Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amezindua Vitambulisho vya Wajasiriamali Wadogo Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizindua Vitambulisho vya Wajasiriamali Wadogo Zanzibar, uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar na (kulia kwa Rais) Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe.Masoud Ali Mohammed  na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe Mustafa Idrisa Kitwana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama.Ndg Talib Ali Talib
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Kitambulisha chake na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serekali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.Mhe. Masoud Ali Mohammed, baada ya kukizindua na kuwakabidhi Wajasiriamali Wadogo wa Unguja na Pemba,  hafla hiyo iliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Kitambulisho Mjasiriamali kutoka Mkoa wa Kusini Pemba Bi.Fatma Khamis Juma, hafla hiyo ya kuwakabidhi Vitambulisho Wajasiriamali Wadogo iliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezindua vitambulisho vya Wajasiriamali na kusema kuwa vitambulisho hivyo vina umuhimu katika kurasimisha shughuli zao, pamoja na kuwatambua kisheria kuwa ni miongoni mwa wachangiaji wa uchumi.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Vitambulisho vya Wajasiriamali, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mbali ya hatua hizo pia, kuwepo kwa vitambulisho hivyo kutawarahisishia Wajasiriamali hao kupata huduma mbali mbali zikiwemo za kupata mikopo katika taasisi kadhaa za kifedha zikiwemo benki.

“Kwa hakika leo ni siku ya furaha kubwa kwangu kuona kuwa tumeweza kuitekeleza ahadi tuliyoitoa kwa wananchi na hasa wajasiriamali wadogo hapa Zanzibar ya kuwapatia vitambulisho maalum na vya kisasa”, alisema Rais Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa pamoja na kuzingatia matakwa ya sheria mbali mbali zinazohusiana na wajasiriamali ikiwemo Sheria Namba 7 ya mwaka 2014, ambapo lengo lake ni kuweka mazingira maalum ya kuyasaidia makundi ya wajasiriamali wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi pia, alieleza malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kutoa Bilioni 100 kwa ajili ya kwuasaidia Wajasiriamali ambapo Serikali itatoa Bilioni 50 na Benki zilizoamua kuwasaidia Wajasiriamali zitatoa Bilioni 50 ambazo fedha hizo zitatumika kwa kuwatafutia mafunzo, mitaji pamoja na masoko..

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia Wajasiriamali kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina dhamira ya dhati ya kuwajengea mazingira bora ya kufanya shughuli zao Wajasiriamali Wadogo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanajengewa maeneo maalum ya kufanyia kazi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa tayari Serikali imeshaanza mazungumzo na wawekezaji katika kufanikisha ujenzi wa masoko kwa kila Wilaya Unguja na Pemba huku akitumia fursa hiyo kutoa taarifa njema kwamba katika kipindi kifupi kijacho Serikali itaanza ujenzi wa masoko katika eneo la Jumbi na Chuini kwa Nyanya.

Vile vile Serrikali ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya ujenzi katika eneo la Darajani eneo ambalo litakuwa na sura mpya na fursa nyingi zaidi kwa wafanyabiashara wadogo kufanya biashara zao kwa ufanisi

“Kwa hakika leo tunafungua ukurasa mpya wa jitihada za Serikali katika malengo yetu ya kuyaimarisha mazingira ya kufanya kazi ya wajasiriamali wetu”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza Wajasiriamali wote waliokwisha jitokeza kujisajili tokea kuanza kwa zoezi hilo na kutumia fursa hiyo kuwahimiza wale wote ambao hawajasajili kufanya hivyo katika vituo vilivyoandaliwa.

Pia, aliwahimiza Wajasiriamali wote kuitumia fursa hiyo kujisajili na kufuata taratibu zote ikiwemo kufanya kazi zao katika maeneo yaliyoruhusiwa na kuzingatia kuweka usafi kwa kushirikiana na Mabara ya Miji, Manispaa na Halmashauri zote.

Aliupongeza uongozi na Watendaji wa Kampuni ya AIM GROUP LIMITED kutoka Dar-es-Saalam kwa kazi nzuri ya utayarishaji wa mfumo wa usajili wa Wajasiriamali wadogo Zanzibar ambao leo umezinduliwa rasmi na kuwawezesha Wajasiriamali kupata vitambulisho vyenye ubora

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed amesema kuwa hatua hiyo inatengeneza misingi imara katika kundi muhimu nchini katika suala zima la maendeleo ya kiuchumi, huku akibainisha kwamba ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025.

Imetayarishwa na kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.