Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Majaliwa Atoa Pole kwa Familia ya Marehemu Kwandikwa.

Waziri Mkuu, Kiassim Majaliwa akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Ushetu , Mhe. Elias Kwandikwa wakati alipokwenda kuhani msiba nyumbani kwa marehemu Kibaha Picha ya Ndege
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waombolezaji katika msiba wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  na Mbunge wa Ushetu, Mhe.  Elias Kwandikwa, nyumbani kwa marehemu, Kibaha Picha ya Ndege
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akimpa pole,  Emmanuel Kwandikwa  ambaye ni kaka wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  na Mbunge wa Ushetu, Mhe.  Elias Kwandikwa, nyumbani kwa marehemu, Kibaha Picha ya Ndege, Agosti 4, 2021.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa kimeacha pengo serikalini na Bungeni kwani marehemu alikuwa mchapakazi, mwadilifu na mtulivu katika utendaji kazi wake.

 

Amesema hayo leo Jumatano (Agosti 4, 2021) alipokwenda nyumbani kwa marehemu Kwandikwa, Kibaha Picha ya Ndege mkoani Pwani kutoa pole kwa familia.

 

“Mchango wake wa utendaji katika Serikali  na Bunge ni mkubwa sana alifanikiwa kuwavutia wengi kwa tabia yake ya upole, unyenyekevu na uzingatiaji wa taratibu na sheria za utumishi  kila alipopangiwa kufanya kazi hivyo kifo chake ni pigo kwa taifa”

 

Mheshimiwa Majaliwa ameishukuru familia kwa kuridhia maombi ya kutaka mazishi yafanyike Jumatatu ijayo ili kuwapa nafasi waombolezaji wakiwemo wabunge kupata nafasi ya kusafiri kutoka waliko na kushiriki katika kutoa heshima za mwisho na mazishi.

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu leo  amekwenda nyumbani  kwa marehemu Biswad Msuya, Kaka Mkubwa wa Mkurugenzi Mkuu wa  Usalama wa Taifa kutoa pole kwa familia kufuatia kifo cha mpendwa wao.

 

Akizungumza na wafiwa na waombolezaji katika msiba huo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa amepokea taarifa ya kifo cha marehemu Biswad kwa mshtuko mkubwa na amewataka waombolezeji wamuombee mke wa marehemu na familia ili awape utulivu na uvumilivu wakati huu wa majonzi. 

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATANO, AGOSTI 4, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.