hususani wanaokaa na kufanya kazi mitaani. Hakuna sababu ya kuwa na watoto hawa hasa kipindi hiki cha elimu bure, lakini pamoja na hayo bado Kuna watoto hawaendi shuleni hasa kwenye miji mikubwa.

Hili kundi tusiposhughulika nalo vizuri hatutakuwa tumetimiza majukumu yetu, tushirikiane pamoja kwani kesho na kesho kutwa hawataweza kufanya shughuli za halali hivyo tuzuie  hili" alisisitiza Dkt. Jingu.

Alifafanua kuwa tatizo la kuwa na makundi ya watoto wa mitaani ni la kijamii linalohitaji ushirikiano wa pamoja kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa ili kuhakikisha linatokomezwa.

Aliongeza kuwa, kundi hilo lipo katika hatari zaidi ya kufanyiwa vitendo vya ukatili hasa ubakaji na ulawiti, hivyo kuambukizwa magonjwa kama UKIMWI na kupata athari za kisaikolojia.

Kutokana na watoto hao kukosa ulinzi wanakuwa wepesi kufanyiwa vitendo vya ukatili na wakati mwingine kufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa aina mbalimbali.

Dkt. Jingu aliendelea kusema kuwa lengo la mwongozo  ni kuimarisha uwezo wa wasimamizi na watoa huduma kwa ajili ya utekelezaji wa programu za Watoto. Hivyo, ametoa wito kwa wadau wote kuja na mipango bunifu ya kuwaondoa watoto mitaani.

"Tupo hapa kuutambulisha mwongozo na baada ya hapo tuusambaze kwa watendaji, hatulengi mwongozo huu ubaki kabatini ni matarajio yetu unakwenda kutumika kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.

" Mhe. Rais Samia pamoja na makamu wa Rais wapo mstari wa mbele katika suala hili la Watoto wanaoishi katika mazingira magumu" alisisitiza Jingu.

Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Rasheed Maftaha amesema wapo tayari kuupokea na kuhakikisha unafanyiwa kazi kulingana na viwango vilivyowekwa katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri.

Aidha,ameziagiza Mamlaka zote za Serikali za Mitaa kutambua kuwa zina wajibu wa kuutekeleza mwongozo huo ikiwemo kuweka bajeti kila mwaka na kufanya tathmini ya utekelezaji wake kila baada ya robo mwaka.

Mmoja wa wadau wanaotekeleza mwongozo huo na kushiriki maandalizi yake kupitia mradi wa Achieve Levina Kikoyo amesema kuwa malengo makuu ni pamoja na kuhakikisha wanaimarisha mifumo kwa kushirikiana na Serikali kwenye masuala ya Ustawi wa Jamii katika kutoa huduma kwa Watoto walio katika mazingira hatarishi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.