Habari za Punde

Masheha Wilaya ya Kaskazini "B" Unguja Watakiwa Kuweka Mpango Mkakati Kuwarejesha Watoto Skuli.

Na Maulid Yussuf WEMA  

Mkuu wa Wilaya ya kaskazini B' Unguja Ndg.Hamid Seif Said amewataka Masheha wa Wilaya hiyo kuweka mpango Mkakati  ili kuhakikisha wanawarejesha watoto Skuli walionje ndani ya mwaka mmoja.

Amesema ni lazima kuhakikisha wanaweka historia juu ya mradi huo kwa kukamilisha kazi hiyo kwa muda huo badala ya miaka mitatu iliyowekwa na mradi.

Akizungumza wakati alipofungua mkutano wa kutoa uelewa juu ya Mradi wa kuwarejesha watoto Skuli, kwa Masheha na Wajumbe wa Masheha, katika Ukumbi wa Mkutano wa Baraza la Mji Kaskazini B' Kinduni amesema, ni jambo la kusikitisha kuona ndani ya Wilaya  hiyo kuna watoto 2485 walio nje ya mfumo rasmi wa masomo ambao ndio Tegemeo la Taifa.

Amesema hali hiyo itawezekana endapo watafanya kazi pamoja na kushirikiana ili kuhakikisha wanaleta umoja na ustawi wa haki kwa maendeleo ya pamoja kama inavyoeleza katiba ya nchi.

Aidha amewataka watendaji hao kuhakikisha wanatekeleza jukumu hilo kwa kila mmoja kwa nafasi yake, kuishajiisha jamii kuwatoa watoto jwa kufuata trtibu, sheria na miongozo, ili lengo la mradi huo liweze kufikiwa.

Nae Mkurugenzi Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima bi Mshavu Ahmada Fakih amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shurika la UNICEF, ni idadi kubwa sana ya watoto walio nje ya masomo ambayo ni 35 elfu 732 kwa Zanzibar nzima, hali ambayo wakiachiwa inaweza kuleta athari kubwa nchini.

Ametaja baadhi ya athari hizo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa jamii isiyojua kusoma na kuandika hali ambayo Serikali imefanikiwa kwa asilimia kubwa katika kuielimisha jamii, pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji vya watoto.

Amesema kutokana na kuwa Masheha na wajumbe wa Masheha kuwa karibu zaidi na jamii ni vyem kuwafichua watoto hao na kuwaelimisha wazazi wa watoto hao ili kuhakikisha wanawarudisha Skuli ili  kupata haki yao ya msingi kikatiba, pamoja na kuwaokoa na majanga mbalimbali.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo bw Mzee Shirazi Hassan amesema kufanikiwa kwa mradi huo, kutatua tatizo la ajira za watoto, utoro Maskulini na hivyo kuchangia kuingezeka kwa ufaulu wa watoto ambao ndio sababu ya kupata wataalmu nchini.

Nao Masheha na Wajumbe wa shehia wakitoa maoni yao wamesema wana kazi kubwa kutokana na baadhi ya wazazi hasa walio katika kaya maskini kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa kuwa na uoga wa kushtakiwa kutokana na kutowapeleka watoto wao Skuli.

Aidha wameeelezea wasiwasi wao juu ya kuwadhibiti watoto watakaofanikiwa  kuwarejesha Skuli kwa kuwafanya kuendelea na masomo yao vizuri,  sambamba na kuwaomba kutafakari sababu zilizowapelekea watoto kutoroka Skuli  na kuzifanyia kazi ili kuhakikisha hazijitikezi tena.

Hata hivyo wameshauriana kutoa ushirikiano wa dhati kwa Serikali yao juu ya suala hilo kwa kuweka uzalendo ili kuokoa watoto wao ambao ndio tegemeo kubwa la Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.