TAREHE 10 SEPTEMBA, 2021 – DODOMA
Shukrani
1.
Mheshimiwa Spika, leo hii tunafikia
tamati ya Mkutano wa Nne wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza
kikao chake cha kwanza tarehe 31 Agosti, 2021. Hivyo, hatunabudi kumshukuru
Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote zilizopangwa
kwenye mkutano huu tukiwa buheri wa afya.
2.
Mheshimiwa Spika, vilevile, ninakushukuru
wewe binafsi kwa kumudu kuliongoza vema Bunge hili tukufu, ukisaidiwa na Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge. Aidha, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa
michango mizuri mliyoitoa kwa kusema na kwa maandishi wakati wa kuchangia hoja
mbalimbali zilizowasilishwa na Serikali kwenye mkutano huu.
3.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu
kuwa, Serikali kwa upande wake ipo tayari muda wote kupokea michango yenu yenye
lengo la kusaidia kuboresha utekelezaji wa mipango yake.
Salamu za Pole
4.
Mheshimiwa Spika, niungane na
Waheshimiwa Wabunge wenzangu kukupa pole kufuatia taarifa za kuhuzunisha za kifo cha Mheshimiwa Elias
John Kwandikwa aliyekuwa Mbunge wa Ushetu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa kilichotokea tarehe
2 Agosti, 2021. Aidha, natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki
na wananchi wote wa Jimbo la Ushetu kwa kuondokewa na mwakilishi wao huyo.
5.
Mheshimiwa Spika, vilevile, natoa salamu za pole kwa Kamanda Simon Nyakoro
Siro, Inspekta Jenerali wa Polisi kufuatia tukio lililotokea
tarehe 25 Agosti, 2021 jijini Dar es Salaam, ambapo askari wetu wazalendo
wapatao watatu na mlinzi mmoja wa kampuni binafsi waliuawa wakati wakitekeleza
majukumu yao ya kiusalama. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema
na awape uponyaji wa haraka majeruhi wa tukio hilo. Amin!
6.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapa pole Watanzania wenzangu
waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki na wengine kupata ulemavu katika matukio
mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani zilizogharimu maisha ya maafisa watano
wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), waliofariki dunia tarehe 23 Agosti, 2021 wakati
wakitekeleza majukumu yao ya kikazi mkoani Songwe. Mwenyezi Mungu aziweke roho
za marehemu mahala pema peponi. Amina!
SHUGHULI ZA BUNGE
Maswali na Majibu
7.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mkutano huu wa 4 wa Bunge la 12, Waheshimiwa
Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali
ya msingi 119 na maswali 263 ya nyongeza ambayo yalijibiwa na
Serikali. Kadhalika, maswali 14 ya papo kwa papo yaliulizwa na
Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Waziri Mkuu.
Maazimio ya Bunge
8.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Waheshimiwa Wabunge walijadili na kupitisha maazimio
mawili ya Bunge kama ifuatavyo: -
Moja: Azimio la Bunge kuhusu kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula
(East African Community Protocol on Sanitary and Phytosanitary – SPS Measures);
Mbili: Azimio la Bunge
kuhusu kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
(African Continental Free Trade Area – AfCFTA); na
9.
Mheshimiwa Spika, kuridhiwa kwa maazimio haya kutasaidia nchi yetu
kuimarisha biashara na uwekezaji kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki sambamba
na kuongeza shughuli za biashara na uwekezaji wa ndani baina ya nchi wanachama
wa Umoja wa Afrika. Halikadhalika, kutaiwezesha Tanzania kuimarisha ushirikiano
na mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Afrika.
Miswada ya Sheria
10. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge pia, walijadili na kupitisha miswada
mitano ya sheria iliyowasilishwa na Serikali katika mkutano huu kama ifuatavyo:
-
Moja: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.2
wa Mwaka 2021;
Mbili: Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.4 wa Mwaka 2021;
Tatu: Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa
Mwaka 2021;
Nne: Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mwaka 2021. Marekebisho
haya pia yanakusudia kuhakikisha shughuli za zimamoto na uokoaji nchini zinafanyika
kwa ufanisi ili kuendelea kuwavutia wawekezaji kwa kuwahakikishia usalama wa maisha
na mali zao; na
Tano: Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.5 wa Mwaka 2021.
