Habari za Punde

Wajasiriamali Watakiwa Kuongeza Ubunifu Katika Uzalishaji wa Bidhaa Zao.

Maofisa wa TAMWA ZNZ wakiwatembelea Wanawake Wajasiriamali wanaojishughulisha na ushonaji wa mikeka na mikoba ya ukili katika Kijiji cha Bambi Wilaya ya Kati Unguja.
Miongoni mwa wanakikundi cha USAWAKI wakiwa katika hatua za awali za uandaaji wa sabuni ya Mche huko Bambi mkoa wa kusini Unguja,kikundi hicho kinasimamiwa na TAMWA-ZNZ chini ya ufadhili wa Milele Zanzibar Foundation.
Baadhi ya wanakikundi cha USAWAKI wakiwa kwenye hatua za utowaji wa sabuni za mche kupitia mashine ya utengezaji wa sabuni hizo huko Bamba mkoa wa kusini Unguja,kikundi hicho kinasimamiwa na TAMWA-ZNZ chini ya ufadhili wa Milele Zanzibar Foundation.

Na Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ.

Imelezwa kuwa Zanzibar inaweza kupunguza idadi kubwa ya uingizwaji wa sabuni iwapo Serikali na taasisi binafsi zitaamua kuwaunga mkono wajasiriamali tofauti ambao wanajikita na uzalishaji wa sabuni hizo.

Kauli hio imetolewa na Mwenyekiti wa kikundi  cha wanawake ambao wanajishughulisha na uzalishaji wa sabuni (USAWIKA) Haitham Mbarouk kilichopo Bambi Wilaya ya kati Unguja.

Alisema kwa kuwa wanawake kupitia kiwanda wanachofanyia kazi wana uwezo wa kuzalisha sabuni za mche zipatazo 180 kwa siku idadi ambayo wanaamini inaweza kuongezeka iwapo wangekua na soko la uhakika ambalo limekosekana kwa sababu mbali mbali zikiwemo zile za wanajamii kutopenda vitu vinavozalishwa na wazawa.

Alisema hadi sasa kupitia kikundi chao ambacho kina wanachama wapata 25 ambao wote ni wanawake wamekua wakifanya uzalishaji huo huku wakikosa sehemu sahihi ya kuuza bidhaa hizo badala yake hukaa muda mrefu bila ya soko.

Sambamba na hayo alisema kwa sasa bei ya mche mmoja wa sabuni inayotokana na 2300 ambayo inatokana na mali ghafi za asili ya Zanzibar ikiwemo mwani,karafuu pamoja njano ambazo zote hizo ni aina zenye kuvutia.

Akizungumza kwa niaba ya Milele Zanzibar Foundation Alice  Mushi aliwataka wajasiriamali hao kuongeza ubunifu zaidi katika uzalishaji wa bidhaa hizo kwa kuwa wateja huhitaji zaidi bidhaa zenye ubora na kiwango bora.

Pamoja na hayo aliwataka wajasirikiamali hao kutanua  wigo zaidi na kutoridhika na soko dogo walilonalo badala yake wafikiri mbali zaidi ikiwa ni pamoja na kusaka masoko ya kitalii yaliopo katika mahoteli mbali mbali visiwani hapa.

Akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar,(WEZA) Afisa kutoka TAMWA-ZNZ Nairat Abdalla alisema utelezaji huo wa awamu ya tatu uliwashirikisha wanufaika wapatao 1752 kutoka Unguja na Pemba huku lengo kuu likiwa ni kupunguza umasikini visiwani hapa.

Alisema katika mradi huo walengwa wakuu ni wanawake na vijana ambao anaamini kuwa ndio jamii ya watu wanaopaswa kuungwa mkono zaidi na kwaharaka ili waweze kuleta maendeleo kwa wote.

Mradi huo unaotekelezwa na TAMWA-ZNZ unafadhiliwa na Milele Zanzibar Foundation na unatekelezwa katika shehia zipatazo 24 Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.