Habari za Punde

Serikali Inaunga Mkono Juhudi za Taasisi Zisizokuwa za Kiserikali Kuwapatia Wananchi Huduma Mbalimbali.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Viongozo ya Jumuiya ya Zanzibar Istiqama Charitable Organization, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amesema Serikali inaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Taasisi zisizo za Kiserikali katika kuwapatia huduma mbali mbali za kijamii wananchi.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa Jumuiya ya ‘Istiqama Cheritable Organization’ ambapo pamoja na mambo mengine umefika kwa ajili ya kujitambulisha. 


Amesema serikali inaunga  mkono juhudi za Jumuiya hiyo katika kuwapatia huduma muhimu wananchi, ikiwemo huduma za elimu, Afya pamoja na huduma nyengine za kijamii, kwa kigezo kuwa uwezo wa Serikali ni mdogo kuyafikia maeneo yote.


Alisema maeneo yanayoshughulikiwa na Jumuiya hiyo yanakabiliwa na  changamoto kubwa na kusema  wakati umefika kwa taasisi binafsi za Dini zinazoshughulikia sekta ya elimu, kushirikiana na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar kutengeneza utaratibu maalum wa viwango vya taaluma.


Aidha, aliipongeza Jumuiya hiyo kwa kuanzisha  Hospitali ya Al-Rahma na kubainisha msaada mkubwa inayotowa kwa jamii, kiasi ambacho kama isingelikuwepo wanananchi wangelazimika kwenda Jijini Dar es Salaam kufuata huduma za  matibabu.


Akigusia azma ya Jumuiya hiyo ya kujenga Chuo Kikuu kupitia msaada wa Serikali ya Oman, Dk. Mwinyi aliahidi kutoa msukumo kwa wafadhili hao (serikali ya Oman) ili kuona inafanikisha  kuanza kwa mradi huo mapema iwezekanavyo.


Alisema hivi sasa Zanzibar inapita katika uchumi wa Kati, akibainisha kuwepo mahitaji makubwa ya ujenzi katika soko la Ajira.


Aidha, Dk. Mwinyi alikubali ombi la kukitembeela Chuo cha Jumuiya hiyo kiliopo Tunguu Mkoa Kusini Unguja pamoja na kutoa ahadi ya kulifanyia kazi suala la ubovu wa barabara kuelekea Chuoni huko.


Mapema, Mwenyekiti wa Jumuiya ya ‘Istiqama Cheritable Organization’ Salum Mohamed Salum alisema uongozi wa Chuo hicho unakusudia kuanzisha Chuo cha Elimu ya Juu katika eneo hilo la Tunguu, kati fani za Ufundi, ualimu na Biashara kwa msaada wa Serikali ya Oman, kwa gharama  ya Dola za Kimarekani Milioni 20.


Alisema mradi huo umeshindwa kutekelezwa kwa wakati kutokana na changamoto ya taratibu za Kidiplomasia .


Alisema Jumuiya hiyo mbali na kutoa elimu ya Dini na elimu mchanganyiko, pia inajihusisha na masuala ya Afya pamoja na masuala mbali mbali ya kijamii.


Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyektii wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  kwa kuwepo madarakani na kuiletea nchi maendeleo.


Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822  

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.