11. Mheshimiwa Spika, nirejee tena
kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri iliyotolewa wakati wa
kujadili Miswada hiyo muhimu ambayo itasaidia kuondoa mapungufu yaliyobainika sambamba
na kuboresha baadhi ya masharti katika utekelezaji wa sheria hizo. Serikali
itafanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji
wa sheria hizo unawanufaisha Watanzania.
12. Mheshimiwa Spika, niwapongeze na
kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri ya
kuwasilisha Miswada iliyojadiliwa katika mkutano huu pamoja na kutoa ufafanuzi
mbalimbali wakati wa kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Aidha, nimpongeze
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu wake kwa kazi nzuri ya kuandaa
miswada iliyowasilishwa katika mkutano huu.
MAENEO YA MSISITIZO KISEKTA
13.
Mheshimiwa Spika, jukumu langu la msingi lililonisimamisha mbele ya Bunge
lako tukufu ni kutoa maelezo mafupi hususan kuhusu shughuli za mkutano huu wa nne
wa Bunge kabla ya kuahirishwa. Hata hivyo, kabla ya kuhitimisha mkutano huu
naomba niweke msisitizo wa baadhi ya masuala kwa viongozi, watendaji na
wananchi kwa ujumla katika kutekeleza majukumu yao ya kuwaletea maendeleo.
14.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo ambayo nitayatolea msisitizo ni suala
la tozo na uendelezaji wa miundombinu ya afya ya msingi, maandalizi ya
uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari 2022, matumizi ya Mfumo
wa Stakabadhi Ghalani, ujenzi wa Mji wa Serikali, tahadhari dhidi ya UVIKO-19
na michezo.
UENDELEZAJI WA
MIUNDOMBINU YA AFYA YA MSINGI
15.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Afya ya Mwaka 2007 yenye
lengo la kuwashirikisha wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya na zahanati. Azma
ya Serikali ni kuona kila kata inapata kituo cha afya na kila kijiji kinakuwa
na zahanati ili kusogeza huduma hizo karibu na wananchi na kuwaondolea adha ya
kusafiri umbali mrefu. Hadi sasa, tarafa 363
zilizopo Tanzania Bara zina vituo vya afya vyenye uwezo wa kutoa huduma za
upasuaji za dharura, huduma za mionzi na maabara za kisasa.
16.
Mheshimiwa Spika, ili kuzifikia tarafa nyingi zaidi, Serikali imeamua, kwanza
kuzitambua kata za kimkakati na tarafa zote ambazo hazina vituo vya afya. Pili,
kutumia fedha zitokanazo na tozo za miamala ya simu kujenga vituo vya afya vya
kimkakati ambavyo vitakuwa na uwezo wa kutoa huduma za upasuaji za dharura, huduma
za mionzi na maabara za kisasa katika kata za kimkakati na makao makuu ya
tarafa hizo.
17.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali imepeleka shilingi bilioni 37.5 zilizotokana na makusanyo
ya tozo ya miamala ya simu kwenye Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya
afya kwenye tarafa 150 kati ya tarafa
207. Kila kituo cha afya kimepelekewa
shilingi milioni 250 kwa
ajili ya kuanza ujenzi huo. Natoa maelekezo kwa watendaji wote wa Serikali za
Mitaa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuakisi
thamani ya fedha kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.
MAANDALIZI YA
UANDIKISHAJI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA KWANZA, JANUARI 2022
18.
Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kwamba jana tarehe 9 Septemba, 2021 vijana
wetu wa darasa la saba walimaliza mtihani wa Taifa wa Elimu ya Msingi ulioanza tarehe
8 Septemba, 2021. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwaombea
Mwenyezi Mungu awajalie wote wafaulu vizuri na kujiunga na kidato cha kwanza,
vyuo vya ufundi na kujiendeleza na taaluma nyinginezo.
19.
Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kwa utekelezaji wa Sera ya Elimumsingi
bila Ada kumekuwa na mwitikio mzuri wa mahudhurio ya wanafunzi na hivyo kuongeza
idadi ya wahitimu katika mitihani ya kujipima na kumaliza elimu ya msingi. Ongezeko
hilo la idadi ya wahitimu, lilisababisha changamoto ya kutokuwepo kwa miundombinu
ya elimu ya kutosha hususan madarasa ya kuweza kupokea wahitimu wa darasa la
saba waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza.
20.
Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, Serikali ilitoa maelekezo kwa
watendaji wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatumia takwimu zilizopo kupanga
maoteo na kutenga fedha katika mipango na bajeti ya kila mwaka ili miundombinu
ya elimu, samani na shule hitajika viwepo kwa wakati.
21.
Mheshimiwa Spika, maelekezo hayo, yalilenga kuiwezesha Serikali kutambua
mahitaji ya miundombinu ya elimu yatakayokidhi idadi hiyo ya wanafunzi na hivyo
kuhakikisha miundombinu hiyo inaandaliwa mapema. Katika mwaka 2021, makadirio
yanaonesha kuwa wanafunzi 934,706
sawa na asilimia 83.68 ya wanafunzi 1,115,041 waliohitimu mtihani
wa darasa la saba wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo
Januari, 2022.
22.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana
na uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari, Serikali imetumia
shilingi bilioni 33.73 kwa ajili ya kujenga maboma 2,699 kati ya maboma 4,539 ya vyumba vya madarasa kwenye
maeneo mbalimbali nchini. Fedha hizo
zinatokana na tozo ya miamala ya simu.
23.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba tayari
Serikali imepeleka shilingi
bilioni saba kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 560 ikiwa ni awamu ya kwanza. Aidha, maboma 1,840 yatakayogharimu shilingi bilioni 23 yatakamilishwa
kupitia ruzuku ya Serikali Kuu.
24.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kurejea maelekezo niliyoyatoa wakati
nikifungua mafunzo elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa
kwamba wahakikishe miundombinu hiyo inakamilika kwa wakati. Lengo la Serikali ni
kuona vijana wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani wanapokelewa
na kuanza masomo yao kwa wakati.
BEI ELEKEZI YA
MAFUTA
25.
Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Agosti, 2021 Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati
nchini (EWURA) ilitangaza bei mpya elekezi kwa bidhaa za mafuta kwa mwezi
Septemba ambapo ilionesha kupanda kwa bei za bidhaa hizo. Kufuatia taarifa hiyo,
na malalamiko ya wananchi juu ya kupanda kwa bei za bidhaa hizo, tarehe 1
Septemba 2021, Serikali ilisitisha bei mpya zilizotangazwa na EWURA ili kufanya
mapitio ya kina ya kupanda huko kwa bei.
26.
Mheshimiwa Spika, tulichukua hatua hizo kutokana na ukweli kwamba kupanda
kwa bei ya mafuta huwaumiza wananchi hususan wale wa hali ya chini. Kwa
kulitambua hilo, tarehe 2 Septemba, 2021, niliunda timu maalumu ya uchunguzi.
27.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine timu hiyo inafuatilia kupanda
kwa bei za bidhaa za mafuta mara kwa mara hususani petroli, dizeli, mafuta ya
taa na ndege na kisha kuishauri Serikali hatua stahiki za kuchukuliwa. Aidha,
nimeielekeza timu hiyo ijiridhishe kuhusu utitiri wa tozo kwenye bidhaa za mafuta
na kuja na mapendekezo ya namna nzuri ya kushughulikia suala hilo.
28.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa timu hiyo tayari
imeanza kutekeleza majukumu yake tangu tarehe 2 Septemba, 2021. Hali kadhalika,
itakapokamilisha taarifa yake Serikali itatoa mwelekeo wa yale
yatakayopendekezwa.
MFUMO WA STAKABADHI ZA MAZAO GHALANI NA USHIRIKA
29. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maeneo
ambayo Serikali inayapa msukumo wa kutosha ni masoko na mifumo ya mauzo ya
mazao ya wakulima. Serikali inachukua hatua hizi ili kuhakikisha kuwa wakulima
wanapata tija na kunufaika na mazao yao. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali
imeondoa mifumo isiyo rasmi ya ununuzi wa mazao ambayo imekuwa ikiwakandamiza
wakulima na kuwanufaisha baadhi ya wanunuzi wasiokuwa waaminifu. Mathalan,
tuliondoa mifumo kama vile kangomba,
butula, chomachoma, kula maua, njemke na mingineyo ambayo ilikuwa
ikimpunja na kumnyonya mkulima.
30. Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, Serikali
imekuwa ikisimamia kikamilifu mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani ambao umeonesha
mafanikio makubwa katika uuzaji wa mazao yakiwemo korosho, ufuta, dengu, choroko na kakao. Kwa lugha nyingine, ufanisi
wa mfumo huo, umekuwa kichocheo katika kupunguza umaskini na kuongeza uchumi wa
nchi na wakulima kwa ujumla.
31. Mheshimiwa Spika, taarifa zinaonesha
kuwa kuuza mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na ushirika kunatoa nguvu
ya pamoja kwa wakulima katika upatikanaji wa masoko sambamba na kuimarisha bei
ya mazao husika. Minada iliyofanyika imesaidia kuongezeka kwa bei ya mazao yaliyotumia
mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwemo korosho,
ufuta, dengu, choroko na kakao.
32. Mheshimiwa Spika, mwaka 2020 bei ya
choroko iliongezeka kutoka shilingi 600 kwa kiwango cha chini hadi 800 kiwango cha
juu kwa kilo na kufikia shilingi 900
hadi 1,300 kwa kilo katika vituo vya Magu,
Uzogele, Igunga na Manyoni. Kadhalika, hivi karibuni tumeona bei ya kakao
ikiongezeka maradufu kutoka shilingi 2,500
hadi 5,000 kwa kilo baada ya kutumia mfumo wa stakabadhi
ghalani.
33. Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, natoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo kushirikiana kwa
karibu na vyama vya ushirika na vyama vya msingi katika kuhakikisha wanawawezesha
wakulima kupata elimu na manufaa ya kutumia mfumo wa
stakabadhi ghalani bila usumbufu ili uwapatie tija.
34. Mheshimiwa Spika, ni kweli mfumo wa
stakabadhi ghalani unahitaji miundombinu ya maghala. Hata hivyo, changamoto
hizo zinaendelea kufanyiwa kazi ili mazao mengi zaidi yaingizwe kwenye mfumo huo
mwaka hata mwaka na kuleta tija zaidi kwa wakulima.
35. Mheshimiwa Spika, rai yangu kwa wakulima
na wanunuzi wa mazao ni kwamba, mfumo wa stakabadhi ghalani ndiyo pekee uliothibitika
na kuonesha matokeo makubwa yenye manufaa. Hivyo basi, tuendelee kuuimarisha
katika mazao yote ya biashara nchini ili kuleta mafanikio kwa wakulima na Taifa
kwa ujumla.
UNUNUZI WA NAFAKA NCHINI
36.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuhamasisha
uzalishaji wa mazao ya chakula hususan nafaka pamoja na mazao ya biashara. Ongezeko
hili la uzalishaji linakwenda sambamba na jitihada za Serikali za kuimarisha
masoko ya ndani ya mazao pamoja na kutafuta masoko ya nje.
37.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuboresha mifumo ya masoko,
Serikali inahamasisha ujenzi wa
viwanda vya uchakataji wa mazao yanayozalishwa hapa nchini ili kuimarisha bei
ya mazao hayo na hivyo kumpatia tija mkulima.
38.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuanza kwa
msimu wa ununuzi wa mahindi hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, tulipokea
malalamiko ya wananchi kuhusu umbali wa vituo vya kununulia mahindi na bei
kutoridhisha. Kama mnavyofahamu, kwa kiasi kikubwa ununuzi wa mahindi nchini
hufanywa na wafanyabiashara binafsi.
Hata hivyo, ili kuimarisha bei ya mahindi, Serikali hutoa fedha kwa Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko
(CPB).
39.
Mheshimiwa Spika, jana tarehe 9 Septemba 2021, Bunge lako tukufu lilipokea hoja binafsi
kutoka kwa Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo na kuungwa mkono na Waheshimiwa
Wabunge. Hoja hiyo, ililenga kuishauri Serikali kuingilia kati soko la mahindi
ili kunusuru wakulima wa zao hilo.
