Habari za Punde

Kutengana kwa wanandoa huchangia athari kubwa kwa watoto ya kukosa malezi na makuzi bora


Mratibu wa Jinsia Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Ofisi ya Makao makuu Dodoma Florence Chaki  akiwasilisha mada ya udhalilisha,wakati wa mafunzo na majadiliano dhidi ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto, huko UKumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.
Viongozi wa Dini,Wazazi na Waratibu wa kupinga vitendo  vya Udhalilishaji wakifuatilia mjadala na mafunzo kuhusu udhalilishaji yaliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Tanzania yaliyofanyika ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.

Mjumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa  Magharibi "B" akichangia mada kuhusu udhalilishaji katika mafunzo na majadiliano dhidi ya  ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto ,yaliyofanyika Ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.
Mjumbe kutoka Jumuiya ya walimu wa Madrasa Bimkubwa Khamis akichangia mada katika majadiliano juu ya udhalilishaji yaliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora huko Ukumbi wa maleria Mwanakwerekwe Zanzibar
Kiongozi wa Dini kutoka KKKT Mwanakwerekwe Benjamini Sudayi akichangia mada katika majadiliano kuhusu udhalilishaji yaliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora katika ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar

 SR. Odilia akichangia mada kuhusu ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto katika mafunzo na majadiliano yaliyofanyika ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.

 

Mwenyekiti mtendaji Taasisi ya Waratibu wa kupinga  vitendo vya udhalilishaji Amina Yussuf  Ramadhan akichangia mada kuhusu ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto katika mafunzo na majadiliano yaliyofanyika ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.


PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR


Na  Khadija Khamis –Maelezo,   14/10/2021.


Kamishna wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Amina Thalib Ali amesema kutengana kwa wanandoa huchangia athari kubwa  kwa watoto ya kukosa malezi na makuzi bora  katika familia zao.


Amesema majukumu ya malezi huachiwa akinamama pekee jambo ambalo huwa vigumu   kuzifuatilia nyendo za watoto wao kutokana na harakati maisha  .


Aliyasema hayo katika Mafunzo ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora katika ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe, ambayo yaliwashirikisha Viongozi wa dini  na  Waratibu wa kupinga vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto .


Aidha alisema vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto vinazidi  kuongezeka siku hadi siku jambo ambalo linapoteza nguvu kazi wa taifa la kesho kwa kuzipoteza ndoto zao.


Alifahamisha kuwa Ofisi za Tume hiyo ziko wazi kwa yeyote mwenye malalamiko awapelekee iwapo ana kesi ambayo taratibu zake zinachelewechwa ni kujuwa kwamba hapo kuna  haki ya mtu inataka kupotezwa.


“Hicho kilio ni chetu sote iwapo kuna kesi iko polisi au  kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na hata mahakamani ambayo taratibu zinacheleweshwa haiyendi hairudi  na watoaji wa haki wapo wamewekwa na wanalipwa kwa kazi hiyo, hapo kuna haki ya mtu inataka kupotezwa njoo tusaidiane kwenye hili janga usikate tamaa.” alisema Kamishna Amina.


 Nae Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Methew P.M. Mwaimu amesema licha ya jitihada za serikali na wadau mbalimbali, kupiga vita vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia na watoto, jumla ya kesi 868 zilizoripotiwa kutoka Zanzibar jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya taifa.


Amesema taarifa za ongezeko la vitendo vya udhalilishaji kwa watoto hususan wa jinsia ya kiume ni kubwa kwa Zanzibar jambo ambalo  linaashiria  maisha ya watoto kuwa hatarini.


Mwenyekiti  huyo amesema tume ya haki za binaadamu na utawala bora imeona kuna umuhimu mkubwa wa wadau kuongeza jitihada ya kutoa elimu ili kuengeza uelewa wa masuala ya haki za binaadamu na utawala bora kwa makundi mbali mbali ya umma.


Pia amesema viongozi wa dini na wanaharakati wakupinga udhalilishaji waliopata mafunzo hayo ni chachu katika jamii ya kuwaelimisha wengine mifumo sahihi ya kutoa taarifa na kudai haki zao.


Aidha alisema Tume inaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za wanawake na watoto zinalindwa zinatunzwa,na kutetewa kote nchini.


Kwa upande wa wanaharakati hao wamesema elimu zaidi inahitajika katika jamii kwa kuhakikisha watoto wanafundishwa miongozo ya dini, kuachana na tabia za kuiga wanamuziki hasa katika vivazi ambavyo sio sahihi,jamii iache tabia ya kumuamini kila mtu kwa kumuachia mtoto ,pamoja na watuhumiwa kuachiliwa kiholela kunachangia vitendo vya udhalilishaji jambo linalorudisha wahanga wa udhalilishaji.


Kauli mbiu ya Tume hiyo ni“ PAZA SAUTI KOMESHA UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA DHIDI YA WATOTO”  No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.