Habari za Punde

Maadhimisho ya siku ya Afya ya akili yafanyika Mnara wa kumbukumbu Michenzani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipokea maandamano ya wahudumu wa Afya pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Afya (ZSH) katika maadhimisho ya siku ya Afya ya akili yaliofanyika katika viwanja vya Mnara wa Kumbukumbu – Michenzani.
 Mratibu wa Huduma za Afya ya Akili Suleiman Abdu Ali akielezea changamoto wanazokabiliana nazo katika majukumu yao ikiwemo changamoto ya bajeti pamoja na usafiri wakati akisoma risala katika maadhimisho ya siku ya Afya ya akili yaliofanyika katika viwanja vya Mnara wa Kumbukumbu – Michenzani.
Mwakilishi kutoka Oakland University Dk. Christina akilezea faraja yake juu ya jitihada zilizochukuliwa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha Afya ya akili ikiwemo kujengwa kwa jengo zuri la kutolea huduma za Afya ya Akili Kidongo chekundu.

 Mhe. Hemed akihutubia wananchi pamoja na watendaji wa Afya katika maadhimisho ya siku ya Afya ya akili yaliofanyika katika viwanja vya Mnara wa Kumbukumbu – Michenzani.


Na Kassim Issa OMPR

Jamii imeshauriwa kujenga utamaduni wa kuvitumia vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya pamoja na Hospitali ya rufaa ya Kidongo Chekundu wanapopatwa na shida ya aikli ili kupata matibabu stahiki.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa wito huo katika maadhimisho ya siku ya afya ya akili duniani hafla iliyofanyika katika viwanja vya Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi - Michenzani.

Alisema jamii inapaswa kutumia haki yao ya msingi ya kupata matibabu kwa kufika katika vituo vya afya na kuachana na dhana ya imani potofu ya ushirikina .

‘’Naomba mtumie haki yenu ya kuwa na afya njema, haki ambayo inapatikana katika taasisi za Serikali nilizoziainisha na zinapatikana bila ya malipo’’ Alieleza Mhe. Hemed

Mhe. Hemed alisema kwa mujibu wa ripoti mbali mbali za Shirika la Afya Duniani kupitia machapisho yake bado kuna changamoto ya ufinyu wa bajeti kwa ajili ya kutibu afya ya akili ambapo Serikali mbali mbali duniani huelekeza wastani ya asilimia 3% tu kwa ujumla wake kwa ajili ya huduma za afya ya akili.

Alisema katika kukabiliana na changamoto hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza uwekezaji katika huduma ya afya ya akili tangu mwaka 2000 ambapo Serikali ya Awamu ya Saba kwa mashirikiano na nchi ya Norway wamejenga hospitali maalum ya kidongo chekundu kwa ajili ya matibabu ya fya ya akili.

Pia alisema Serikali katika kutoa msukumo tayari imeshapeleka wataalamu saba kusomea fani mbali mbali ya matibabu ya afya ya akili ndani na nje ya nchi wakiwemo madaktari bingwa wanne (4) na wanasaikolojia watatu (3)

Mhe. Hemed alifafanua kuwa Serikali ina mpango wa kuwezesha kulazwa hospitiali watoto wenye matatizo ya afya ya akili wenye umri kati ya miaka saba (7) hadi minane (8) mara baada ya jengo jipya litakapokamilika na kufunguliwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa takwimu zinaonesha magonjwa ya akili yanachukua nafasi ya kumi na tatu (13) miongoni mwa magonjwa makuu yanayotikisa ulimwengu ambapo kila penye watu wanne basi mtu mmoja ameweza kuugua tatizo la afya ya akili maishani.

Akisoma risala kwa niaba ya wahudumu wa afya ya akili mratibu Suleiman Abdu Ali alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa bado huduma za afya ya akili zinaathiriwa kutokana na utofauti wa mitazamo ndani ya jamii hali ambayo inasabaisha kuendelea kwa tatizo la unyanyapaaji wa wagonjwa akili.

Aidha mratbi Suleiman alisema wafanyakazi wa huduma za afya ya akili wanaipongeza Seriklai ya Awamu ya Nane kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha huduma za afya ya akili kupitia vituo mbali mbali vilivyomo katika Wilaya pamoja na hospitali ya kidongo chekundu.

Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo alibainisha changamoto hizo ni pamoja na udogo wa bajeti usiokidhi kufikia malengo, changamoto ya usafiri, unifomu pamoja na changamoto ya mgongano wa sheria.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Oakland University Dk. Christina alisema ushirikiano wa pamoja kati ya SMZ na Norway katika huduma za afya ya akili ulioanza 2011 umezaa matunda kutokana na kujengwa jengo zuri la kutoa huduma za afya ya akili hapa Zanzibar liliopo katika eneo la Kidongo Chekundu

Maadhimisho ya siku ya afya ya akili duniani huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 10, kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema ‘’AFYA YA AKILI KATIKA ILIMWENGU USIO SAWA’’

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.