40.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa shilingi
bilioni 15 kwa ajili kuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
kununua mahindi maeneo mbalimbali nchini. Pia, Serikali ilitoa kwa Bodi ya
Nafaka na Mazao Mchanganyiko shilingi bilioni 10 kuongeza mtaji wa
ununuzi wa mazao.
41.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua
kuwa kiasi hicho cha fedha ni kidogo ukilinganisha na uzalishaji wa mahindi
uliopo. Hivyo, Serikali imesikia kilio cha wakulima kupitia Waheshimiwa Wabunge
na kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa wakulima wa mahindi wanapata soko
la mahindi waliyozalisha.
42.
Mheshimiwa Spika, tayari Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa shilingi bilioni 50 na ununuzi utaanza
Jumatatu, tarehe 13 Septemba, 2021. Hivyo, Wizara iendelee kutafuta masoko ya
mahindi kwa kukamilisha mikataba mipya ya ununuzi wa mahindi na nchi za Sudan
ya Kusini, DRC na Zimbabwe.
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia
imeruhusu wafanyabiashara kutafuta masoko ya nje ya nchi ambapo vibali vya
usafirishaji hutolewa kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Aidha, uuzaji wa
chakula utafanywa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na hifadhi
ya kutosha ya chakula. Niendelee kusisitiza Wizara kushirikiana na Sekta
Binafsi katika kuongeza thamani ya mazao yetu ikiwemo mazao ya nafaka badala ya
kuyauza nje yakiwa hayajaongezwa thamani.
44.
Mheshimiwa Spika, naiagiza Wizara ya Kilimo kuisimamia kwa karibu NFRA na CPB ili zinunue
mahindi ya wakulima pekee, tena watoke ndani ya nchi. Aidha,
ongezeni vituo vya kununulia mahindi hadi wilayani na kwenye miji midogo.
45.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Serikali inafuatilia mwenendo wa upatikanaji wa mbolea ili
kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wingi na bei nafuu. Lengo la Serikali
ni kuwezesha wakulima kumudu gharama za mbolea.
UJENZI WA MJI WA SERIKALI
46.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi
wa Mji wa Serikali, mradi ambao unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Itakumbukwa
kuwa katika awamu ya kwanza, Wizara 23 zilijenga ofisi zake na
kuhamishia watumishi wapatao 18,300 jijini Dodoma. Aidha, ujenzi wa majengo ya kudumu ya wizara 23 na taasisi
zake utaanza tarehe 30 Septemba, 2021. Ujenzi huo, utahusisha ipasavyo kampuni za
ujenzi za umma na binafsi.
47.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru
na kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuridhia shilingi bilioni 300 zitumike katika awamu ya pili
ya ujenzi huo. Kadhalika, shilingi bilioni 300 nyingine zitatolewa kadri ujenzi unavyoendelea. Hivi
sasa, ujenzi wa miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, majisafi na majitaka,
umeme, gesi, mifumo ya TEHAMA, huduma za zimamoto na upandaji miti unaendelea
vizuri na kasi kubwa.
TAHADHARI DHIDI YA
UVIKO-19
48.
Mheshimiwa Spika, Tanzania na dunia kwa ujumla
bado imeendelea kupambana na ugonjwa wa virusi vya korona maarufu kama UVIKO-19.
Janga limesababisha baadhi ya ndugu zetu kupoteza maisha na wengine kuendelea
kuugua. Hivyo basi, hatuna budi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kujikinga na
maambukizi ya UVIKO-19.
49.
Mheshimiwa Spika, ninawasihi Waheshimiwa Wabunge
wenzangu na wananchi wote, tufuate maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya
na pale mtu anapoona dalili ambazo hazielewi, awahi kwenye kituo cha kutolea
huduma za afya kilicho karibu ili afanyiwe uchunguzi na kupatiwa matibabu.
50.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine ya kukabiliana na UVIKO-19, tarehe 28 Julai, 2021 Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi kampeni
ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo. Hivi sasa, chanjo hiyo inapatikana maeneo yote
nchini katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya wilayani na mikoani.
51.
