Habari za Punde

JE UTAKUMBUKWA KWA LIPI?

 

Na. Adeladius Makwega.  Kinole Morogoro

Tangu Mzee Augustno Lyatonga Mrema kuondoka CCM na kwenda upinzani yaani NCCR MAGEUZI na baadaye TLP sasa ni miaka zaidi ya 26.Kwa hakika huo ni umri wa mtu mzima ambaye ameshaanza kupiga kura kumchagua Diwani, Mbunge na hata Rais.

Kuwepo kwake upinzani Mrema amefunikwa na giza moja huku akitazamwa na baadhi ya watu kama ni mtu mamruki, dhaifu tu wala siyo mwanasiasa wa kweli ambaye hajawahi kufanya lolote lile.

Japokuwa kuna mtazama huo Augustino Lyatonga Mrema ni mwanasiasa makini sana ambaye amewahi kulitumikia taifa hili kwa moyo wote ambapo kwa wale tuliwahi kumuona na kushuhudia tunaweza kuwa mashahidi.

Mwaka 1992 nikiwa mwanafunzi wa Tambaza sekondari Ndugu Mrema alifika shuleni hapa na kuzungumza na wanafunzi wa shule hii ili kutatua mgogoro usafiri wa wanafunzi Dar es Salaam.

Katika kikao hicho mie nikiwa mwanafunzi wa kidato cha pili na Mrema akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na baadaye akawa Naibu Waziri Mkuu alifika hapo kwa hoja moja tu ya kutatua mgogoro uliokuwepo baina ya makondakta wa chai maharage (Daladala za wakati huo) na wanafunzi juu ya idadi ya wanafunzi katika kila Chai Maharage.

Mgogoro huu ulileta taharuki huku wanafunzi wa Tambaza wakifanya vurugu ambazo zilisababisha hata kuondoa utulivu na kuharibu baadhi ya vyombo vya usafiri Jijini Dar es Salaam

Tukiwa katika ukumbi wa Tambaza ambao ni ukumbi wa miaka mingi wenye kujaza wanafunzi juu na chini mkuu wa shule aliyefahamika kama mwalimu Julius Mushi alisimama na kuukarisha ugeni huo na yeye alimualika Afisa Elimu wa Jiji Ndugu Abdul Mbegu.

Utambulisho uliendelea huku ukumbi ukiwa kimya kwani ugeni huu mkubwa, huku baadhi ya wanafunzi watukutu wa Tambaza wakidhani kuwa linakuja Karandinga (lori la Polisi la kubeba wahalifu) la Polisi kuwachukua wanafunzi wote na kuwapeleka Kituo cha Kati kutokana na vurugu. Huku shule nzima ikiwa imezungukwa na polisi wenye silaha.

Huku baadhi yetu tukidanganya kuwa tunakwenda chooni nao polisi wakiwa kila kona wakisema rudini ukumbini.

Sasa akakaribishwa Ditopile Mzuzuri ambaye alikuwa ndiye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Alisimama na suti yake ya rangi ya kaki ikiwa na mifuko mifuko mingi akasema

“Mambo! Hamjambo! Mimi ndiye Ditopile Ukiwaona Ramandhani wa Mzuzuri ambaye nimewahi kusoma Tambaza…” Ukumbi ulilipuka kwa makofi miluzi na huku Dj akicheza wimbo wa Buffaloo Soldier-Bob Marley.

Hapo ukumbi wote ulianza kuucheza wimbo huo Ditopile naye akiungana na wanafunzi hao kwa sekunde chache kuucheza muziki huo wa rege. Mkuu wa Mkoa alitambulisha viongozi wengine wa mkoa huo akiwamo RPC wa Dar es Salaam Afande Typhoni Maji.

Ditopile alilisisitiza umuhimu wa shule na akamkaribisha Mheshimwa Waziri wa Mambo ya Ndani Augustino Lyatonga Mrema akaanza kuzungumza kwa lafudhi ya kichaga. Aliyazungumza mengi likiwamo suala la kutumia muda wa shule kusoma huku akisema kuwa serikali italifanyia kazi tatizo la usafiri wa wanafunzi katika Jiji la Dar es Salaam.

“Mimi sitaki kuona wanafunzi mnagombana na makondakta wa Chai Maharage nataka msome kwa bidii huu mgogoro leo utamaliziki.”

Alipomaliza kuzungumza alitoa nafasi ya kuulizwa maswali na mwanafunzi wa kwanza ambaye jina silikumbuki alimuuliza juu ya idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kupanda katika Chai Maharage moja.

Katika kulijibu swali hilo Ndugu Mrema alimnyanyua RPC Maji kwanza alimuuliza idadi ya abiria wanaojaza chombo hicho alafu alipojibiwa akasema

“Haya mambo yanatakiwa hekima tu kwani kama kuna abiria wengi angalau wanafunzi 10 lakini hakuna abiria kwani muwaache wanafunzi? ” Huku akiulizwa tena juu wanafunzi kuketi katika viti hivyo, Ndugu Mrema akisema kuwa siyo hekima mtu mzima kusimama nawe mwanafunzi umekaa katika kiti.

Aliulizwa swali lingine juu ya basi ndogo zilizokuwa zinabeba abiria kutoka Msimbazi hadi Muhimbili (town hiace) kwamba wanafunzi wa Tambaza wanapata tabu wanakataliwa kupanda. Ndugu Mrema alimnyanyua RPC Maji akamuuliza namna hizo Town Hiace zilivyo. Alipomaliza kujibiwa na RPC Maji aliagizwa kila Town Hiace iwe na kiti nyuma ya kiti kwa mgongo wa dereva na kiwe kiti cha wanafunzi watano na viti vingine waketi abiria. Hapa RPC Maji aliagizwa kulisimamia na lilitekelezwa.

Ndugu Mrema aliuzwa swali lingine juu ya mabasi ya mashirika ya umma kuwachukua wanafunzi waliokuwa wakiingia mchana maana kulikuwa na makundi mawili wiki asubuhi kundi A kundi B mchana yakipokezana mchana, asubuhi, mchana asubuhi.

Kweli zoezi hilo nalo lilifanyika ambapo mabasi hayo yalitakiwa kusimama karibu na Azania, Jangwani sekondari pia Elimu Kwa Njia Ya Posta

Katika kikao hicho huku Ndugu Mrema akishangiliwa na wanafunzi, alitoa siku saba kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam Afande Typhoni Maji kuhakikisha yote aliyoagiza yanakamilika na baada ya siku hizo  wanafunzi tulisafiri kwa utaratibu huo.

Mwanakwetu yote yalitekelezwa na ndiyo maana siku hizi hiace zote zina kiti hicho nyuma ya mgongo wa dereva. Hiace zilianza kubeba abiria ambapo wakati huo nchini nzima Hiace zilikuwa ni Msimbazi-Muhimbili tu.

Naweka kalamu yangu chini kwa siku ya leo kwa swali moja tu, je wewe ukiondoka katika nafasi hii uliyonayo leo utakumbukwa kwa lipi? Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.