Habari za Punde

Wajasiriamali Pemba waaswa kubadili mfumo wa shughuli zao

Washiriki wakiwa katika kazi za makundi wakati wa mafunzo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Idara ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kutoka Ofisi ya Rais, kazi, uchumi na uwekezaji Zanzibar, Amin Omar Ali akiendelea na mafunzo.
Mmoja wa washiriki Meiye Hamad Juma akiwasilisha kazi za vikundi wakati wa mafunzo.
Washiriki wa mafunzo wakiendelea na mafunzo 

WAJASIRIAMALI kisiwani Pemba wameaswa kubadili mfumo wa uendeshaji wa shughui zao kwa kufanya utafiti wa kibiashara kabla ya kuanzisha biashara au huduma ili kuendana na matakwa ya mazingira husika.

Wito huo umetolewa na afisa kutoka Idara ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kutoka Ofisi ya Rais, kazi, uchumi na uwekezaji Zanzibar, Amin Omar Ali wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wajasiriamali kisiwani humo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar, (TAMWA ZNZ) kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi (WEZAIII) unaofadhiliwa na Milele Zanzibar Foundation.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyowajumuisha washiriki wanawake 25 kutoka vikundi vya ujasiriamali katika Wilaya za Micheweni, Chake chake, Wete na Mkoani afisa huyo alisema wajasiliamali wengi wanashindwa kufanikiwa kutokana na kuanzisha biashara kwa kuigana pasipo kufanya utafiti.

Alisema licha ya nguvu kubwa ambayo wajasiriamali wengi wamekuwa wakiitumia kuanzisha shughuli mbalimbali lakini shughuli nyingi zinashindwa kuendelea kutokana na utamaduni mbaya wa wajasiriamali kuigana jambo linalopelekea kuzalisha bidhaa nyingi za aina moja kuliko mahitaji yenyewe.

“Ukiangalia huko kwenye vikundi vyetu vya ujasiriamali kikundi kimoja kikianzisha mradi wa kuzalisha sabuni na wengine wakishaona hivo nao watakuja na kuzalisha vilevile bila kuangalia ukubwa soko,” alisema.

Alieleza, ‘tatizo hilo limepelekea wajasiriamali wengi kukata tamaa ya kuendelea na shughuli zao za uzalishaji hasa baada ya kupata hasara kutokana na wingi wa bidhaa ambazo ni zaidi ya mahitaji ya wateja wenyewe.”

Kutokana na hiyo afisa huyo aliwasisitiza wajasiriamali kuachana na dhana hiyo ya kufanya biashara kwa mazoea na badala yake waongeze ubunifu zaidi kwa kufanya ufatiti wa mazingira ya kibiashara kabla ya kuanzisha shughuli fulai ili kuepukana na hasara wanazozipata.

Mshiriki wa mafunzo hayo Bashira Mktuba Abdalla kutoka shehia ya Mkungu alisema ukosefu wa taaluma ya ujasiriamali ndicho kikwazo kikubwa kinachopelekea wajasiriamali wengi kushindwa kufanikiwa licha ya kuwa na hamu kubwa ya kuanzisha biashara mbalimbali.

Alisema, “wajasiriamali wengi tunahamu ya kuanzisha biashara ndogondogo kwaajili ya kujipatia kipato lakini kinachotukwaza ni kukosa elimu nzuri ya ujasiriamali ndiyo maana unakuta tunafanya kazi kwa kuigiliziana tu mtu ukiona mwenzako kaanzisha hiki na anauza basi namimi naanzisha kitu hichohicho.”

Nae Fatma Ali Msanifu kutoka shehia ya Kangagani alishukuru uwepo wa mradi wa WEZAIII kwani umesaidia kuwafumbua macho wajasiriamali kwa kubuni shighuli mbalimbali za ujasiriamali na kuondokana na mazoea.

“Kwakweli tunashukuru sana mafunzo ambayo tunayapata kupitia mradi huu yanatusaidia sana kutubadilisha kutoka kwenye dhana ya kufanya ujasirimali kwa kuigiliziana na badala yake sasa tumeanza kubuni bidhaa mbalimbali kulingana na mahitaji ya wateja,” alisema.

Mapema afisa uwezeshaji wanawake kiuchumi wa mradi huo, Asha Mussa Omar alisema uwepo wa mradi huo umelenga kuwawezesha wanawake kukabiliana na hali ngumu ya maisha kupitia shughuli za ujasriamali.

Alisema kutokana na wajasiriamali wengi hasa wanawake kukumbana na changamoto za ukosefu wa taaluma ya mbinu bora za ujasiriamali, kupitia mafunzo hayo watapata fursa ya kujifunza mbinu hizo ili kufanikisha lengo la kujiinua zaidi kiuchumi.

“Kadri ambavyo mtaendelea na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ndivyo mtaweza kuongeza kipato, na sisi TAMWA ZNZ hilo ndilo fahari yetu kuona kwamba tumewawezesha wajasiriamali na wanaendelea na uzalishaji wa bidhaa kwa kuzingatia mahitaji ya masoko,” alisema.

Katika mafunzo hayo wajasiriamali wamefanikiwa kujifunza juu ya mbinu za ubunifu na utafiti kabla na baada ya kuanzisha biashara pamoja na utafutaji wa masoko.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.