Mheshimiwa Spika, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote kuwa chanjo hii
ni salama na haina madhara yoyote. Chanjo hiyo ambayo imethibitishwa na
watalaamu na maabara zetu, ni hiyari lakini ni muhimu. Hivyo, niwaombe twendeni
tukachanje ili kukabiliana na janga hili.
MATUMIZI YA MITANDAO
52.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumejitokea
tabia ya baadhi ya watu kutumia vibaya haki ya uhuru wa mawazo na mifumo
mbalimbali ya mawasiliano. Matumizi mabaya ya mitandao yamesababisha kusambazwa
kwa taarifa za upotoshaji, kashfa, kutisha, na wakati mwingine kudhalilisha
watu, kikundi au viongozi.
53.
Mheshimiwa Spika, katika kulinda na kutunza
usalama, amani, maadili, umoja na mshikamano wa nchi ninawaagiza Mawaziri wa
Mambo ya Ndani na mwenzake wa Habari na Teknolojia ya Mawasiliano watumie
sheria, kanuni na taratibu zilizopo kuhakikisha vitendo na mienendo hiyo
inadhibitiwa nchini.
MICHEZO
54.
Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kwamba kumekuwepo na mwamko
mkubwa wa masuala ya sanaa, burudani na michezo nchini. Hivi sasa, michezo imekuwa
chanzo kikubwa cha biashara, utalii, kuimarisha afya na ajira kwa vijana wetu.
Kwa kuzingatia hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi za kukuza
michezo nchini. Hatua hizo zinahusisha kuundwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya
Michezo na kurejesha mashindano ya UMITASHUMTA, UMISSETA na SHIMIWI.
55.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia kuanzishwa kwa
Mfuko wa Maendeleo ya Michezo nchini na kukubali kudhamini mashindano ya
wanawake ya CECAFA ili kutoa motisha kwa wanawake kushiriki zaidi katika
michezo. Mashindano hayo, yatajulikana kama Samia Cup sambamba na Kagame
Cup kwa upande wa wanaume.
56.
Mheshimiwa Spika, Mfuko huo, utasaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuziandaa vyema timu zetu za Taifa za michezo mbalimbali na
kuziwezesha kushiriki kwa tija katika mashindano na michezo ya kimataifa. Pia,
utatumika kuimarisha miundombinu ya michezo na upatikanaji wa vifaa vya
michezo, kuendeleza na kuwezesha shule na vituo vya umahiri wa michezo,
kuendesha programu za mafunzo ili kupata wataalaamu wa kutosha, kuwezesha
programu za michezo kwa jamii na mashindano ya kitaifa na kimataifa.
57.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kueleza, michezo ni biashara na
imekuwa chanzo muhimu cha ajira hususan kwa vijana. Aidha, ibara ya 243 ya
Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 inaielekeza Serikali
kuanzisha mfumo thabiti wa michezo ya kulipwa ili kulinda na kuendeleza vipaji
vilivyopo kwa manufaa ya Taifa letu na vijana kujipatia ajira kwa kutumia vipaji
vyao. Tayari, Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imefanyiwa mabadiliko
na kuruhusu michezo ya kulipwa na baadhi ya timu zetu zimeshaingia kwenye mfumo
huo.
58.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa sheria hiyo, hivi karibuni,
tumeshuhudia watalaamu wa michezo na wachezaji kutoka katika mataifa makubwa
yaliyoendelea kimichezo wakija nchini kutafuta ajira kupitia michezo. Vilevile,
tumeshuhudia uwekezaji mkubwa kwenye vilabu vyetu vikubwa nchini hususan Azam,
Simba na Yanga na kuvifanya viendeshwe kibiashara.
59.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kwanza kuupongeza uongozi wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia kwa usimamizi
mzuri wa soka nchini. Pili, nawapongeza sana wawekezaji na watendaji wa vilabu
vya Azam, Simba na Yanga kwa uwekezaji mkubwa na usimamizi mzuri wa vilabu
hivyo kwenye soka letu ambao umeanza kuzaa matunda.
60.
Mheshimiwa Spika, ninataka niwahakikishie wadau na wapenzi wa michezo
kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kuvutia uwekezaji mkubwa katika tasnia
ya michezo. Lengo ni kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wetu kimichezo ili
waweze kushindana katika masoko ya michezo ya ndani na nje ya nchi, na hivyo
kuimarisha ajira, mapato yatokanayo na shughuli za michezo pamoja na mchango wa
sekta ya michezo katika pato la Taifa.
61. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuipongeza timu yetu ya Taifa ya
Mpira wa Miguu (Taifa Stars) kufuatia ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi
ya Madagascar na hivyo kuongoza KUNDI J
katika hatua ya pili ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.
Vilevile, tunaitakia kila la heri timu yetu ya wanawake ya
kriketi inayoshiriki mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la mchezo huo
nchini Botswana na timu yetu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) itakayoshiriki mashindano ya COSAFA nchini Afrika Kusini kuanzia tarehe 28 Septemba,
2021 pamoja na kuitakia mafanikio timu yetu ya mchezo
wa wavu inayoendelea kushiriki mashindano ya Afrika ya mchezo huo nchini
Rwanda. Ninavitakia kila la
heri pia vilabu vyetu vya Azam, Biashara United, Simba na Yanga katika
uwakilishi wao kwenye michuano ya Shirikisho na Ligi ya Mabingwa ya Chama cha
Soka barani Afrika (CAF).
62. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia
kukipongeza kituo cha matangazo cha Azam (Azam Media) hususan upande wa matangazo ya
runinga kwa kuuibua na kuutangaza vyema mchezo wa masumbwi nchini. Juhudi hizo
za Azam
Media wakishirikiana na wadau wengine zimewezesha wanamasumbwi wetu kutumia
vizuri fursa hiyo kukuza vipaji vyao.
63. Mheshimiwa Spika, niwapongeze mabondia wetu Twaha Kiduku kwa
kumtwanga Dulla Mbabe katika pambano lililovuta hisia za Watanzania wengi.
Vilevile, nimpongeze bondia Hassan Mwakinyo kwa kumdunda mpinzani wake Mnamibia
Julius Indongo kwa TKO na kutetea mkanda wake wa Chama cha Ngumi Afrika
(ABU). Wanamasumbwi wetu wameendelea kuifanya Tanzania itambulike zaidi
ulimwenguni. Sasa tunasubiri pambano la watani Mwakinyo dhidi ya Kiduku.
HITIMISHO
64.
Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kumshukuru Katibu wa Bunge
na watendaji wa ofisi ya Bunge kwa kazi kubwa ya kuratibu vikao vya mkutano
huu. Aidha, niwashukuru watendaji wa Serikali kwa kufanikisha shughuli
zilizopangwa na Bunge lako tukufu kwa weledi na ufanisi mkubwa.
65.
Mheshimiwa Spika, kipekee, niwashukuru wanahabari kwa kufikisha habari kuhusu
mkutano huu kwa wananchi. Nivishukuru pia vyombo vya ulinzi na usalama kwa
huduma wanazozitoa kwa washiriki wa Bunge hili bila kuwasahau madereva
waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa Bungeni.
66.
Mheshimiwa Spika, natambua kuwa baada ya mkutano huu Waheshimiwa Wabunge wenzangu
watakuwa wakirejea majimboni kwao kuendelea na shughuli za kuwahudumia wananchi
ikiwa ni pamoja na kuwaeleza mambo yaliyojiri hapa Bungeni. Kwa hiyo, niwatakie
safari njema na niwaombe kuwa mkawaeleze wananchi pia kuhusu matarajio yetu kwao
na kuwasihi waendelee kutuunga mkono kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
67.
Mheshimiwa Spika, tarehe 19 Oktoba 2021, ikitegemewa na mwandamo wa
mwezi, ndugu zetu Waislamu wataadhimisha Mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu
Alayh Wasallam. Hivyo, nitumie nafasi hii kuwatakia kila la heri katika
maandalizi na hatimaye maadhimisho ya shughuli hiyo ya maulid ya kuadhimisha
Mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam.
68.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa, naomba kutoa hoja kwamba
Bunge lako tukufu liahirishwe hadi tarehe 2 Novemba, 2021 siku ya Jumanne, saa
tatu kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu jijini Dodoma.
69.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment